SPIKA AWATUMIA SALAMU MDEE, BULAYA

0
1062

 

 

Na KULWA MZEE -DODOMA

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amesema wabunge wa Chadema, Halima Mdee wa Kawe na Esther Bulaya wa Bunda, wanaweza kupewa adhabu kubwa zaidi ya waliyopewa endapo wataendelea kufanya malumbano na Bunge.

Ndugai, alitoa onyo hilo jana baada ya kumalizika muda wa mjadala wa bajeti ya mwaka 2017/18.

“Wabunge waliochukuliwa hatua wanaendelea kulumbana na Bunge, huko waliko wanaweza kuitwa kuhojiwa na kupewa adhabu kubwa zaidi ya waliyopewa, nawapa onyo la jumla.

“Mtu ukitaka kupambana na mtu, unayepambana naye pia atataka kupambana na wewe. Kwa hiyo, naomba ndugu na jamaa muwafikishie onyo hilo ili waache malumbano.

“Napenda kuwafahamisha wabunge hawa, kwamba wamevumiliwa kwa mengi, lakini kama bado huko waliko wanafikiri wanaweza kuendelea na tabia hizo, wanaweza kuitwa na kupata adhabu kubwa zaidi ya waliyopata.

“Na kama mtu anataka kwenda mahakamani, hawezi kualika watu kwenye mkutano wa hadhara bali ataamua kwenda tu,” alisema Spika Ndugai.

Juni 5, mwaka huu, Mdee na Bulaya walihukumiwa kutohudhuria vikao vyote vya Bunge linaloendelea hadi mkutano ujao wa Bunge la Bajeti la mwaka wa fedha 2018/19.

Bulaya alituhumiwa kuwahamasisha wabunge wenzake wa upinzani watoke nje ya Bunge baada ya Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema) kutolewa bungeni kwa nguvu na askari wa Bunge.

Mdee kwa upande wake alikuwa akituhumiwa kumvuta koti askari wa Bunge aliyekuwa akishirikiana na askari wenzake kumtoa bungeni Mnyika.

Wabunge hao walipewa adhabu hiyo na Bunge baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge, George Mkuchika, kuwasilisha bungeni mapendekezo ya kamati yake iliyowajadili watuhumiwa hao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here