26.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Spika atafakari wabunge CUF waliofukuzwa uanachama

Na Mwandishi Wetu

-DAR ES SALAAM

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amesema anatafakari suala la wabunge wanane wa viti maalumu wa Chama cha Wananchi (CUF) waliofukuzwa uanachama.

Uamuzi huo wa Spika umekuja baada ya kupokea barua ya kufukuzwa uanachama iliyowasilishwa jana ofisini kwake na Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Profesa Ibrahim Lipumba na Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Magdalena Sakaya.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na ofisi ya Spika ilieleza kuwa kutokana na uamuzi huo, Spika Ndugai anatambua kuwa suala la kuwavua uanachama wabunge hao ni la utashi wa vyama vyenyewe na kila chama kina utaratibu wake.

“Mheshimiwa  Spika amepokea barua kutoka kwa Mhe. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF) na Mhe. Magdalena Sakaya, (MB) – Kaimu Katibu Mkuu (CUF) ambapo wamemuarifu kuhusu uamuzi wa Baraza Kuu la chama hicho kuwafukuza uanachama wabunge wanane na madiwani wawili kwa makosa kadhaa ya kinidhamu.

“Katika barua hiyo, viongozi hao wamewataja wanachama hao ambao ni Riziki Shahali Ngwali, Saverina Mwijage, Salma Mwassa, Saumu Sakala, Raisa Abdallah Mussa, Miza Bakari, Halima Ali Mohammed,  Khadija El Kassim.

“Mhesimiwa Spika anapenda kuuarifu umma kuwa, suala la kuwaondoa uanachama ni la utashi wa vyama vyenyewe na kila chama kina utaratibu wake, hivyo bado anaendelea kuitafakari barua hiyo na taarifa rasmi kuhusu maamuzi ya Spika kwa wabunge waliofukuzwa ataitoa hapo baadaye,” ilieleza taarifa hiyo.

Barua hiyo iliainisha makosa yaliyofanywa na wabunge hao ikiwamo kukiuka kifungu cha 83 (4) na (5) cha katiba ya CUF kwa kutenda makosa ikiwamo kukihujumu chama katika uchaguzi wa marudio wa madiwani wa Januari 22, mwaka huu.

“Kumkashifu na kumdhalilisha Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Prof. Ibrahim Haruna Lipumba, Naibu Katibu Mkuu na Mbunge wa Kaliua, mhe. Magdalena Hamisi Sakaya na wakurugenzi wa chama.

“Kushirikiana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupanga oparesheni waliyoiita “ONDOA MSALITI BUGURUNI” wakiwa na lengo la kumwondoa mwenyekiti halali wa chama hicho kinyume cha taratibu ya katiba ya CUF na Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 1992 na kuipa fursa CHADEMA kuwa msemaji wa masuala ya CUF kinyume cha matakwa ya katiba ya CUF,” ilieleza barua hiyo.

Mbali na hilo pia inadaiwa wabunge hao walilipia pango na kufungua ofisi ya CUF Magomeni bila kufuata taratibu za kikatiba pamoja na kuchangia fedha zilizotumika kukodisha ma-baunsa kwa lengo la kuwadhuru viongozi watiifu wa chama.

Viongozi hao watiifu kwa chama waliotajwa katika barua hiyo ni Mwenyekiti wa Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, Naibu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya na Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma ambaye pia ni Mkurugenzi wa CUF wa Mambo ya Nje.

Kutokana na hali hiyo MTANZANIA ilimtafuta Riziki Shahali Ngwali, ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni ili kupata kauli yake kuhusu uamuzi huo, ambapo alisema hajaona barua ya Lipumba hivyo hawezi kusema lolote kwa sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles