22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 14, 2024

Contact us: [email protected]

Sonona inavyoweza kuharibu maisha, usitamani kuishi

MWANDISHI WETU

SONONA ni hali ambayo akili yako inaweza kukuambia kwamba mwili wako umechoka na kumfanya mtu kuchanganyikiwa na kuona kama hakuna umuhimu wowote wa kubaki duniani.

Ugonjwa huu unaweza kumpata mtu aliyeachishwa kazi, kutengana na mwenza wake, kufiwa au kukatishwa tama. Pia huweza kumfanya mtu ahisi kama dunia imesimama na kuona hakuna umuhimu wa kuendelea kuishi.

Wajawazito wengi duniani hukabiliwa na ugonjwa wa sonona, japo wapo ambao hawajui kwamba wanaugua maradhi hayo.

Wengi huwa na mawazo ya hapa na pale ukijumlisha na vikwazo wanavyokumbana navyo katika familia basi hujikuta wakikabiliwa na sonona.

Mwandishi Anna Ceesay, ambaye ni mwanzilishi wa jarida linalohusu masuala ya kina mama la  Motherdom, alipokuwa na ujauzito wa mtoto wake wa pili, alianza kusononeka na kuwa na hofu, lakini ilikuwa ni siri yake, hata mumewe hakuwahi kujua.

Anna aliamua kuanzisha jarida hilo ili kuwasaidia wazazi wengine kujua hali zao za afya ya akili.

Anna Ceesay akiwa na mumewe

Kwa mzazi yeyote mwenye watoto wadogo, atakwambia kuwa ana muda mdogo mno kwa ajili yake mwenyewe, mara nyingi hufikiria na kuhisi jambo lingine.

Matatizo ya Anna Ceesay (33), yalianza wakati mtoto wake wa kike akiwa na miaka mitatu, huku akiwa na ujauzito mwingine wa miezi sita, ya mtoto wake wa pili.

“Majira ya alfajiri nilikuwa ninahisi kuwa si mzima, nilikuwa nahisi uchovu na kuchanganyikiwa.

“Hali hiyo huwa inakuja na kuondoka na kuna wakati haiondoki kabisa hivyo, kuna siku nilikuwa vizuri zaidi ya nyingine,” anasema Anna.

Caesay alikuwa analea watoto peke yake kwa sababu mumewe hakuwapo, alikuwa anafanya kazi katika nyumba yao iliyopo Bromley, Kusini mwa London, ambayo ilikuwa inafanyiwa marekebisho.

Hata baada ya marekebisho ya nyumba, dalili za kuchanganyikiwa ziliendelea kumuandama Anna.

“Nilikuwa nina wasiwasi hasa wakati ninapokuwa jikoni napika. Nilijihisi kuwa ninaenda kuwapa watu sumu katika chakula kila wakati ninapopika mchuzi wa kuku, licha ya kwamba nilikuwa ninapika kila mwisho wa juma.

“Kila ninapohitaji kupika, nilikuwa ninapenda kuangalia maelekezo katika mtandao wa google, hasa ninapotaka kupika kuku kulingana na uzito wa kuku mwenyewe, ingawa nilikuwa ninanunua kiasi hichohicho kila wiki.

Nilikuwa nafanya hivyo kwa sababu nilihisi  nitakosea na kuwawekea watu chakula chenye sumu, na kuna mtu atakufa,” anasema.

Anna alifanikiwa kuficha tatizo lake la sonona kwa kila mtu aliyekuwa karibu yake, akiwamo mume wake, wazazi na marafiki zake.

Yeye mwenyewe pia hakuweza kukubali kwamba ana tatizo hilo.

“Nadhani siko peke yangu, kuwa na hisia kwamba kuna jambo halipo sawa, kuna wakati unajaribu kuliondoa akilini ili maisha yaendelee kama kawaida, lakini inashindikana.

“Ukiwa na watoto wadogo inabidi tu ujitahidi. Hivyo, ilinilazimu kuwahudumia watoto kwanza na kujijali mwenyewe ni baadae.

“Ilinichukua miezi kadhaa kuanza kufikiria, ‘Unajua nini? Siwezi kufanya hili mwenyewe na ninahitaji kupata msaada na nilivyoamua kufanya hivyo, nilikuwa ninaogopa mno,” anasimulia namna alivyoteseka na sonona.

Anasema siku moja alipompeleka mtoto wake shule ya awali, aliegemea usukani wa gari na kuanza kuangalia namba ya huduma ya msaada inayowasaidia watu wanaosumbuliwa na afya ya akili.

Akiwa na miezi nane ya ujauzito, alikuwa akiangalia namba hiyo kwa zaidi ya wiki, lakini hapigi simu, ndipo siku hiyo akapata ujasiri wa kupiga simu.

“Mara ya kwanza, nilisema neno moja kwa sauti na nilipowapigia namba ya Panda inayotoa msaada kwa watu wenye matatizo ya afya ya akili, iliniwia vigumu mno.

“Ilibidi nikubali tu kwamba ninahitaji msaada, japo ilikuwa ni hatua ngumu kwangu kwa sababu mimi ni mtu mwenye tabia ya kujivunia kuwa nina uhuru na jasiri hivyo, kuomba msaada kwa kitu ambacho sijawahi kufanya kabla iliniwia vigumu.”

“Nilivyoweza kuzungumza na namba hiyo, nilijihisi sina nguvu na ndipo tulipomtaarifu mume wangu ambaye alikuwa mbali, akashtuka kusikia hivyo,” anasema.

Mume wake alikiri kwa kusema kuwa mfumo wao wa maisha ndio umewafanya kutotatua tatizo kwa wakati.

“Kwanza kwa mtu ambaye ninampenda kufikwa na tatizo hilo, nilipata msongo wa mawazo na kusikitishwa mno. Ilinibidi nirudi nyumbani haraka niwezavyo,” mume wake anaeleza.

Anasema wakati huo ndio kipindi ambacho ilimbidi awe mkimya na kusikiliza kila ambacho Anna alikuwa anasema.

Anasema alishtuka mno kupata taarifa kwamba mkewe ana sonona, na kwamba halikuwa jambo rahisi kukabiliana nalo.

APATA SONONA BAADA YA KUFIWA NA MWANAWE

Belinda Nyapili ni miongoni mwa watu waliowahi kupata ugonjwa huu.

Alianza kupata tatizo hili wiki mbili baada ya kumzika mtoto wake wa kwanza aliyegua kwa muda mfupi na kufariki.

Anasema alianza kwa kujihisi kutotaka kujichanganya na watu, kutongumza, kutokula na kukosa furaha, kikubwa alichokuwa akikifanya ni kunywa pombe.

“Nilifikia ile hali ya kutaka kujiua kabisa, nilikuwa nasikia sauti na nguvu ya kutaka kujiua. Ndani ya kichwa changu nilikuwa nasikia kelele na ilinisababishia hadi kunywa vidonge 60 ili tu nife. Ni kitu ambacho bado kinanishangaza, ilikuwaje nilipona maana nilikunywa pombe nyingi pamoja na dawa,” anaeleza Belinda.

Belinda anasema suala la kujiua mwanzoni alikuwa analiona kama watu wanaofanya hivyo huwa wana ubinafsi. Hivyo, hali hiyo ilimshangaza kuona hata yeye alitaka kujiua wakati akiwa bado ana mtoto mwingine anayemtegemea.

“Niliwahi kulazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili katika wodi ya wagonjwa wa akili. Nilipata matibabu kwa kusikiliza ushauri nasaha kutoka kwa madaktari, na huko ndiko kulikonisaidia nipone, ingawa hali hiyo huwa inajirudia tu bila kutegemea.

“Nafahamu kuwa jamii haina uelewa wa kutosha kuhusu sonona, wengi wanaokutana na hali kama yangu, lakini wanajaribu kutafutiwa tiba katika upande wa kiimani na wapo ambao huwa na imani potofu juu ya suala hili.

“Kuna dada mmoja mbaye nilikuwa naye wakati napata tiba, yeye alijiua kwa sababu alikuwa hana mtu wa karibu wa kumfuatilia kunywa dawa na kupata tiba.

“Mapito yote haya ambayo nimeyashuhudia katika maisha yangu yamenifanya nianzishe asasi ya kuwasaidia wagonjwa wa sonona,” anasema Belinda.

Marcus Mwemezi Foundation, ni asasi ambayo Belinda aliipa jina la mtoto wake kwa lengo la kuelimisha jamii kuhusu masuala ya afya ya akili na kuwakutanisha wagonjwa wa akili na wataalamu wa afya.

“Sonona huwezi kuiona hadi hatua ya mwisho kabisa, ndio unaweza kugundua tatizo. Mimi ilifikia hatua ambayo hadi nilikuwa nafungwa minyororo.

“Thamani ya utu huwa inapotea, na hata jamii huwa haina muda wa kumhudumia bila kumpa majina,” anasema Belinda na kuongeza kuwa kuna changamoto nyingi mno ambazo binadamu hupitia lakini hakuna maumivu makali ambayo mtu anaweza kuyapata kama pale anapopoteza mtoto wake.

Anasema watu wenye hatari ya kupata magonjwa ya akili wanaweza kuyaepuka iwapo watapata watu wa kuwasikiliza kwa upendo, kuwajali na kutoa ushauri pale inapobidi, hata pasipo ushauri ni msaada mkubwa.

Anasema kuwa jamii ya Watanzania bado inawanyanyapaa wagonjwa wa afya ya akili, kwa sababu ya kukosa elimu au uelewa kuhusu hali hiyo, watu wengi huwa wanatoa majina kwa wagonjwa wa sonona kwa kuwaita vichaa, chizi, mwendawazimu na majina mengine mengi badala ya kuwapatia matibabu.

MATATIZO YA SONONA WAKATI NA BAADA YA UJAUZITO

Profesa Lorraine Sherr, ambaye ni mwanasaikolojia wa chuo kimoja mjini London, anasema ujauzito unaweza kusababisha matatizo ya afya ya akili au kuchochea yaliyokuwapo.

Anasema kuwa jambo la muhimu la kufanya unapokumbana na tatizo la afya ya akili ni kuzungumza na watu na si kubaki nayo hiyo hali mwenyewe, tafuta msaada kwa wataalamu wa afya.

Anasema: “Kawaida ukipata jeraha unaenda kutafuta usaidizi, ni sawa na ukipata tatizo la akili unapaswa kufanya hivyo.”

Anna anasema alipata fundisho kubwa la namna fikra zake hazipaswi kumsukuma kufanya uamuzi. Lazima ziweze kukabiliwa.

Kuna unyanyapaa mkubwa katika tatizo la afya ya akili, lakini jamii inapaswa kuelewa tatizo na kuwasaidia watu pindi wanapokumbana na tatizo hilo.

 IFAHAMU SONONA

Kila mtu huwa anapata hii hali ya sonona anapokuwa hana furaha, ingawa huwa inachukua muda mfupi. Ukiwa na sonona akili huwa inavuruga mipango ya shughuli za kila siku na hivyo kusabisha maumivu kwa muhusika na watu wanaomzunguka.

Watu wengi huwa wanapata ugonjwa huu wa sonona lakini huwa hawatafuti tiba.

Daktari Christopher Peterson kutoka Hospitali ya Sanitas, iliyopo jijini Dar es Salaam, anasema huwa kuna aina nyingi za sonona lakini katika ukanda wetu wa Afrika, inayowapata watu wengi huwa ni ile ambayo inayomfanya mtu kushindwa kufanya kazi, kulala, kula na kufurahia maisha. Hii huwa inajirudia mara kadhaa.

Sonona nyingine ni ile ambayo huwa inawapata wanawake wanapotoka kujifungua na inakadiriwa kuwa asilimia 10 hadi 15 ya wanawake huwapata pindi wanapotoka kujifungua.

 DALILI ZAKE

Miongoni mwa dalili za sonona ni kujihisi unyonge, kukata tama, kuhisi kama umekosea na huna thamani, kuchoka, kukosa hamu ya kufanya shughuli yeyote ikiwa ni pamoja na kufanya mapenzi.

Dalili nyingine ni kukosa nguvu, kushindwa kuwa na kumbukumbu na kufanya uamuzi, kukosa usingizi, kukaa macho usiku kwa muda mrefu, kukosa hamu ya kula, kuwaza kujiua na kuumwa kichwa.

Dk. Peterson anasema mtu mwenye sonona ana tofauti kubwa na mtu mwenye kichaa. Anasema sonona haiwezi kusababishwa na vitu kama dawa za kulevya lakini kichaa kinaweza.

Mtu mwenye kichaa hawezi kujaribu kujiua huwa anafurahia maisha yake kwa hali ile ile aliyonayo, ambayo kila mtu anaona si maisha wakati sonona mtu anakuwa hana hamu ya kuishi na anashindwa kuiona thamani yake, hupoteza matumaini ya maisha kabisa.

Sonona inaweza kupona kwa ushauri nasaha au wa kiimani wakati mgonjwa wa akili ambaye ni kichaa hawezi kupona kwa njia hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles