28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Somalia yakana madai ya Kenya kuhusu mpaka

MOGADISHU, SOMALIA

SERIKALI ya Somalia imekanusha tuhuma za Kenya kwamba imepiga mnada visima vya mafuta ya petroli na gesi vilivyoko baharini.

Jumamosi iliyopita Serikali ya Kenya ilimrejesha nyumbani balozi wake mjini Mogadishu kwa mashauriano kuhusu mvutano wa mpaka wa baharini wenye utajiri mkubwa wa mafuta ya petroli na gesi.

Kenya ilichukua hatua hiyo kwa kile ilichodai uamuzi mbaya wa Somalia wa kupiga mnada visima vya mafuta na gesi vilivyoko katika eneo lake la bahari linalopakana na Somalia.

Lakini katika taarifa yake juzi Jumapili, Serikali ya Somalia ilisema ‘haina mpango wala haikuwa na mpango wa kufanya hivyo’.

Taarifa hiyo ilitolewa baada ya kuwepo ripoti za kikao kilichofanyika katika mji mkuu wa Mogadishu cha maofisa wakuu serikalini akiwemo Rais Mohamed Abdullahi Mohamed Farmajo na Waziri Mkuu Hassan Ali Khayre.

“Somalia kwa sasa haina mpango wala haikuwa na mpango wa kunadi sehemu yoyote katika eneo linalogombaniwa baharini hadi pale Mahakama ya Kimataifa ya Masuala ya Sheria (ICJ) itakapobaini mipaka ya nchi husika,” imeeleza taarifa hiyo rasmi.

Imeihakikishia Kenya kuwa haitojihusisha katika shughuli zozote katika maeneo yaliyo kwenye mzozo hadi mahakama itakapotoa uamuzi wa mwisho.

Awali Jumamosi jioni, Nairobi ilitangaza kumrudisha nyumbani balozi wake aliyepo Mogadishu, Luteni Jenerali mstaafu Lucas Tumbo, ikidai kuwa uamuzi wa Somalia kupiga mnada eneo moja la mafuta mjini London wiki iliyopita ni sawa na uchokozi dhidi yake na mali yake asili.

Pia ilimrudisha nyumbani balozi wa Somalia nchini Kenya, Mohamed Nur katika kile ambacho Serikali ya Kenya baadaye ilifafanua kwenye vyombo vya habari nchini kuwa ni kutoa fursa ya majadiliano ya kila upande katika suala hilo.

Aidha Somalia kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ilikuwa imeeleza masikitiko yake kufuatia hatua hiyo ya Kenya kumrudisha balozi wake pasi kuwepo mashauriano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles