25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

SPIKA USIPOSIKIA WEWE, NANI ATASIKIA?

HILI  nimewahi kuliandika siku za nyuma na leo nimeamua kulirudia tena kwa sababu inavyoonekana bado linaendelea. Jambo lenyewe ni kuendekeza siasa katika uendeshaji wa taasisi muhimu za nchi ambazo hazipaswi kuendeshwa kisiasa.

Kwa Bahati mbaya sana ,moja ya taasisi zilizoangukia katika mtego huo ni Bunge.

Tukio la wiki iliyopita la kutolewa ndani ya Bunge kwa Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, ni tukio la kusikitisha sana. Na linasikitisha pande zote. Linasikitisha kwa sababu kinaonyesha jinsi siasa zinavyotumika vibaya ndani ya Bunge.

Kwa upande wa Mnyika, ni dhahiri kuwa kwa kutumia hulka za binadamu, alilazimika kusimama kidete kutetea haki yake baada ya Spika Job Ndugai kumuamuru aondoke ndani ya Bunge.

Lakini ukiangalia kimantiki, hakupaswa kuibishia amri ya Spika kwa sababu kanuni zinamtaka afanye hivyo. Pamoja na umuhimu wa yeye kutetea haki yake, lakini kuna umuhimu pia wa yeye kuheshimu mamlaka. Hivyo, Spika alipomuamuru atoke, ingawa kimsingi anaamini kuwa hakuwa na kosa lililostahili yeye kupewa hukumu hiyo, alipaswa kutii.

Mnyika alipaswa kutii kwa sababu zipo njia nyingine ambazo angeweza kuzitumia kuhakikisha anaipata haki yake aliyokuwa anaidai kwenye hoja yake.

Lakini, zipo kanuni ambazo Mnyika angeweza kuzitumia kuonyesha kuwa amri ya kumtoa ndani ya Bunge haikuwa halali. Hivyo, angeweza kutoka bila kusababisha rabsha tulizozishuhudia na baadaye akapata haki yake.

Rabsha tulizoziona si nzuri kwa sababu kwa kiasi fulani, hata kama tutapata mtu wa kumlaumu au kuzitetea, lakini kwa ujumla zimelifedhehesha Bunge. Inapotokea nguvu inatumika kumtoa Mbunge ndani ya Bunge, basi lazima kuna walakini na walakini huo unavuka wajibu wa Mbunge mmoja mmoja.

Ni wajibu wa Bunge (kwa maana ya uongozi wake) kuhakikisha Wabunge wanakuwa na nidhamu ya hali ya juu na wanafuata kanuni, taratibu na sheria.

Lakini kwa upande wa pili Spika Ndugai naye alikuwa na nafasi ya kulishughulikia suala hili kwa namna ambayo isingelifikisha Bunge pale lilipofika.

Ukiangalia kwa upana, mjadala ambao ulisababisha Mnyika kupewa amri ya kutoka ndani ya Bunge na yeye kuibishia kwa muda, ulitawaliwa na mivutano ya kisiasa. Licha ya maonyo yaliyopata kutolewa siku za nyuma, jambo hili limeachwa liendelee kwa muda mrefu sana. Matokeo yake, leo linaanza kutugeuka na kuiumiza nchi.

Kwa hali ilivyo hivi sasa, ni vigumu sana Bunge kuepuka mgawanyiko wa kisiasa hata linapojadili masuala muhimu ya nchi ambayo hayapaswi kuwagawa wabunge.

Mara nyingi, wabunge wanajadili jambo kwa kuzingatia hoja imetolewa na nani. Wengi wanajadili bila kupima hoja husika. Kwa sababu tu imetolewa na mtu mwenye itikadi ya kisiasa tofauti, basi hoja hiyo ni ya kupingwa.

Makosa ya kuacha siasa zitawale mijadala ndani ya Bunge ndio imetufikisha mahali ambapo kunakuwa si tu na shida ya kujadili hoja za msingi ndani ya Bunge, bali pia hisia za kuwa Bunge linaendeshwa kisiasa.

Wakati Mnyika alipokuwa anasisitiza aliyemwita mwizi athibitishe au afute kauli, Spika Ndugai akasisitiza pia kuwa hakusikia Mnyika akiitwa mwizi. Ni ajabu kwa sababu hata sie ambao hatukuwapo ndani ya Bunge wakati huo tumelisikia neno hilo na Spika ambaye ndiye alikuwa anaongoza kikao hakulisikia. Sasa kama Ndugai anayeongoza vikao hasikii yanayosemwa bungeni, tena kupitia vipaza sauti, nani atawasikia wabunge wanapokuwa bungeni?

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles