23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

SUA: Ni muhimu kupima udongo kabla ya kutumia mbolea

Eliya Kamwela Mtaalamu wa Udongo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA)
Eliya Kamwela Mtaalamu wa Udongo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA)

 Jonas Mushi, Dar es Salaam

TANGU Tanzania ipate uhuru serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuendeleza kilimo ambacho kwa kipindi kirefu kilikuwa kinapewa kipaumbele na kuchukuliwa kama uti wa mgongo wa Taifa.

Sera mbalimbali za kilimo zilianzishwa ili tu kuhakikisha kilimo kinapewa nafasi kubwa katika uzalishaji wa Tanzania.

Zitakumbukwa kauli kama Siasa ni kilimo, kilimo ni uti wa mgongo, kilimo kwanza zote hizo zilitamkwa mara nyingi na viongozi wa kitaifa pale wanapozungumzia kilimo.

Kauli hizo zilienda sambamba na kuanzishwa kwa vyama vya ushirika vya wakulima, bodi za mazao ya kilimo, mfumo wa ununuzi wa skakabadhi ghalani, pamoja na kuweka ruzuku katika pembejeo za kilimo.

Jitihada hizo za serikali zilionekana kuzaa matunda  na wakulima wengi wakaitikia wito wa kulima kisasa kwa kupanda kwa nafasi na kutumia mbolea za kupandia na kukuzia.

Hata hivyo elimu juu ya matumizi sahihi ya mbolea imekuwa haitiliwi mkazo kwani wakulima wengi nchini wanatumia mbolea kwa mazoea kwasababu tu wameambiwa watumie mbolea.

Eliya Kamwela ni Mtaalamu wa Udongo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilichopo Morogoro ambaye katika makala haya anaelezea umuhimu wa kupima udongo kabla ya kutumia mbolea.

Anasema wakulima wengi hawana tabia ya  kupima udongo ili kujua tatizo lililopo kabla ya kutumia mbolea za viwandani na kwamba wengi wamekuwa wakitumia mbolea kwa mazoea bila kujua tatizo la udongo.

Anasisitiza kwamba kila aina ya mbolea ina kazi ya kuongeza virutubisho vya aina fulani vilivyopungua katika udongo hivyo utumiaji holela wa mbolea hautamaliza tatizo la udongo.

“Kabla ya kutumia mbolea lazima ujue udongo wako umepungukiwa virutubisho gani ili uweke mbolea itakayoongeza virutubisho hivyo,” anasema Kamwela na kusisitiza:

“Utumiaji holela wa mbolea hautamaliza tatizo la udongo kwasababu inawezekana mbolea unayotumia kila mara haina virutubisho vilivyopungua kwenye udongo wako.”

Anafafanua kwamba mimea ina tabia ya kumaliza virutubisho vilivyopo katika udongo hivyo suala la kutumia mbolea haliepukiki bali lazima itumike kwa usahihi.

“Mimea ina tabia ya kumaliza virutubisho vingi kwenye udongo hivyo ni lazima kujua kwanza ni aina gani ya virutubisho inakosekana ili uweke mbolea sahihi.”

Anasema SUA ni moja ya Taasisi inayofanya vipimo vya udongo kwa gharama nafuu ambayo mkulima mdogo anaweza kuimudu.

“SUA tunafanya kazi hii ya kupima udongo ambapo tunapima  vipimo 15 ambavyo kila kimoja kina gharama yake na jumla yake ni sh 45,000,” alisema Kamwela.

Anaongeza kuwa mkulima anayetaka kupima udongo anatakiwa kupeleka sampuli katika maabara ya Chuo hicho na kuchagua kipimo anachotaka kipimwe.

Baadha ya vitu ambavyo hupimwa katika udongo ni pamoja na phosphate, Nitrate, Haidrojeni,

“Mkulima akileta sampuli anachagua kupima kile ambacho pengine anahisi kimepungua katika udongo wake na kama hajui anaweza kuchukua vipimo vyote.

“Tukishagundua tatizo tunamshauri kuhusu aina ya mbolea anayotakiwa kutumia na kumpatia elimu juu ya matumizi endelevu ya udongo,” anasema.

Anatahadharisha kwamba ili kupata sampuli sahihi itakayowakilisha udongo wa shamba zima ni vyema wakulima wakawatumia wataalamu wa udongo wakiwemo maofisa ughani wanaopatikana katika maeneo yao.

“Wakulima wasijichukulie tu sampuli na kuileta maabara kwani anaweza asichukue udongo unaowakilisha shamba zima hivyo anashauriwa kutumia wataalamu wa kilimo wa halmashauri au wilaya au maofisa ughani wa maeneo husika,” anasema Kamwela.

Anashauri pia wakulima kupima maji hususani ya visima na marambo kabla ya kuyatumia katika kilimo cha umwagiliaji.

Anasema kutokana na umuhimu wa kupima udongo na maji ni vyema serikali iwekeze upya kwenye maabara zake za kilimo ambazo zipo lakini hazina vifaa ili wananchi wapate huduma hiyo kwa urahisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles