NA HARRIETH MANDARI- GEITA
SOKO kuu la dhahabu mkoani Geita linatarajiwa kuanza rasmi hivi karibuni, imefahamika.
Katibu wa Kamati ya Uanzishaji Masoko ya Madini ikiweamo dhahabu mkoani Geita, Ramadhani Mcharo amesema ujenzi wa soko hilo uko katika hatua za mwisho baada ya kukamilika kwa asilimia 85.
Mcharo alikuwa akizungumza katika kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa wa Geita juzi.
Awali kumekuwa na changamoto kubwa ya soko la dhahabu kiasi kwamba wachimbaji wengi wamekuwa wakihangaika kupata sehemu ya kuuzia bidhaa yao.
Wengi wao walilazimika kuuza nje ya nchi jambo ambalo lilikuwa likiikoseha serikali mapato na hata kuleta usumbufu mkubwa kwa wafanyabiashara hao.
Mcharo alisema kutakua na soko kuu mjini Geita na mengine madogo manane.
“Masoko madogo yataanzishwa katika maeneo yote yenye uchimbaji madini hali itakayosaidia kuondokana na changamoto ya soko,”alisema.
Alitaja maeneno ya uchimbaji ambako masoko madogo yataanzishwa kuwa ni Nyarugusu, Nyakagwe, Rwamgasa, Chato, Bukombe, Ushirombo na Masumbwe.
Alisema katika soko kuu kutakua na vyumba 14 kwa ajili ya wanunuzi wa dhahabu, ambavyo tayari vimekwisha kupata wanunuzi.
Mcharo alisema leseni za wanunuzi zipatazo saba zimekwisha kukamilika usajili na nyingine sita ziko katika hatua ya mwisho ya usajili.
Pia alisema wapo madalali wa dhahabu wapatao 114.
Ofisa Madini wa Mkoa wa Geita, Daniel Mapunda alisema kuwapo masoko hayo ya madini kutasaidia kuongezeka mapato ya serikali.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel alitoa rai kwa watendaji kuhakikisha fedha zinazopatikana zinatumika vizuri kwa kuzipa kipaumbele sekta muhimu kama afya na elimu.