Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limepiga hatua katika kufungamanisha sekta ya madini na nishati kwa kuongeza uzalishaji wa Nishati mbadala ya Rafiki Briquettes ili kuokoa mazingira.
Akizungumza katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam ‘Sabasaba’, Mkurugenzi wa STAMICO, Dk. Venance Mwasse amesema STAMICO imekuja katika maonesho haya ili kutoa elimu na kuonesha fursa za uwekezaji zilizomo katika miradi mbalimbali ya STAMICO sambamba na namna inavyojikita katika utunzaji wa mazingira.
Amesema kupitia mkaa wa Rafiki Briquette STAMICO imeamua kutafsiri maana halisi ya kufungamanisha sekta kwa kutengeneza nishati mbadala unaokwenda na dira ya Taifa inayotaka asilima 80 ya watanzania kutumia nishati safi na salama ya kupikia ifikapo 2033 ili kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Akitoa maelezo kuhusu nishati hiyo Mratibu mradi, Mhandisi Happy Mbenyange amesema nishati hiyo ni nishati safi na salama kwa watumiaji wake kwani umeondolewa moshi, sumu, na hewa zote chafu zinazoweza kuathiri mtumiaji.
Mbenyange amesema kuwa mkaa huu unaweza kutumiwa na kila mtu hata Taasisi kwa vile bei yake ni nafuu na umezingatia usalama wa mazingira na afya ya watumiaji.
Amewahimiza watanzania kutumia mkaa huu ili kutunza mazingira ili kuepuka athari za mabadiliko ya tabia ya nchi na kufanya nchi ya kijani.
Naye Mwenyekiti wa Foundation for Disabilities Hope, Michael Salali amesema ubunifu wa mkaa huo una maana kubwa sana kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) ambao ni wahaanga wa kubwa wa miale na mwanga wa jua.
Ameongeza kuwa uwepo wa mkaa huu ambao ni mbadala wa mkaa wa miti kutachangia uwepo wa na miti ya kivuli sambamba na kuzuia uzalishaji wa hewa ukaa inayopelekea mabadiliko ya tabia nchi.
Mkaa huo umepokelewa kwa namna ya kipekee na watanzania hasa wanaojishughulisha na upishi kwa kuwa unawasaidia sana kupunguza gharama katika manunuzi ya nishati ya kupikia.
Akizungumza kwa niaba ya baadhi ya wapishi waliotumia mkaa huo, Mary Philipo amekiri kuona manufaa ya mkaa huo na kusema umekuja kupunguza suala la ukataji miti kwa kuwa ni unadumu na hauna moshi katika kutumia hivyo unasaidia kutunza mazingira.
Ametoa wito kwa wapishi kutumia mkaa huu ili waweze kuondokana na gharama za nishati ya kupikia sambamba na kuchangia jitihada za Serikali za kupambana na uharibifu wa mazingira.