25.3 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

SOPHIA MWAKAGENDA: LIANZISHWE BARAZA LA WANAWAKE

Na ELIZABETH HOMBO


LEO ni Siku ya Wanawake Duniani. Ni siku ambayo huadhimishwa Machi 8 ya kila mwaka, lengo likiwa ni kukuza usawa wa jinsia na kuwawezesha wanawake katika ngazi mbalimbali.

Katika nchi nyingi za Afrika suala la usawa wa kijinsia limeendelea kufanyiwa kampeni, lakini bado wanawake wengi wanaendelea kukabiliwa na ubaguzi katika upatikanaji wa elimu, kazi, mali na kushirikishwa katika maamuzi na uongozi serikalini.

MTANZANIA limefanya mahojiano na Mbunge wa Viti Maalumu Sophia Mwakagenda, ambapo amezungumzia nafasi ya mwanamke katika nyanja mbalimbali.

Mwakagenda ambaye pia ni mwanaharakati wa wanawake anasema katika awamu iliyopita, Rais Jakaya Kikwete alijitahidi kuwainua wanawake kwa kuwaweka katika nafasi mbalimbali lakini alipokuja Rais wa awamu ya tano hata ile nafasi ndogo ya wanawake ikashuka.

Kutokana na hilo, anasema wanapata wasiwasi idadi ya wanawake wanaogombea majimbo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, inaweza ikapungua.

 “Kimsingi awamu ya nne Rais Kikwete alijitahidi sana kuwainua wanawake kwa kuwaweka katika nafasi mbalimbali lakini alipokuja Rais wa awamu ya tano, hata ile nafasi ndogo ya wanawake ikashuka pia.

“Inatupa wasiwasi mwaka 2020, wanawake watapungua hata wale ambao wamekuwa wakijitokeza kugombea majimbo itapungua, kwa sababu hali ya uchumi imekuwa mbaya na wengi wamekata tamaa hivyo tutegemee wanawake wachache watakaogombea majimbo uchaguzi unaokuja.

“Pia nafasi ya mwanamke kwenye siasa imeshuka japo wabunge tunajitahidi kuinua nafasi ya mwanamke,”anasema.

Akizungumzia kuhusu nafasi ya wanawake katika Tanzania ya viwanda, Mwakagenda anasema bado hawajanufaika kwa sababu hakuna kiwanda hata kimoja.

“Tumesema Tanzania ya viwanda, sasa wanawake wamefaidika vipi, wanaosoma vyuo wamekosa mkopo watawezaje kufikia malengo yao?

“Pia tuangalie wanawake walemavu bado wana changamoto kubwa, huyu mlemavu ananufaika vipi na viwanda wakati mpaka sasa sijaona kiwanda hata kimoja.

“Mfano vyuo vya walemavu Yombo na viziwi Buguruni miundombinu yake inategemea wafadhili. Mtoto kiziwi anapokuwa kwenye hedhi anajisaidiaje kusitiri,”anahoji.

Kutokana na hilo, Mwakagenda anashauri kuwa kuwe na utaratibu wa halmashauri zote nchini kupanga bajeti kwa ajili ya mambo hayo na kwanza viongozi waache siasa katika mambo ya msingi kama hayo.

Mbunge huyo pia anashauri kuwa wanawake wajawazito wapewe ruzuku au bima za afya kama ilivyo Rwanda

“Wanawake wajawazito wapewe ruzuku au bima kama ilivyo Rwanda, hivyo  serikali yetu nayo iandae bima kusaidia wanawake kwa sababu wanapitia changamoto nyingi.

“Pia wanawake wanajeshi wafikie brigedia hivyo hivyo na kwenye fani zingine. Hatuwabebi tu kwa sababu ni wanawake lakini kwa wale wenye uwezo,”anasema.

Mwakagenda anaeleza kuwa lianzishwe baraza la wanawake ambapo serikali itakuwa inatoa ruzuku lakini isiingilie chochote.

“Kwa sisi ambao tumepewa nafasi, tusaidie wenzetu na si kusaidia familia zetu. Lianzishwe baraza la wanawake, mataifa mengine wana mabaraza ya wanawake.

“Kuna umuhimu wa kuanzisha mabaraza haya kwa sababu wapo watu ambao wao hawataki mambo ya siasa lakini likianzishwa baraza hili wote wataingia humo na hawatagusia mambo ya vyama vya siasa. Tufikirie kuanzisha baraza la wanawake, serikali itoe ruzuku lakini isiingilie chochote.

“Najua serikali haipendi kusikia baraza la wanawake. Tuache uvyama, tubadilike kama taifa.

“Binafsi nilianza kazi hii ya harakati za wanawake muda mrefu; jumla ya wanawake 520 walipata mafunzo tukishirikiana na NMB ambapo walitufadhili kufungua vikundi na wanafanya ujasiriamali na NHIF nao walitusaidia umuhimu wa kuwa na bima za afya.

“Baada ya mafunzo hayo, nimewapatia verehani 100, niliamua kuanzisha community library ambapo nilipata ufadhili wa vitabu kutoka Canada,”anasema Mwakagenda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles