27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

STEVEN NYERERE MIKONONI MWA POLISI

NA TUNU NASSOR

-DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya kuanza kusambaa kwa sauti inayodhaniwa kwamba ni ya Msanii Steven Mengere maarufu kama Steven Nyerere, akizungumza na mama mzazi wa Msanii Wema Sepetu, mwigizaji huyo wa vichekesho anadaiwa kushikiliwa na polisi.

Kwenye sauti iliyosambaa juzi katika mitandao ya kijamii, wawili hao walizungumza mambo mbalimbali ambapo sauti ya mtu anayedhaniwa kuwa ni mama mzazi wa Wema, alikuwa akimuuliza mwigizaji huyo sababu za kutofika Kituo Kikuu cha Polisi kumsalimia mwanawe alipokuwa ameshikiliwa na jeshi hilo kwa siku saba akihusishwa na dawa za kulevya.

Kwa upande wa sauti ya mtu anayedhaniwa kuwa ni Steven, alijitetea kwa kusema alitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwamba akionekana polisi naye atakamatwa.

Alisema kutokana na hali hiyo, alilazimika kwenda mjini Dodoma kuonana na wabunge ili kuwashawishi wamtetee Wema jambo ambalo lilifanikiwa.

Jana Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, alipoulizwa juu ya kushikiliwa kwa msanii huyo na jeshi hilo, alisema: “Steven Nyerere kama ameitwa itakuwa ameitwa na wapelelezi.”

Bado sijapata habari zake kwa sababu kuna timu inashughulika na masuala haya, kwa hiyo kama ameitwa ni jambo jema kwani atahojiwa na baadaye uamuzi utatolewa aidha tuendelee kuwa naye ama apewe dhamana kwa hiyo kama ameitwa ni jambo jema.”

Katika sauti hiyo inayodhaniwa kuwa ni ya Steven Nyerere, mbali na kusema aliwashawishi wabunge kuibua mjadala wa suala hilo bungeni, pia aliwataja mawaziri kadhaa aliosema amefanya nao mazungumzo.

Pia alisema baadhi ya wasanii waliokamatwa kwa kuhusishwa na dawa za kulevya, waliachiwa baada ya kupewa fedha bila ya kufafanua zilikuwa za nini.

Katika hatua nyingine, Kamanda Sirro alisema hataacha kumwita Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, wakati wowote atakapokuwa anamhitaji kwa sababu ana uwezo huo.

 “Nina nguvu za kisheria na kimamlaka ya kumwita Mbowe na nitamwita tena na tena kumhoji,” alisema Kamanda Sirro.

Alisema pia kuwa jeshi hilo limewakamata watuhumiwa 257 kwa makosa ya kukutwa na dawa za kulevya katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.

“Watuhumiwa hawa wamekamatwa kati ya Februari 16 na 23 kutokana na msako unaoendelea kupiga vita uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya,” alisema Kamanda Sirro.

Alisema katika msako huo kete 1,526 za dawa za kulevya aina ya heroin, vidonge 112, misokoto 247 ya bangi pamoja na lita 372 za pombe haramu ya gongo zilikamatwa.

Katika hatua nyingine kikosi cha usalama barabarani cha kanda hiyo kimekusanya Sh 460,020,000 kama tozo na faini mbalimbali ya makosa ya barabarani kwa makosa 15,334 kati ya Februari 18 na 23 mwaka huu.

Kamanda Sirro alisema jumla ya magari 14,054 na pikipiki 1,280 zilikamatwa kwa makosa mbalimbali ya barabarani.

“Bodaboda waliofikishwa mahakamani kwa makosa ya kutovaa kofia ngumu na kupakia mishikaki ni 23,” alisema Kamanda huyo.

Aliongeza kuwa waendesha bodaboda 30 walikamatwa wakiendesha katika barabara ya magari yaendayo haraka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles