31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

SUGU: TUNAHITAJI BAJETI RAFIKI KWA WATANZANIA

Na PENDO FUNDISHA-MBEYA


MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Chadema), amewatoa hofu wakazi wa Jiji la Mbeya kwa kuwahakikishia kwamba Bunge la bajeti litakaloanza vikao vyake mwaka huu, limejipanga katika kupitisha bajeti rafiki itakayosaidia kupunguza makali ya maisha ya Watanzania.

Sugu aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na wananchi wa Jiji la Mbeya katika viwanja vya mikutano vya Shule ya Msingi ya Mwenge, eneo la Soweto jijini hapa.

Alisema Bunge limejipanga katika kusimamia uchumi wa nchi pamoja na masilahi ya Watanzania hasa katika suala zima la ajira na biashara kwa wajasiriamali.

“Uchumi wa nchi usipokaa sawa, hakuna mafanikio yanayopatikana, kwani ikumbukwe kwamba mafanikio ndiyo silaha ya maisha kwa mwananchi mmoja mmoja, hivyo ni lazima hili likaangaliwa na kutafutiwa ufumbuzi,” alisema.

Alisema bajeti rafiki ndiyo inayohitajika kwa Watanzania kuweza kutoa ajira kwa vijana na kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri ajira za Serikali ambazo hadi sasa Serikali imesimamisha zoezi hilo na kuwafanya wahitimu wa vyuo kuendelea kubaki mitaani.

Mbunge huyo aliongeza kwamba kwa hali ya nchi ilipofikia, ni mbaya hivyo wao kama wabunge wataangalia njia mbadala ya kuishauri Serikali.

“Bunge litasimamia taratibu bila kujali masilahi ya vyama, lengo ni kuhakikisha mambo yanakaa kwenye mstari ikiwa na muhimili huu muhimu wa bunge kuweza kuheshimika,” alisema.

Hata hivyo, Sugu aliwataka wakazi wa Jiji la Mbeya hasa vijana kubadilika na kuachana na tabia za kuwashabikia viongozi ambao wamekuwa wakiendesha mambo kisiasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles