25.5 C
Dar es Salaam
Monday, December 16, 2024

Contact us: [email protected]

Stamigold ilivyojipanga kujiendesha kwa faida, kulipa kodi za Serikali

Na Mwandishi Wetu

JULAI 2017, ikiwa ni miaka miwili tangu kuingia madarani, Rais Dk. John Magufuli alianza kufumua sekta ya madini, hususani dhahabu ili kuhakikisha rasilimali hiyo inachangia ipasavyo uchumi wa taifa.

Akizungumza katika ziara yake mkoani Kigoma ambako alizindua Barabara ya Kibondo-Nyakanazi, Rais Magufuli alisema taifa linapoteza fedha nyingi kutokana na upotevu wa madini.

Rais Magufuli alisema Serikali haitasita kufunga migodi yote ya madini ambayo wamiliki walitakiwa kufanya mazungumzo na Serikali kuhusu ulipaji kodi.

 “Ni matrilioni ya fedha ambayo yanapotea, na sasa hivi tumewaita tufanye mazungumzo, lakini wakichelewachelewa nitafunga migodi yote,” alisema.

Alisema ni bora migodi hiyo ikakabidhiwa kwa Watanzania kuliko wawekezaji ambao hawalipi kodi.

Baada ya kauli hiyo, wengi walidhani Watanzania wakikabidhiwa mgodi hawataweza, lakini Stamigold Biharamulo Mine (SBM), ambayo kwa sasa inaendeshwa na Watanzania kwa asilimia 100, imeonyesha kuwa suala hilo linawezekana.

Stamigold ni kampuni tanzu ya Stamico ambayo kwa sasa ndiyo inayohusika moja kwa moja na uendeshaji na shughuli za uzalishaji kila siku za mgodi huo tangu ilipoanzishwa Oktoba 2013 na kuanza rasmi uzalishaji Julai 2014.

Stamico ilipewa jukumu la kuendeleza mgodi wa dhahabu wa Stamigold uliorithiwa kutoka kampuni za Pangea Minerals Ltd na African Barrick Gold/Acacia zilizokuwa wamiliki wa awali kupitia leseni ya uchimbaji mkubwa Na. 157/2003.

Hadi kufikia Juni 2019, Stamigold imeweza kuzalisha na kuuza wakia 71,375.40 za dhahabu na wakia 7,828.02 za madini ya fedha, vyote vikiwa na thamani ya Dola za Marekani 87,470,127.50 (Sh bilioni 197.7) kwa viwango vya sasa vya ubadilishaji fedha.

Kutokana na ukweli kwamba uhai na maisha ya mgodi hutegemea kiasi cha mashapo yaliyopo na uwezekano wa kuyachimba kwa faida, kazi kubwa imefanyika kutafiti na kuhakiki mashapo katika mgodi.

Kiwango cha mashapo kilichohakikiwa hadi Juni 2019 ni tani 884,041 zenye wastani wa gramu 1.20 kwa tani (1.20g/t) sawa na wakia 34,146.

 Kulingana na mwenendo uliopo wa kuendesha mradi huu kwa faida (profit making trend), mashapo hayo yanaweza kuchimbwa kwa faida ya Dola za Marekani milioni 7.1 (kwa bei ya kuuzia ya wastani wa dola 1,280 kwa wakia) na kuongeza uhai wa mgodi kwa miezi 23 zaidi hadi Juni 2021.

Vilevile mgodi unatarajia kuendelea na uchorongaji wa miamba  ili kuhakiki mashapo yenye tani 132,240 za mbale zenye ‘grade’ ya 20.24 gramu kwa tani yaliyopo eneo la East Pit. Mashapo hayo yaliachwa na Kampuni ya Pangea baada ya kufanya utafiti wa kina.

Kusudio la kampuni hiyo kuyachimba mashapo hayo kupitia mgodi wa chini ya ardhi halikufanikiwa kwa sababu ya njia waliyotarajia kufikia wakia hizo kujaa maji.

“Kusudio la mgodi ni kufanya uchorongaji wa mashimo sita ili kuhakiki uwepo wa mbale hizo zinazokadiriwa kuwa na zaidi ya wakia 87,340 za dhahabu. Pamoja na uhakiki huo, mgodi unaendelea kufanya tathmini ya kubaini njia bora ya kuchimba dhahabu hiyo kwa faida.”

Pia kampuni inatarajia kufanya utafutaji wa madini katika leseni za utafutaji wa madini zinazoizunguka leseni maalumu ya uchimbaji.

  Utafutaji huo unatarajiwa kufanyika katika leseni mbili kati ya tisa za mgodi za utafutaji wa madini ambazo ni Na. PL9548/2014 na Na. PL6141/2009.

Kwa sasa mgodi kupitia Stamico unaendelea na mazungumzo yenye lengo la kuishirikisha Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kufanya shughuli za utafutaji wa dhahabu ndani ya leseni maalumu ya uchimbaji Na. SML157/2009 pamoja na leseni za utafutaji wa madini Na. PL6141/2009 na Na. PL9548/2014.

Utafiti wa awali uliofanywa na mgodi pamoja na taarifa za kijiolojia za Kampuni ya Pangea unabainisha kuwa leseni ya utafutaji wa madini Na. PL9548/2014 ina madini ya dhahabu yanayohitaji kufanyiwa ufuatiliaji wa kina.

Aidha, utafutaji wa madini wa awali uliofanywa na Kampuni ya Pangea katika leseni Na. PL6141/2009 ulibainisha viashiria vya uwepo wa madini ya dhahabu yanayohitaji kufanyiwa utafutaji wa kina. 

Mradi wa Visusu (Tailings)

Menejimenti ilipeleka sampuli za visusu kiasi cha ndoo kumi katika maabara ya The African Minerals and Geo-sciences Centre (AMGC) zamani Seamic, kufanya uchunguzi wa kina ili kujua uwepo wa dhahabu katika sampuli hizo.

Waziri wa Madini, Doto Biteko wapili kulia akisikiliza maelezo juu mradi wa bwawa la visusu, kulia ni Meneja Mkuu wa Stamigold, Mhandisi Gilay Shamika.

Kwa mujibu wa matokeo ya kiuchunguzi wa kimaabara uliofanywa na maabara hiyo mapema mwaka jana, imebainisha uwepo wa wastani wa wakia 200,000 za dhahabu kutoka katika bwawa la visusu (Tailings Storage Facility) lenye ujazo wa tani 8,600,000 za visusu vikiwa na wastani mizania (weighted average) wa grade ya 0.72g/t.

Kwa sasa, mgodi tayari umeshaandaa mpango wa biashara (Business Plan) mahsusi ili kuchenjua visusu hivyo.

Mpango huo unaelezea makadirio ya mapato yatakayopatikana, gharama na faida zitakazotokana na mradi huo.

Utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kuongeza uhai wa mgodi (life of mine) kwa takriban zaidi ya miaka saba.

Kadhalika, kampuni inakamilisha matayarisho ya mpango mkakati wa miaka mitano, ambao unaweka malengo na kutoa dira ya jinsi ya kuyafikia malengo hayo ifikapo mwaka 2023.

Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/19 jumla ya wakia 13,194.58 za madini ya dhahabu na wakia 1,813.57 za madini ya fedha zote zenye thamani ya Sh bilioni 38.3 zimezalishwa na kuuzwa.

Mgodi umeweza kufanikisha ukarabati muhimu wa mtambo wa uchenjuaji wa madini ya dhahabu.

 Ukarabati huo ulihusisha ubadilishwaji wa rollers, liners, lifters na kipande cha conveyor belt chenye urefu wa mita 300.

Kampuni iliandaa mpango wa biashara unaotoa mwongozo wa jumla kibiashara kuhusu miradi ya kutekeleza na kipindi kitakachotumika kutekeleza (Project Profiling).

Aidha, mpango huo unaonyesha maoteo ya mtiririko wa mapato na matumizi (Forecasted Cash Flows) kwa lengo la kuonyesha kama uchimbaji utakuwa wenye tija.

Uongozi umeendelea kupunguza gharama za uzalishaji wa mgodi ambazo zimepungua kutoka wastani wa Dola za Marekani 1,800 kwa wakia moja katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi, mwaka jana na kufikia wastani wa Dola za Marekani 940.14 kwa wakia moja katika kipindi cha Julai mwaka jana hadi Juni mwaka huu.

Katika mwaka wa fedha 2018/19, mgodi uliilipa Serikali Sh 2,661,435,778.26 kama mrabaha, ada ya ukaguzi na kibali cha kusafirisha madini nje ya nchi.

Malipo ya Mrabaha na Tozo Mbalimbali Katika Kipindi cha Julai 2018 hadi Juni 2019

      JINA JULAI HADI SEPTEMBA 2018   OKTOBA HADI DESEMBA 2018   JANUARI HADI MACHI 2019   APRIL HADI JUNI 2019     JUMLA
Mrabaha (6%) 575,613,510.22 686,045,103.32 596,762,225.07 421,812,385.40 2,280,233,224.01
Adaya ukaguzi(1%) 96,313,016.75 114,340,827.81 99,460,367.04 68,580,217.71 378,694,429.31
Kibali cha kusafirisha madini nje ya nchi     682,359.00      682,359.00 686,206.94 457,200.00 2,508,124.94
JUMLA 672,608,885.00 567,876,431.00 696,908,799.00 490,849,803.00 2,661,435,778.26
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles