29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Stamigold katika mafanikio ya miaka minne ya Rais John Magufuli

Stamigold; kielelezo cha wazawa wanavyoweza kuendesha kampuni

Na Mwandishi Wetu

STAMIGOLD ni kampuni pekee ya Kitanzania inayozalisha dhahabu kwa kiwango cha kati, ambayo inaendeshwa na Watanzania kwa asilimia 100.

Kampuni imejikita katika kuwaandaa wataalamu wazawa kwa kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wawapo vyuoni na wamalizapo masomo vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Stamigold imewapa kazi wakandarasi na wazabuni wazawa kwa kiwango kikubwa katika uendeshaji wa shughuli za uchimbaji na uzalishaji wa dhahabu nchini.

Mgodi awali ulikuwa ukimilikiwa na Kampuni ya Pangea Minerals, kupitia African Barrick Gold na Januari 2014 Shirika la Madini la Taifa (Stamico) lilikabidhiwa mgodi likiwa na hisa asilimia 99.99 na Msajili wa Hazina asilimia 0.11.

Stamigold ambayo ni kampuni tanzu ya Stamico, ni ya kitaifa inayokua, iliyolenga kuzalisha dhahabu kwa gharama nafuu na kuongeza rasilimali ya muda mrefu wa uwezekano wa biashara huku ikitengeneza fursa za ajira na kuwashirikisha wadau wote kwa maendeleo ya taifa.

Dira yake ni kuwa wazalishaji maarufu wa dhahabu kwa lengo la kuchangia katika uchumi wa taifa na kuwa mfano wa kuigwa sekta ya madini.

Ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli, Stamigold imefanya mapinduzi makubwa katika uzalishaji wa dhahabu.

Uangalizi wa karibu wa viongozi katika sekta hii, ni moja ya chachu zinazofanya menejimenti ya Stamigold na wafanyakazi wote, kuhakikisha wanaongeza tija ili kuweza kupata faida.

Ni katika hilo, Waziri wa Madini, Doto Biteko, anaonyesha kuridhishwa na jinsi Stamigold inavyojiendesha na kuweza kupunguza gharama za uzalishaji na kuanza kupata faida.

Ikiwa ni sehemu ya kuendelea kufuatilia sekta ya madini, Septemba 19, Waziri Biteko alitembelea mgodi wa Stamigold Biharamulo na kuridhishwa na uendeshaji wake.

Waziri wa Madini, Doto Biteko alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya mgodi huo.

Akizungumza mgodini hapo, Biteko anasema; “Stamigold Biharamulo Mine  inayomilikiwa na Stamico, yapo mambo mengi yamefanyika ambayo ni hatua kubwa, ambayo mgodi umechukua.

“Kwanza wameshusha sana gharama za uendeshaji, mwanzo walikuwa wanazalisha wakia moja kwa dola za Marekani 1,800 na kuiuza kwa dola 1,223, sasa uzalishaji wa wakia moja umeshuka mpaka dola 940.

“Tunaamini wataishusha pia mpaka ifike 800 ndipo ambapo tunaweza kupata faida kubwa, lakini wamefanya kazi kubwa kuhakikisha uhai wa mgodi unaweza kuendelea.

“Moja ya hoja inayofanya uendeshaji kuwa juu ni matumizi ya mafuta, tunatumia zaidi ya Sh bilioni moja kwa mwezi kwa ajili ya mafuta, tukipata umeme gharama itashuka, tutakuwa tunatumia Sh milioni 300, tutakuwa tumeokoa karibu Sh milioni 700.

“Wizara ya Madini imeshazungumza na Wizara ya Nishati na kabla ya hapo wakati ikiwa ni wizara moja (Wizara ya Nishati na Madini) mchakato uliokuwepo ni umeme unaotoka Rusumo kwenda Geita, tupate ‘line’ yetu ya megawati tatu ambayo itasambaza umeme kwenye mgodi huu na kushusha gharama za uendeshaji, mradi huu (wa umeme) unakamilika mwakani.

Shughuli za uchimbaji zikiendele katika mgodi wa Stamigold

“Kwa wafanyakazi wa mgodi tunapongeza jitihada zao za kupunguza gharama za uendeshaji na kuanza kupata faida, imani yetu ni kwamba wataendelea kuwa waaminifu, tufanye mgodi huu wa Watanzania uwe mfano, tuondoe aibu kwamba Watanzania wakipewa kitu wakisimamie wenyewe kinawafia mikononi mwao,” anasema Biteko.

