24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, March 29, 2023

Contact us: [email protected]

Serikali yafanyia mabadiliko Sheria ya Takwimu

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

SERIKALI imefanyia mabadiliko Sheria ya Takwimu, marekebisho yaliyolenga kwenye vifungu vya  haki ya kuchapisha au kutoa taarifa za takwimu kwa umma

Mabadiliko hayo yalifanywa na Bunge jana kupitia Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali, Namba 3 wa Mwaka 2019, uliowasilishwa kwa hati ya dharura.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Prof. Adelardus Kilangi, alisema mapendekezo hayo yanakusudia kuanzisha Kamati ya Kitaalam (Technical Committee) ambayo jukumu lake litakuwa kupokea kujadili malalamiko yanayotokana na wadau kuhusu usahihi wa takwimu zilizotolewa kwa umma.

“Katika jedwali la marekebisho, inapendekezwa kufuta vifungu vya 24A na 24B na kuviandika upya, pia kuongeza vifungu vipya vya 24C, 24D, 24E na 24F kwa lengo la kuweka utaratibu wa kutoa matokeo ya takwimu zinazotofautiana na takwimu rasmi zilizotolewa na serikali,”alisema Kilangi.

Alisema marekebisho hayo yanatoa fursa kwa mtu yeyote kutoa takwimu zinazotofautiana na zilizotolewa na Serikali, iwapo atakuwa amezingatia misingi ya kitakwimu iliyowekwa katika miongozo mbalimbali ya kitaifa na kimataifa inayosimamia utoaji wa takwimu.

Sambamba na marekebisho hayo sheria hiyo inapendekeza kufutwa kwa kifungu cha 37 (4) kinachotoa adhabu kwa mtu anayetoa taarifa za takwimu bila kupata kibali cha Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Vibanda vya video kurasmishwa

Wakati anatoa maelezo yake kuhusu marekebisho ya Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza (Sura ya 230), Prof. Kilangi alisema lengo la marekebisho hayo ni kuhakikisha kwamba kumbi na vibanda vinavyotumika kunesha video vinapaswa kurasimishwa chini ya kifungu cha 10 cha sheria hiyo.

“Kwa mujibu wa kifungu kipya cha 6A, mtu au kampuni ya kigeni inayotaka kutumia eneo lolote a Tanzania kutengeneza filamu, itapaswa kuwasilisha nakaa ya awali iliyotumika kutengeneza filamu husika, kubainisha maene ya Tanzania ambayo yametumika katika kuandaa fiamu husika.

“Na pia kuwasilisha kwa Bodi ya Filamu nakala ya filamu iliyotengenezwa na kuruhusu filamu au kipande cha picha jongevu kutumiwa na serikali ya Tanzania kutangaza maliasili na utalii, mila na tamaduni za mtanzania.”

Sheria ya NGOs

Pia Bunge lilipitisha mabadiliko ya sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali ambapo Prof. Kilangi, itasaidia kuleta uwazi na uwajibikaji kwa kuhakikisha miradi na shughuli zinazofanywa na asasi hizo zinakuwa na tija kwa jamii na taifa.

Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), yalikuwa yakipinga muswada huo yakisema inabana uhuru na kuweka vipengele mbalimbali vikavyovyofanya baadhi yashindwe kujiendesha.

Jana Prof. Kilangi alisema marekebisho ya kifungu cha 31 cha sura ya 56 cha sheria hiyo ya NGO’S kinaweka masharti kwa mashirika hayo kufuata kanuni za fedha za uwazi na uwajibikaji.

 “Marekebisho ya kifungu cha 4 yanalenga kupanua wigo wa majukumu na wajibu wa Mkurugenzi wa Uratibu wa Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’S) ili kumwezesha kuzuia shirika lisilo la kiserikali kutekeleza majukumu yake endapo litakuwa linatekeleza majukumu yake kinyume cha sheria na kutathimini shughuli zinazotekelezwa na shirika lisilo la kiserikali,” alisema.

Alisema kifungu kipya cha 4A kinampa Msajili mamlaka ya kufanya uchunguzi wa mwenendo wa shirika lolote lililo chini yake.

Pia, kila baada ya miaka 10, shirika lisilo la kiserikali litapaswa kuzingatia masharti ya kifungu cha cha 17 cha sheria hiyo ambacho kinaweka ukomo wa vyeti vya usajili na utaratibu wa kuhuisha vyeti hivyo.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, mashirika hayo ni yale tu yanayolenga kunufaisha jamii na sio wanachama wake.

Sheria ya Vyama vya Kijamii

Aidha alisema katika Sheria ya Vyama vya Kijamii (Sura ya 337) marekebish yanayofanywa hivi sasa, yanalenga kuondoa mkanganyiko kati ya Msajili wa Jumuiya za Kijamii na Taasisi zingine za usajili kama vile NGO’s na Wakala wa Usajili wa Leseni na Biashara (Brela).

Vile vile, marekebisho hayo yanayopendekezwa yanakusudia kuhuisha adhabu zilizopitwa na wakati ili ziweze kuendana na hali ya sasa.

Miswada mingine iliyosomwa Bungeni na kujadiliwa na wabunge ni pamoja na Sheria ya Makampuni (Sura ya 212), Sheria ya Haki Miliki (Sura ya 218), Sheria ya Uwakala wa Meli (Sura ya 415) na Sheria ya Miunganisho ya Wadhamini (Sura ya 318)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,259FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles