Na MWANDISHI WETU |
KAMPUNI ya kubashiri michezo ya SportPesa na klabu ya soka ya Everton ya Uingereza zimezawadiwa tuzo kutokana na ushirikiano wao kwenye tuzo za Sports Industry Awards kwenye vipengele vya Best African Sponsorship na Pan-African Campaign of the Year.
Kwenye udhamini huo ambao ulianza kwa klabu ya Everton kusafiri kwenda Dar es Salaam, walicheza dhidi ya timu ya Gor Mahia ya Kenya, umetambuliwa na kusherehekewa kwa kuleta klabu inayoshiriki Ligi Kuu England kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza.
Mafanikio ya safari hiyo ambayo ilijulikana kama ‘Everton in Tanzania’, yalitoa hamasa kwenye michezo na kuipa SportPesa ushindi wa tuzo hizo ambazo zilitangazwa kwenye Ukumbi wa Sandton Convention Centre jijini Johannesburg Ijumaa iliyopita.
Mkuu wa Ushirikiano na Utawala wa Everton, Mark Rollings, alisema wanayo furaha kuwa ushirikiano wao na SportPesa umetambulika kwenye ngazi muhimu Sports Industry Awards.
“Tuzo ya Industry Awards ndio tuzo zenye heshima kubwa Afrika Kusini kwa upande wa michezo na kwa hivyo kushinda tuzo zote mbili za Best African Sponsorship na Pan-African Campaign of the Year ni uthibitisho wa kuendeleza ushirikiano wetu na SportPesa pamoja na wadau wake,” alisema.
Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa SportPesa Tanzania, Abbas Tarimba, alisema ni furaha kubwa kwao na yeye binafsi kushuhudia heshima kubwa hiyo ambayo kampuni imepata kwa kushinda tuzo hizo ambazo zitawapa hamasa kuendeleza michezo barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Akizungumzia kuhusu kuandaa michezo hapa nchini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Susan Mlawi, alisema tuzo hizo ni muhimu sana kwa Afrika Mashariki.