Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
MATUKIO mawili ya kuchanganywa miili ya marehemu yaliyotokea April 9 na Juni 20, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, yamewang’oa wakurugenzi wawili katika nafasi zao.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaesha, iliwataja waliosimamishwa kuwa ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Shirikishi, Dk. Praxeda Ongwenyo na Mkuu wa Kitengo cha Kuhifadhi Maiti wa hospitali hiyo, Dk. Inocent Mosha
Aligaesha alisema Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Profesa Lawrence Museru ametengua uteuzi wa wakurugenzi hao kupisha uchunguzi dhidi yao.
“Wameondolewa kupisha uchunguzi kutokana na kushindwa kusimamia vizuri wafanyakazi walioko chini yake na kusababisha kitengo cha kuhifadhi maiti kuchanganya maiti wakati wa kuzitoa kwa ndugu mara mbili katika kipindi kisichozidi miezi mitatu.
“Hali hiyo imesababisha usumbufu mkubwa kwa wafiwa na hospitali kwa ujumla,” alisema Eligaesha katika taarifa yake.
Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Museru, amemteua Mkuu wa Idara ya Radiolojia Dk. Flora Lwakatare, kukaimu nafasi ya ukurugenzi ya tiba shirikishi ambayo inasimamiwa idara ya mionzi na idara ya maabara.
“Amemteua pia Dk. Herbert Nguvumali kukaimu nafasi ya Dk. Mosha na wahudumu waliohusika katika matukio hayo wameondolewa katika chumba cha kuhifadhia maiti kuanzia jana kupisha uchunguzi dhidi yao,” alisema.
Alisema katika uchunguzi huo kamati maalumu imeundwa kuangalia kwa kina utendaji wa kitengo cha kuhifadhia maiti ili kutoa mapendekezo ya jinsi ya kurekebisha utendaji wa kitengo hicho matukio kama hayo yasijitokeze tena.