33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Sultan Qaboos wa Oman afariki dunia, binamu yake Haitham atangazwa kumrithi

MUSCAT, OMAN 

SULTANI Qaboos bin Said wa Oman aliyeitawala nchi hiyo kwa karibu nusu karne amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 79.

Shirika la habari la taifa hilolimeripoti kuwa Qaboos ambaye amekuwa sultan wa Oman tangu mwaka 1970 baada ya kumpindua baba yake, amekuwa mgonjwa kwa muda mrefu na inaaminika alikuwa akitibiwa saratani ya utumbo.

Kutokana na  kifo chake Serikali imetangaza siku tatu za maombelezo ya taifa na bendera zitapepea nusu mlingoti kwa muda wa siku 40.

Qaboos aliyepata elimu yake nchini Uingereza alifanya magueuzi makubwa nchini Oman, taifa ambalo wakati akichukua madaraka lilikuwa na shule tatu pekee na sheria kandamizi zilizopiga marufuku nishati ya umeme, redio, miwani na hata matumizi ya miamvuli.

Chini ya utawala wake Oman ilikuja kufahamika kuwa eneo linapendelewa zaidi na watalii na taifa na zaidi kuonekana  kiungo kwenye eneo la Mashariki ya Kati.

Akiwa kiongozi wake Taifa hilo  limekuwa likisaidia Marekani kuwaokoa wanadiplomasia wake waliokamatwa mateka nchini Iran na Yemen na hata kuwakaribisha maofisa wa Israeli wakati huo huo yeye binafsi akipinga ukaliaji wa mabavu ardhi ya wapalestina.

MRITHI WAKE 

Haitham bin Tariq Al Said

Kifo cha sultani Qaboos awali kilisababisha wasiwasi mkubwa wa kutokea machafuko kwenye Taifa hilo la pembezoni ya rasi ya bara arabu lenye takribani raia milioni 4.6.

Sultani Qaboos ambaye hakuwa na mke wala watoto hakutaja hadharani mrithi wake.

Ingawa tayari serikali imetoa taarifa ikisema kuwa binamu yake Haitham bin Tariq Al Said amekwishaapishwa kama mrithi wake.

Haitham bin Tariq Al Said ambaye alikuwa Waziri wa Utamaduni na Thurathi za Kitaifa aliapishwa jana Jumamosi baada ya mkutano wa Baraza la Familia ya Kifalme, serikali imesema.

Kulingana na Katiba ya Oman familia ya sultani inapaswa kumtaja mrithi wa kiti hicho ndani muda wa siku tatu tangu kinapotangazwa kuwa wazi.

Iwapo familia itashindwa kuafikiana kuhusu jina la yule anakayechukua wadhifa huo, mtu aliyeteuliwa na Qaboos kupitia barua kwenda kwa familia yake ndiye atakuwa mrithi wa kiti cha usultani.

Katiba ya Oman inameanisha kuwa sultani anapaswa kuwa sehemu ya familia ya kifalme, muumini wa dini ya kiislamu, mtu mzima, timamu na mtoto halali wa wazazi waislamu wa Oman.

MRITHI WAKE

Awali Wataalamu walibashiri kuwa kulikuwa kuna zaidi ya watu 80 wenye sifa za kumrithi sultani Qaboos.

Aliyetajwa zaidi alikuwa ni Asad bin Tariq mwenye umri wa miaka 65 ambaye mwaka 2002 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya kimataifa na mahusiano ya kigeni.

Wengine waliotajwa awali ni binamu wawili wa Sultan Qaboos, Haitham bin Tariq ambaye ni Waziri wa Utamaduni na  Shihab bin Tariq aliyekuwa mshauri wa karibu wa Qaboos.

HUYU NDIYE SULTAN QABOOS

Sultan Qaboos alitawala siasa za Oman kwa karibu miaka 50

Sultan alimng’oa madarakani baba yake katika mapinduzi ya amani kwa ushriikiano na Uingereza mwaka 1970 na kuiweka Oman katika mwanzo mpya wa maendeleo kwa kutumia utajiri wake wa mafuta.

Alikuwa maarufu sana na yeyote aliyejitokeza kumpinga alinyamazishwa.

Sultan ndio mwenye kufanya maamuzi nchini Oman. 

Pia anashikilia wadhifa wa waziri mkuu, amiri jeshi mkuu, waziri wa ulinzi, waziri wa fedha na waziri wa mambo ya nje. 

