STARS INAKIBARUA KIZITO AFCON 2019

0
1342

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

TIMU ya soka ya Taifa, ‘Taifa Satrs’, inaweza kuwa na  kibarua kizito cha  kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, yanayotarajia kufanyika nchini Cameroon 2019, endapo hawatacheza kwa kujituma na kutambua wanacheza kwa maslahi ya Watanzania.

Taifa Stars imeanza vibaya mbio za Cameroon 2019 usiku wa jumamosi iliyopita, baada ya kulazimishwa sare ya nyumbani ya bao 1-1 na timu ya taifa ya Lesotho katika mchezo wa kwanza wa Kundi L uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam. 
Sare hiyo inaweza kuwa changamoto kwa Taifa Stars kupenya kwenye kundi L linalojumuisha timu za Uganda, Cape Verde na Lesotho kwani mshindi wa kila kundi katika makundi 12 atafuzu kucheza fainali hizo.

Licha ya Lesotho kutokuwa na rekodi ya kutisha lakini pia wanapaswa kuchukuliwa tahadhari kubwa katika mchezo wa marudiani kutokana na uwezo walioonesha mchezo wa awali na ukweli ni kwamba nchi nyingi za Afrika zilizokuwa chini katika kiwango cha soka zimekuwa na program endelevu ambazo zimepandisha soka lao.

Karata ya pili ya Taifa Stars itakuwa Machi mwakani kwa kupambana na Uganda jijini Kampala, Uganda kabla ya Septemba tena kukwaana na Cape Verde ugenini.

Septemba hiyo hiyo Stars watarudiana na Cape Verde nyumbani ambapo pia itakuwa kibaruani Oktoba kucheza na Lesotho ugenini na kumaliza nyumbani kwa kurudiana na Uganda.

Kwa mtazamo wa haraka  haraka kundi hilo lilikuwa likionekana kama jepesi sana hivyo kuipa nafasi kubwa Taifa Stars ya kufuzu.

Wengi wamekuwa na mtazamo kwamba timu ngumu ni zile zinazotoka kaskazini au Magharibi mwa bara hili zikiwamo Ivory Coast, Ghana, Nigeria, Senegal, Algeria, Moroco, Tunisia, Cameroon au Misri wakati ukweli halisi kwa sasa kila nchi imekuwa na mabadiliko makubwa sana katika soka.

Wachambuzi wa masuala ya soka hapa nchini wamekuwa wakiliangalia kundi hilo katika mtazamo kwamba iwapo jitihada zitafanyika ikiwa ni pamoja na mkakati unaotekelezeka basi Taifa Stars inaweza kwenda Cameroon katika fainali hizo.

Pamoja na mtazamo huo, ukweli halisi Taifa Stars ina kazi kubwa ya kufanya mbele ya Uganda, ‘The Cranes’, ambayo kikosi chake kimetengenezwa kutokana na mpango wa muda mrefu ambao uliwafanya kushiriki Afcon zilizofanyika nchini Gabon hivi karibuni.

Bado ugumu wa kufua dafu kwa The Cranes unaonekana hata unapokiangalia kikosi chake tu, kwani karibu chote kinaundwa na wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya Uganda ukilinganisha na Taifa Stars ambayo jicho lao ni kwa profeshno wawili tu yaani Mbwana Samatta anayecheza Genk ya Ubelgiji na Thomas Ulimwengu, AFC Eskilstuna ya Sweeden.

Lulu ya The Cranes ni wachezaji kama Forouk Miya (Standard League, Ubelgiji), Denis Onyango (Mamelodi Sundowns), Khalid Aucho na Geofrey Massa kutoka Baroka zote za Afrika Kusini), Luwaga Willian Kizito (Rio Ave, Ureno) na Robert Odongkara (St Geroge, Ethiopia), Magola Salim Omar (El Mareikh, Sufdan), na Azira Michael (Colorado, Marekani).

Wengine ni Juuko Murshid (Simba, Tanzania), Tony Mawejje (Thotur, Iceland), Sentamu Junior Yunus (Lives,Finland), Denis Iguma kutoka Al ahed na Hassan Mawanda Wasswa, kutoka Nijmeh zote za Lebanoon, Mosses Oloya wa Honoi T and T na Geofrey Kizito wa Than Quang Ninh zote za nchini Vietnam.

Lakini ukiangalia kikosi chao utagundua kwamba  ni The Cranes chini ya Milutin ‘Mitcho’ Sredojevic kimekuwa na mfumo mzuri ambao wachezaji wanaounda timu hiyo wamekaa kwa muda mrefu bila kubadilishwa tofauti na Taifa Stars ambao kila mara hubadilishwa kulingana na kocha anayeitwa kuifundisha.

Kumbukumbu ya kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa The Cranes katika michuano ya CHAN mwaka jana kinaweza kuwa somo tosha kwa watanzania wanaojiandaa kucheza na Uganda katika kuwania kufuzu Afcon 2019.

Wakati wadau wakijipa matumaini ya kufanya vizuri mbele ya Uganda wanapaswa kukiangalia kwa undani kikosi hicho.

Ukiachia nafasi waliyonayo Uganda katika ubora wa viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ambapo kwa miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakishika nafasi za juu ukilinganisha na Tanzania.

Watanzania kwa ujumla wanapaswa kuchukua tahadhari pia kwa Cape Verde ambayo bado Taifa Stars ina kumbukumbu ya kufungwa bao 1-0 mwaka 2008 wakati ikishiriki kuwania kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2010 Afrika Kusini.

Kufuzu kwa fainali zijazo za mwaka 2019 si kazi rahisi kama inavyofikiriwa na wengi kwa kigezo cha kutokuwapo kundi moja na timu za waarabu au yale mataifa yenye wachezaji wanaocheza ligi kubwa barani Ulaya, kinachotakiwa ni mikakakti.

Ni vema TFF kukutana na wadau ili kuweka mikakati itakayofanya timu kufanya vizuri katika michuano ambayo wengi wanaamini ina nafasi ya kufuzu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here