Safina Sarwatt,Same,
Serikali mkoani Kilimanjaro imezidua soko la kuuza madini aina ya Metali na vito wilayani Same, kutokana na wilaya hiyo kuongoza kuwa na madini mengi kuliko wilaya zote za mkoani humo.
Wilaya zingine ambazo zimegundulika kuwa na madini kama hayo ni Mwanga, Rombo, Siha na Moshi Vijijini.
Akizungumza wakati alipokuwa akifungua soko hilo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk Anna Mghwira amesema soko hilo litakuwa likifanyika mara mbili kwa mwezi lengo ni kukuza soko la madini na kuongeza thamani .
Amesema soko hilo litaisaidia serikali kukusanya mapato sahihi yatokanayo na madini pamoja na kudhibithi utoroshaji wa madini lakini pia litasaidia kujua viwango vya uzalishaji madini aina Metali na Vito katika wilaya Same na kukusanya mapato sahihi.
“Kumekuwa na tabia ya baadhi ya wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kutorosha madini na kuikosesha serikali mapato hivyo kuanzishwa kwa soko hili katika wilaya hii litasaidia kudhibiti utoroshaji wa madini,”amesema.
Alisema kuwa kwa kipindi cha miaka sita mwaka tangu mwaka 2014 hadi kufikia mwaka huu sekta ya madini mkoani Kilimanjaro imeweza kuchangia mapato ya jumla ya Sh.936, 510, 303.19.