Christopher Msekena
MIAKA mitatu iliyopita staa wa Hip hop, Boniventure Kabogo ‘ Stamina’, akiwa kwenye kazi zake alikutana na Veronica Peter, binti mwenye asili ya Kinyarwanda aliyekuwa anafanya mafunzo kwa vitendo (field) katika kituo fulani cha redio jijini Dodoma.
Mchizi alisaka mawasiliano ya mrembo huyo mpaka akayapata na hapo ndipo mapenzi yao yalipoanza na ndani ya muda mfupi yalifika hatua kubwa ya kutambulishana kwa ndugu zao ambao wengi wanaishi mkoani Morogoro.
Desemba 11, 2017, Stamina alipiga goti na kuuliza lile swali maarufu kwa kimombo, ‘Will you marry me?’ na akamvisha pete ya uchumba mrembo huyo tayari kuingia kwenye maisha mapya ya ndoa.
Mei 5, mwaka juzi alifanikiwa kufunga ndoa na Veronica katika kanisa la Mtakatifu Consolata huko SUA, Morogoro mbele ya wasimamizi wao ambao ni rapa Roma Mkatoliki na mke wake Nancy.
Kwa mujibu wa Roma anasema ndoa hiyo ilivunjika rasmi mwaka jana mwezi Februari baada ya mke wa Stamina kuondoka nyumbani licha ya kufanyika kwa vikao vingi vya ushuruhishi ndoa hiyo iliendelea kupumlia mipira.
Roma anasema ingawa Veronica kuwa na mapungufu ila Stamina naye alikuwa na matatizo yake ambayo ni kawaida kuwapo ndani ya ndoa nyingi kutokana wanandoa kuwa ni bi binadamu wenye madhaifu yao.
Mapema juzi, Stamina alichia ngoma yake, Asiwaze ambayo sasa hivi imeshika namba moja katika video zinazotazamwa zaidi YouTube. Ndani ya wimbo huo ametumia sanaa ya uandishi kuelezea matatizo ya ndoa yake huku akitaja usaliti ndiyo chanzo kikubwa cha kuvunjika kwa ndoa yake.
Stamina alimtumuhu mkewe kuchepuka na aliyekuwa mchezaji wa klabu ya Simba ambaye hakutaka kumuweka wazi jambo lililofanya ndoa yake kuvunjika ikiwa haijafikisha hata mwaka.
Katika hilo Stamina ametoa ushauri kwa vijana wanaotarajiwa kuingia kwenye ndoa pamoja na wazazi wenye watoto wenye mipango ya kufunga pingu za maisha.
“Mnavyoingia kwenye ndoa mnakutana watu kutoka familia tofauti, tabia tofauti, malezi tofauti mpaka kuja kuelewana na kuwa kitu kimoja inachukua muda, kwahiyo uchumba inatakiwa uwe mrefu angalau miaka mitano.
“Siyo mapenzi ya mbali yaani babe yupo Mwanza wewe upo Dar, mkikutana lazima utaigiziwa tu, utaona daaah mwanamke ana heshima huyu kumbe heshima yenyewe umeonyeshwa mara nne tu,” anasema Stamina.
Aidha Stamina aliongeza kuwa: “Wapenzi nawashauri wapate muda mwingi wa kuwa pamoja ili waweze kujuana, huyu ana tabia hii yule ana tabia ile harafu ikiwezekana wazazi waruhusu kabla ya ndoa watoto wakae hata mwaka tu ndani ili wasomane.
“Mimi sikuwahi kuishi naye kabla ya ndoa, tulikuwa tunakutana tu kisha anarudi nyumbani siyo ile pika pakua pika pakua ya muda mrefu ndiyo naama nashauri sana iwe hivyo sababu inasaidia kujuana vizuri.”.