28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Sumaye apinga Muswadawa Vyama vya Siasa


 Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

WAZIRI Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, ameitaka Serikali kuuondoa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa, kwa kile alichodai kuwa unaua demokrasia ambayo iko ndani ya Katiba ya nchi.

Muswada huo tayari ulishasomwa kwa mara ya kwanza bungeni na unasubiriwa kujadiliwa katika kikao kijacho cha Bunge.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Sumaye ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Pwani alisema kwa mtiririko wa mambo yalivyo kuna dalili kuwa muswada huo unakwenda kupitishwa na Bunge. 

“Serikali kama ni sikivu iondoe huu muswada kwa sababu unaua demokrasia ambayo iko ndani ya Katiba ya nchi. Kama haitaondoa tunaomba wabunge wote waupinge muswada huu,” alisema Sumaye.

Chama hicho pia kilisema bado kuna uhitaji wa kuwa na katiba mpya itakayoendana na mfumo wa demokrasia ya vyama vingi uliopo kwa sababu katiba ya sasa ina viraka vingi.

“Kama mchakato wa katiba ulioanzishwa haukuwa uamuzi sahihi ni vema wahusika wachukuliwe hatua za kisheria kwa ubadhirifu wa fedha za umma.

“Kama ulikuwa halali basi watawala wa sasa ama chama chao kiwalazimishe kuendelea nao au kiwawajibishe na kuwashitaki kwa ubadhirifu wa fedha za umma,” alisema.

Sumaye pia aliitaka Serikali kuhakikisha zoezi la uhakiki wa daftari la wapigakura linafanyika haraka badala ya kufanywa kama dharura ili kila mwananchi apate haki yake.

Katika hatua nyingine chama hicho kilisema kimeanza kuchangishana fedha kuongeza nguvu ya wanasheria katika kesi zinazowakabili wanachama na viongozi wake wakiwamo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.

Mbowe na Matiko ambao wanakabiliwa na kesi ya uchochezi inayowakabili pamoja na viongozi wengine saba wa chama hicho, walifutiwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Sumaye alisema wanataka haki itendeke haraka ili viongozi hao watoke gerezani waendelee na shughuli zao.

“Kanda ya Pwani kwa kuona kwamba mwenyekiti wa taifa yuko ndani tuliitisha mchango wa kusaidia jambo hilo na juzi tulipata Sh 800,000 za kuanzia.

“Iringa wanaendelea na michango hiyo na tutandelea kuongeza nguvu ya mawakili. Tunaguswa sana na matatizo yanayotupata na tunaendelea kushirikiana,” alisema Sumaye

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles