NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MBUNGE wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu, amesema kifo cha mama yake Desideria Mbilinyi (62), kilisababishwa na mshtuko baada ya yeye kuhukumiwa kifungo cha miezi mitano jela.
Sugu aliyasema hayo jana katika Kanisa Katoliki  ndani ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dar es Salaam, wakati wa akisoma wasifu wa mama yake.
Alisema kabla ya tukio hilo mama yake alikuwa hasumbuliwi na magonjwa yoyote.
Alisema baada ya mama yake kupata taarifa za mwanaye kuhukumiwa, aliamini kwamba alionewa na baada ya hapo akapatwa na shinikizo la damu (BP) na baadaye figo kutokufanya kazi sawasawa.
“Mama yangu alianza kuugua nilipohukumiwa jela wiki ya kwanza tu, awali hakuwa na magonjwa hayo licha ya kwamba kufa kumeumbiwa mwanadamu.
“Mama aliamini mwanawe alikuwa ameonewa, akaanza kuugua na kupelekwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya  Februari na Julai mwaka huu ndipo alipata rufaa na kuletwa Muhimbili baada ya hali yake kuendelea kuwa mbaya,’’alieleza Sugu.
Alisema alizaliwa Desemba 25 mwaka 1956 na kufariki dunia Agosti 26 mwaka huu.
Pia alisema mama yake alikuwa mjane tangu mwaka 1992 na hakutaka kuolewa tena kwa kuwa aliamua kulitumikia Kanisa mjini Mbeya.
Alisema marehemu ameacha watoto watano wa kuwazaa na wawili aliachiwa na marehemu mumewe.
Mbunge huyo pia aliwashukuru madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, madaktari wa Taasisi ya Jakaya Kikwete, Muhimbili na majirani zake wa Mkoa wa Dar es Saalam.
Naye Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, alisema licha ya kuwa kufa kupo na ni lazima kwa mwanadamu, kifo cha mama yake Sugu kilisababishwa na kifungo cha kuonewa  mwanawe.
“Unapompoteza mzazi wa kike ni sawa umepoteza ubavu mmoja, kifo cha mama Sugu kimeniuma sana na malipo ni hapa hapa duniani,’’alisema Halima.
Misa ya kuaga mwili wa marehemu iliyoanza saa 4.00 asubuhi ikiogozwa na Padri Ephraim Oghan wa Parokia ya Muhimbili.
Katika mahubiri yake, Padri Oghan alisema hakuna wa kuwafariji wafiwa zaidi ya mfariji mkuu ambaye ni Mungu pekee.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria misa hiyo ni   Meya wa Dar es Salaam Isaya Mwita, Mbunge wa Tarime vijijini, John Heche, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, Meya wa Ubungo, Boniface Jacob na mtoto wa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema, Fred Lowassa.
Pia wasanii waliohudhuria ni   Kala Jeremiah pamoja na Suma G.
Baada ya ibada hiyo mwili ulisafirishwa kwenda mkoani Mbeya kwa ajili ya mazishi yanayotarajia kufanyika Agosti 29 Â mchana.
Imeandaliwa na ASHA BANI, HALIMA ALLY, SALMA OMARY, MAGRETH MSANGI (TUDARCO).                                   Â