KLABU ya soka ya Stand United imesema kitendo cha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kusimamisha uchaguzi wa klabu hiyo ni mbinu ya kutaka kuhujumu uchaguzi wao uliotarajiwa kufanyika Juni 24 hadi Julai 3 mwaka huu.
TFF ilifikia uamuzi huo baada ya kutokea msuguano kati ya makundi mawili ndani ya klabu hiyo, ambayo ni Stand United Kampuni na Stand United Wanachama yaliyotaka kufanya uchaguzi wa viongozi wapya.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Dk. Jonas Tiboroha, alisema hakukuwa na sababu za msingi za kusimamisha uchaguzi huo kwa kuwa kati ya makundi hayo mawili, moja lipo kisheria na linatambulika na klabu kwa kuwa ni wanachama halali.
“Kundi la Stand Kampuni lenye watu 52 ndio wanachama halali wa klabu hii lilisajiliwa mwaka jana, lakini hao wanaojiita Stand United wanachama si wanachama halali wa klabu hii kinachotokea sasa wanatumika kuhujumu uchaguzi huu.
“TFF inajaribu kuingilia kati uchaguzi huu, kwa kuwa kuna watu wao ambao wana masilahi nao wanataka waingie ndani ya klabu hii ili kuivuruga, lakini jambo hilo halitawezekana,” alisema Tiboroha.
Hata hivyo, Tiboroha alisema kutokana na TFF kuvunja sheria mara kwa mara waliamua suala hilo kulifikisha Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ili kupata mwafaka na kuendelea na mchakato wao wa uchaguzi.
“Stand hakuna tatizo hata kidogo kwa kuwa kila kitu kipo wazi, TFF inachofanya ni kupindisha sheria na kanuni ambazo tumekuwa tukizitunga wenyewe ili zituongoze.
“Kuna kesi nyingi za malalamiko juu ya vitendo vya uvunjwaji wa sheria vinavyofanywa na TFF kutoka mkoa wa Tabora, Kigoma na Geita,” alisema.