TAARIFA ZA KIFO CHAKE

Mwezi uliopita, Sultan Qaboos – ambaye hakuwa na mrithi ama mtu aliyekuwa ameteuliwa kuchukua nafasi yake – alikuwa nchini Ubelgiji kwa wiki nzima akipata matibabu na kulikuwa na taarifa kwamba anaugua saratani.

“Kwa huzuni na masikitiko makubwa…familia ya kifalme inaomboleza kifo cha Mfalme Sultan Qaboos bin Said, ambaye alikufa Ijumaa,” taarifa kutoka familia ya kifalme ilisema, na kutangaza siku tatu za maombolezo.

Picha zilionyesha kundi la wanaume waliokusanyika nje ya msikiti mkuu wa Sultan Qaboos mji mkuu wa Muscat, ambapo jeneza lake lilipelekwa kwa ajili ya maombi maalum.

SULTANI Qaboos bin Said wa Oman

SERA ZA SULTAN QABOOS 

Kwa kipindi cha miaka 50, Sultan Qaboos ametawala siasa za Oman, nchi yenye idadi ya watu milioni 4.6 huku takriban asilimia 43 wakiwa ni kutoka nchi nyingine.

ALIVYOMPINDUA BABA YAKE

Akiwa na umri wa miaka 29, Sultan Qaboos alimpindua mamlakani babake, Said bin Taimur, mfalme huyo aliyekuwa na msimamo mkali alipiga marufuku mambo kadhaa ikiwemo kusikiliza redio ama kuvaa miwani ya jua na kuamua nani atakaye oa, kupata elimu au kuondolewa nchini humo.

Sultan Qaboos alimngoa babake madarakani katika mapinduzi ya amani mwaka 1970

Mara moja Sultan Qaboos alitangaza kwamba anataka kuunda serikali ya kisasa na kutumia fedha alizopata kwa utajiri wake wa mafuta kuendeleza nchi hiyo wakati ambapo ilikuwa na barabara nzuri ya umbali wa kilomita 10 tu na shule tatu pekee.

Miaka ya kwanza ya utawala wake, kwa usaidizi wa vikosi maalum vya Uingereza, alifanikiwa kukandamiza wanamgambo wa eneo la kusini la Dhofar la watu wa makabila yaliyoungwa mkono na Jamhuri ya Yemen.

Akielezewa kama mtu aliyekuwa na kipaji na maono, Sultan Qaboos aliamua kuchukua msimamo wa kutounga mkono upande wowote katika masuala ya mambo ya nje na alifanikiwa kufanya mazungumzo ya siri na Marekani na Iran mwaka 2013 ambayo yalipelekea kufikiwa kwa makubaliano ya kihistoria ya nyuklia miaka miwili baadaye.

UTAWALA WAKE 

Hali ya kutoridhishwa na utawala wake ilijitokeza mwaka 2011 wakati wa vuguvugu la Mapinduzi ya Arabuni.

Oman haikushuhudia msukosuko mkubwa lakini maelfu ya watu walikusanyika barabarani kote nchini humo wakidai mishahara ya juu, nafasi zaidi za ajira na kumalizwa kwa ufisadi.

Pamoja na malalamiko hayo akitumia utajiri wake wa mafuta, Sultan Qaboos aliigeuza Oman kuwa ya kisasa na kuendeleza ustawi wa watu wake.

Awali, vikosi vya usalama vilivumilia maandamano hayo lakini baadaye vikaanza kutumia gesi ya kutoa machozi, risasi za mpira na kufyatua risasi hewani ili kutawanya waandamanaji.

Watu wawili waliuawa na makumi ya wengine wakajeruhiwa.

Pia mamia ya wengine walishtakiwa kwa makosa ya uhalifu, kufanya mikusanyiko ya pamoja kinyume cha sheria na kumtukana sultan.

Hata hivyo maandamano hayo hayakufanikiwa kuleta mabadiliko makubwa japo Sultan Qaboos alichukua hatua ya kuwaondoa madarakani mawaziri kadhaa waliokuwa wamehudumu kwa muda mrefu kwa madai ya ufisadi, akaongeza nguvu ya Baraza la Ushauri na pia akaahidi kuunda nafasi zaidi za ajira katika sekta ya umma.

Kulingana na Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch tangu wakati huo, mamlaka imekuwa ikiendelea kuzuia magazeti na majarida yanayojitegemea yanayokosoa serikali, kuchukua kwa nguvu vitabu vinavyoonekana kupinga utawala na kuwanyanyasa wanaharakati,.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles