27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

 SSRA yatoa maelekeo kwa mifuko ya Jamii

onoriusNa NORA DAMIAN – DAR ES SALAAM

MIFUKO yote ya hifadhi ya jamii imetakiwa kupunguza gharama za uendeshaji.

Imesema  kuanzia sasa ukomo wa kiwango cha matumizi ya fedha unatakiwa usizidi asilimia 10 ya michango ya wanachama.

Mapendekezo hayo yametolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kupitia miongozo yake 15 katika maeneo mbalimbali huku mojawapo likiwa ni la gharama za uendeshaji mifuko.

Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa mamlaka hiyo, Onorius Njole, alikuwa akizungumza mwishoni mwa wiki alipozungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari.

Alisema mwongozo huo umeanza kutekelezwa Julai Mosi mwaka huu.

“Iko mifuko ambayo matumizi yake ni chini ya asilimia 10 na mingine ni zaidi ya asilimia 10, lakini haina maana kwamba hawa ambao wako chini basi ndiyo wazidishe hadi kufikia kiwango hicho.

“Mifuko yote inatakiwa iendeshwe kwa gharama za chini na iwe na uwezo wa kulipa mafao wanachama wake,” alisema Njole.

Awali, Mkurugenzi  Mkuu wa SSRA, Irene Isaka, alisema sekta hiyo imeendelea kukua ambako idadi ya wanachama imefikia milioni 2.1 huku michango ikiwa ni Sh trilioni 1.8.

Akizungumzia mafao ya kujitoa, alisema yalikwisha kufutwa kwa  Sheria Namba Tano ya mwaka 2012 na kwamba hivi sasa serikali inaangalia namna ya kufikia suluhisho la kudumu.

“Tathmini na utafiti umekamilika na sasa tunakusanya maoni ya wadau  tuweze kurekebisha sheria mfanyakazi anapopata janga aweze kupata fidia.

“Utaratibu utakaowekwa utaangalia makundi yote kwa sababu kuna wafanyakazi ambao hawawezi kufika miaka 55 (umri wa kustaafu kwa hiari) na wengine ajira zao si za kudumu,” alisema Isaka.

Alisema mifuko ya LAPF na PSPF ilikuwa na vipengele vinavyoruhusu mtu kujitoa lakini wanaojitoa zaidi ni wanachama wa mifuko ya NSSF na PPF, hivyo utaratibu utakaowekwa utaingizwa kwenye mifuko yote.

Naye Mkurugenzi wa Utafiti, Tathimini na Sera wa mamlaka hiyo, Ansgar Mushi, alisema sababu kubwa zinazochangia watu kujitoa katika mifuko ni mabadiliko ya soko la ajira.

Alisema  asilimia 78 ya wanaochukua mafao huwa ni wale walioacha kazi na asilimia 22 ni wale waliokosa ajira kwa sababu mbalimbali.

Alisema hasara ya kujitoa katika mifuko ni kubwa kwa vile  mwanachama husika anaweza kukosa kipato  anapokuwa amestaafu hivyo kuwaumiza wengi wanaomtegemea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles