MWANDISHI WETU-KIGALI
TIMU ya Taifa Tanzania, ‘Taifa Stars’, leo itakuwa ugenini kuvaana na wenyeji wao, Rwanda ‘Amavubi’ , katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki utakaopigwa Uwanja wa Amahoro, Kigali.
Mchezo huo ni kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa(Fifa).
Benchi la ufundi la Stars chini ya Kocha Mkuu, Etienne Ndayiragije linataka kuutumia mchezo huo kujiimarisha kabla ya kuumana na Sudan katika mchezo wa marudiano kusaka tiketi ya kufuzu fainali za Mataifa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) utakaochezwa Oktoba 18, Uwanja wa Omdurman, Khartoum.
Timu hiyo itashuka dimbani kuikabili Rwanda, ikitoka kupokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Sudan, katika mchezo wa kwanza wa Chan uliochezwa Septemba 22, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mbali ya kutafuta mzuka wa kuivaa Sudan, Ndayiragije anataka kushindfa mchezo huo ili kupaa juu katika viwango ya ubora wa soka duniani.
Viwango vya ubora vilivyotolewa Septemba 19 mwaka huu, Tanzania ilishika nafasi ya 135, huku Rwanda ikishika nafasi ya 130.
Timu hizo zilipioumana mara ya mwisho ilikuwa katika michuano ya Chalenji ya Cecafa, ambapo Stars ililala kwa Rwanda mabao 2-1, mchezo uliopigwa Disemba 9, mwaka juzi jijini Kigali.
Rekodi za jumla zinaonyesha, timu hizo zimekutana mara 17, Stars ikishinda michezo sita, sare nne na kupoteza sita.
Mara ya mwisho Stars kuibuka na ushindi ugenini dhidi ya Amavubi ilikuwa Novemba 24, mwaka 2015.
Katika mchezo huo wa Chalenji ya Cecafa,Stars ilishinda mabao 2-1.
Hata hivyo, takwimu zinaonyesha katika michezo mitano ya mwisho ya timu hizo ambayo Stars ilikua ugenini, ilishinda mmoja pekee, ilipigwa mara mbili na kutoka sare mara mbili.
Amavubi kwa upande wake, ilishinda miwili , sare mbili na kuchapwa mmoja.
Stars inashikilia rekodi ya kushinda kwa idadi kubwa ya mabao katika michezo kati ya timu hizo.
Disemba 11, 2002, iliifumua Rwanda mabao 3-0, mchezo wa Chalenji ya Cecafa uliochezwa Uwanja wa Taifa(sasa Uwanja wa Uhuru), Dar es Salaam.
Mchezo wa leo utakuwa wa sita kwa Ndayiragije tangu akaimu nafasi ya Kocha Mkuu wa timu hiyo akirithi mikoba ya Emmanuel Amunike.
Ndayiragije atakuwa na kazi ngumu ya kusaka rekodi binafsi ya ushindi wa kwanza dhidi ya Rwanda.
Katika michezo mitano iliyopita ameiongoza Stars kutoka sare minne na kupoteza mmoja dhidi ya Sudan.
Tayari ameiwezesha Stars kutinga hatua ya makundi ya michezo ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2022, nchini Qatar, baada ya kuitupa nje Burundi kwa ushindi wa mikwaju ya penalti 3-0.
Timu hizo zilifikia hatua ya changamoto za mikwaju ya penalti, baada ya dakika 90 za mchezo wa kwanza na 120 za marudiano kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Ndayiragije alianza kuifurusha Kenya baada ya kikosi chake kuibuka na ushindi wa penalti 4-1, kabla ya kukutana na Sudan.
Lakini kabla ya penalti kutumika na kuivusha Stars, timu hizo zilitoka suluhu katika michezo yote miwili ya nyumbani na ugenini.
Akizungumzia mchezo huo, Ndayiragije Etiene alisema kikosi hicho kiko kamili kwa ajili ya kuhakikisha kinaichapa Rwanda kwao na kujenga hali ya kujiamini kuelekea mchezo wao wa Chan dhidi ya Sudan.
“Kila kitu kipo sawa kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Rwanda, tunafahamu umuhimu wa mchezo huu, ndiyo maana tumeweka msisitizo wa hali juu ili kile tulichopanga kuelekea mechi ya Sudan kipatikane.
“ Rwanda wana timu nzuri, ni kipimo kizuri kulingana na namna timu yao ilivyo, tumechagua tucheze ugenini ili kuwapunguzia presha wachezaji wetu, mkakati wa ushindi dhidi ya Sudan unaanzia hapa Kigali , tutahakikisha tunafanya kila tuwezalo ili kufanikisha mipango ya kupindua matokeo Khartoum na kufuzu Chan,” alisema Ndayiragije ambaye pia ni kocha wa Azam FC inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.