Suluhu Academy yapania ubingwa Chipukizi Cup

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

Timu ya soka ya vijana ya  Suluhu Academy’, imesema imejipanga kuchukua ubingwa katika michuano ya Afrika ya Chipukizi Cup yanayotarajia kuanza Desemba 11, 2023, jijini Arusha.

Mashindano hayo yanashirikisha timu nane zikiwamo Tanzania  Bara, Kenya, Afrika Kusini, Somalia, Rwanda, Uganda na Zimbabwe.

Kocha Mkuu wa  Suluhu Academy, Yussuf Ramadhani Khamis amewaambia waandishi wa habari leo Desemba 7, 2023 kuwa amekiandaa kikosi hicho kiushindani.

“Tumewaweka vijana wetu sawa kwenda kushindana, hivi ni vipaji vipya niwaambie watanzania waje kuwaona kina Samatta wapya,” amesema kocha huyo.

Naye mmoja wa viongozi wa benchi la ufundi, Msim Suluhu, amesema wanataka kuonesha wapenzi wa michezo kuwa wanaweza na lengo ni kuondoka na kombe katika michuano hiyo.

Kwa upande wake Mlezi wa kituo hicho,Otieno Igogo, ameeleza kuwa muasisi wa kituo ni Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kukuza na vipaji vya michezo nchini.

“Ameweza kuwajengea academy ambayo inawafundisha vijana michezo mbalimbali ili kwa pamoja kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tuweze kupaza sauti zetu kwa vitendo kwa michezo, hatimaye sifa ya Tanzania kimichezo iweze kufika kila kona ya dunia.

Amesema anaamini vijana hawatamuangusha katika mashindano hayo makubwa, ukizingatia yanafanyika nyumbani ni heshima kubakiza kombe nchini.

Aidha wadhamini wa timu hiyo, mwakilishi wa kampuni ya Bin Slum, Idd Moshi amesema wamechamini ili kusapoti harakati za Rais Samia za kukuza vipaji vya michezo.