Akizungumzia mgodi huo ulivyokuwa awali kabla hawajaamua kufanya mapinduzi ambayo sasa yanaonekana, Biteko anasema; “Stamigold ilikuwa na historia mbaya sana.

“Mgodi huu ulikuwa ‘shamba la bibi’, na watu walikuwa wanaiba bila aibu na gharama inabeba Serikali. Gharama ya mafuta na kemikali ilikuwa inaongezwa mara dufu.

 “Serikali iliwekeza Sh bilioni 20 za kuendeleza mgodi, lakini matokeo yake mgodi ukazalisha madeni ya Sh bilioni 63 baada ya ukaguzi ikawa Sh bilioni 45.

Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza na wafanyakazi wa Stamigold, kushoto ni Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Brigedia Jenerali Silvester Ghuliko, katikati ni Meneja Mkuu wa Stamigold, Mhandisi Gilay Shamika.

 “Ilifika mahali tukapeleka kwa Rais ombi kutaka mgodi huo uvunjwe, tulisema labda pepo hili linaloitwa Stamigold labda lifutwe. Tukaleta timu ya kwanza ikakubali, bahati nzuri Stamico wakajiongeza wakabadili uongozi.

 “Tulivyoleta timu ya pili kukagua, tukakuta hali imekuwa angalau nzuri, uzalishaji wa wakii moja umeshuka kutoka dola za Marekani 1,800 hadi 940, tunataka ishuke mpaka 800.”

Meneja Mkuu wa Stamigold, Gray Shamika, anamuhakikishia Waziri Biteko kuwa wanajiendesha wenyewe kwa kugharamia gharama zote, ikiwemo kulipa mishahara ya watumishi na kulipa wazabuni.

Anasema taarifa za kijiolojia zinaonyesha kuwa mgodi bado utaendelea kuishi pamoja na uwepo wa changamoto mbalimbali zikiwemo za madeni.

Shamika anasema kwa sasa mgodi upo katika utaratibu kuanzisha mradi wa kuchenjua visusu (tailings), utakaoupa uhai mgodi kwa miaka saba hadi 10 ijayo.

Kuhusu kupunguza gharama za uzalishaji, Shamika anasema mgodi umepunguza gharama za uzalishaji kutoka dola 1,800 hadi 940 kwa wakia (ounce) moja.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Brigedia Jenerali Silvester Ghuliko, anasema wako tayari kutekeleza maagizo ya waziri na walishaanza kujipanga kuyatekeleza, hususani kuanza kuuza dhahabu katika soko la ndani mara baada ya mkataba wa kuuza nje kumalizika Novemba.

Wafanyakazi wa Stamigold wakimpa Waziri wa Madini, Doto Biteko, melezo ya uchimbaji madini kwenye mgodi huo.

Hata hivyo, kwenye taarifa ya Shamika ilieleza kwa kina walivyofanya utafiti kuhusu faida za kuuza dhahabu ndani ya nchi ama nje ya nchi.

Taarifa hiyo inasema; “licha ya kuwa na changamoto ya upatikanaji wa mnunuzi wa ndani mwenye uwezo wa kununua kiasi kikubwa cha madini kwa wakati mmoja, bado kampuni ipo katika mchakato wa utafiti wa kuona kama uuzaji wa dhahabu katika masoko ya ndani utapelekea kupanda kwa mapato ikilinganishwa na uuzaji katika masoko ya  kimataifa.

“Kuna uwezekano kuwa gharama za usafirishaji, mkandarasi anayepokea dhahabu uwanja wa ndege na kuuza katika soko la dunia zitapungua kuondolewa pindi tukipata soko la uhakika la ndani.”

Mathalani, taarifa hiyo inasema mauzo ya madini ya Julai 2019, gharama iliyotumika kuuza soko la nje ilikuwa ni Dola za Marekani 185,034.04, ambayo ingetumika kuuza kwenye soko la ndani ingekuwa Dola za Marekani 140,956.66.

“Kiasi cha fedha ambacho mgodi ungeokoa kwa kuuza soko la ndani zingekuwa Dola za Marekani 44,077.38 kwa mwezi huo wa Julai 2019. Kwa mtiririko kama huo, kiasi cha fedha ambacho mgodi ungeokoa kwa mwaka ni Dola za Marekani 528,928.56.

“Mikataba kati ya mgodi na mawakala wetu wanaosimamia uuzaji wa madini nchini Switzerland inafikia ukomo wake Novemba 2019,” inasema taarifa hiyo.

Baada ya kwisha kwa mktabaha huo, mgodi utaanza kuuza dhahabu katika masoko ya ndani ya nchi ambayo yameanzishwa kipindi cha uongozi wa Rais Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles