MANCHESTER, ENGLAND
WAMILIKI wa timu ya Manchester United, familia ya Glazer, imemuhakikishia kocha wa timu hiyo Ole Gunnar Solskjaer kibarua chake kuwa sehemu salama baada ya ushindi wa wiki iliopita dhidi ya timu kubwa nchini England.
Kocha huyo alipewa michezo miwili kuweza kuokoa kibarua chake wiki iliopita mchezo dhidi ya Tottenham inayofundishwa na kocha wa zamani wa United, Jose Mourinho pamoja na mchezo mwingine dhidi ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Manchester City ikiwa chini ya kocha Pep Guardiola.
Mchezo wa kwanza ulipigwa kwenye uwanja wa Old Ttafford dhidi ya Tottenham na Manchester United ikafanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-1, huku mchezo uliofuata dhidi ya Manchester City kwenye Uwanja wa Etihad na Manchester United ikashinda mabao 2-1.
Kutokana na matokeo hayo, uongozi huo wa Manchester United umethibitisha hawana mpango wa kuachana na kocha huyo na kikubwa wanatakiwa kumpa muda ili aweze kuijenga timu hiyo vizuri.
Uongozi huo unaamini endapo nyota wao Paul Pogba atarejea kikosini na kuongezewa wachezaji wawili wakati wa Januari timu hiyo itarudi kwenye ubora wake. Wachezaji ambao wapo kwenye mipango ya kusajiliwa ni wawili katika safu ya kiungo na ushambuliaji.
Hata hivyo, miongoni mwa wachezaji ambao wanaweza kuwasajili ni nyota wa Atletico Madrid, Saul Niguez, mshambuliaji wa timu ya Red Bull Salzburg, Erling Haaland na kiungo wa Ajax, Donny van de Beek, lakini mchezaji huyo anawindwa na mabingwa wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Real Madrid mwishoni mwa msimu huu.
Kwa sasa Manchester United wanashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi huku ikiwa imecheza jumla ya michezo 16 na kufanikiwa kujikusanyia pointi 24.