Na Mwandishi Wetu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuweka mkazo zaidi kwenye sekta ya mwani ili kuzalisha bidhaa zenye ubora na kuzipatia soko la uhakika.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo 21 Agosti 2024, Ikulu Zanzibar alipozungumza na Balozi wa Umoja wa Ulaya, Tanzania, Christine Grau.
Amesema asilimia 99 ya wakulima wa zao la mwani Zanzibar ni wanawake, hivyo alimueleza balozi huyo kuangalia haja ya kuwaunga mkono wanawake na wakulima wa mwani nchini, hasa kwa mafunzo na vifaa vya kisasa ili wazalishe mwani wenye ubora utakaoendana sambamba na soko la uhakika.
Mbali na mambo mengine ya maendeleo na uwekezaji ikiwemo utalii, Rais Dk. Mwinyi pia amemueleza Balozi Grau kuwa Uchumi wa Buluu ni sera kuu ya uchumi wa Zanzibar, hivyo amemueleza kuangalia fursa zinazotokana na sera hiyo.
Kwa upande wake, Balozi Christine Grau amesifu juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dk. Mwinyi na kueleza kuwa wanafanya kazi kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo kushirikiana na jamii kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo na ustawi wa jamii Unguja na Pemba.