29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

SMZ haitamvumilia mtumishi yeyote atakayesababisha matumizi mabaya ya fedha za TASAF

Na James Mwanamyoto, Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya mtumishi yeyote atakayesababisha matumizi mabaya ya fedha za ruzuku zinazotolewa kwa kaya maskini kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini.

Makamu wa Pili wa Rais ameyasema hayo leo ofisini kwake alipotembelewa na ujumbe kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ulioongozwa na Waziri mwenye dhamana ya ofisi hiyo, Mohamed Mchengerwa.

Abdulla amesema Serikali itahakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya kuzinusuru kaya maskini Zanzibar, zinatumika kwa malengo yalikusudiwa ili kuboresha maisha ya kaya hizo.

“Ni lazima tuwe na nidhamu ya kutumia vema rasilimali za umma ikiwemo fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kuziwezesha kaya maskini,” Abdulla amesisitiza.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa amesema ofisi yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar inayoratibu masuala ya TASAF itahakikisha inasimamia vema matumizi mazuri ya fedha za ruzuku zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kuzinusuru kaya maskini.

Aidha, Mchengerwa amewataka Waratibu wote wa TASAF wa Tanzania Bara na Zanzibar kushirikiana katika kutoa elimu kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili kuwawezesha kutumia ruzuku wanayoipata kuboresha maisha yao.

Akiwa katika ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya TASAF ya Kituo cha Afya cha Kianga na shule ya Sekondari ya Fujoni, Mchengerwa amewataka watumishi wa kituo hicho cha afya na wananchi wanaofuata huduma kukitunza kituo hicho ili kiendelee kutoa huduma bora na kuondoa adha ya upatikanaji wa huduma za afya ambazo zilikuwa zikiwakabili kabla ya ujenzi wa kituo hicho.

Akizungumzia ujenzi wa jengo la shule ya Sekondari Fujoni, Mchengerwa amesema, jengo hilo litatatua changamoto ya kutokuwepo kwa chumba cha kufanyia mitihani kwa wanafunzi wa shule hiyo ambayo kwa muda mrefu walikuwa wakifanyia mitihani yao chini ya miti na kupata adha kubwa kipindi cha mvua.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga aliwashukuru wananchi wa Fujoni kwa jitihada zao katika kukamilisha ujenzi wa chumba cha kufanyia mitihani.

Mwamanga amemueleza Waziri kuwa mradi huo umetekelezwa kwa kasi kubwa sana katika kipindi kisichozidi miezi sita tofauti na maeneo mengine ambayo hutumia mwaka mmoja na kuongeza kuwa utekelezaji huo unatokana na ushiriki mzuri wa wananchi ambao walikuwa na hamu kubwa kuhakikisha wanafunzi wanapata eneo zuri la kufanyia mitihani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles