ABIDJAN, IVORY COAST
UWEZEKANO wa kujiuzulu kwa Spika wa Bunge la nchini Ivory Coast, Guilluame Soro, ni mkubwa baada ya kukubali kutokukubaliana na Rais Allasane Ouattara, mapema mwezi uliopita juu ya uamuzi wa kujiunga na chama kipya cha siasa cha RHDP, hatua ambayo imezua gumzo nchini humo.
Katika kikao kisichokuwa cha kawaida cha Bunge la Ivory Coast, kiliitishwa jana nchini humo kikiwa na lengo la kujadili hatima ya Spika wa Bunge, Guilluame Soro, kama ahadi aliyotoa mwezi uliopita kuwa atajiuzulu wadhifa wake baada ya kufikia makubaliano na Rais wa nchi hiyo.
Uamuzi wa kujiuzulu kwa Spika Soro ulitangazwa mwishoni mwa Januari na Rais Alassane Ouattara wa nchi hiyo.
Ripoti za vyombo vya habari zinasema kuwa viongozi hao wawili walikubaliana kuhusu suala hilo, baada ya Soro kukataa kujiunga na chama kipya cha RHDP.
Suala hilo la kujiuzulu kwa Soro limekuwa gumzo nchini humo. Spika wa Bunge na Rais Alassane Ouattara, walikutana mara mbili tangu mwanzoni wa mwaka huu ili kujadili suala hilo la kujiuzulu kwenye nafasi ya uspika.
Rais Ouattara mwenyewe alitamka mbele ya waandishi wa habari Januari 28 mwaka huu akisema: “Soro atajiuzulu mnamo Februari, tumekubaliana, suala hilo limekwishapatiwa ufumbuzi.”
Hata hivyo, haijajulikana hatima ya spika huyo katika siasa za nchi hiyo mara baada ya kuachia ngazi.