SIYO KILA MSANII NI KOMEDIANI

0
605

SOKO la filamu linazidi kuteketea. Kelele za kunusuru ni nyingi kuliko jitihada. Yapo mambo mengi yanayosababisha industry imomonyoke taratibu siku hadi siku.

Mara kadhaa nimekuwa nikiandika na kutaja sababu kadha wa kadha. Sijawahi kuchoka na niliahidi kuendelea kuandika hadi pale soko litakaporudi kwenye hadhi yake.

Leo naandika tena. Kuna hili tatizo la baadhi ya wasanii kujiingia kwenye komedi. Yaani msanii siku zote amekuwa akiigiza kwenye filamu na scene za kawaida, lakini ghafla  naye ameanza kucheza komedi.

Kimsingi ukiangalia kwa undani utagundua kuwa filamu za Kibongo siku hizi ni kama zinakwenda kwa mihemko na kufuata upepo wa soko.

Huu ndiyo ukweli ambao wasanii wengine wanaweza kuukataa, kwani kuna wakati msanii fulani akifanya filamu ya aina fulani na ikaonekana kukubalika au kupata mafanikio basi mrengo wa filamu nyingi unaanza kuwa wa aina hiyo kiasi kwamba zinafurika sinema za aina moja sokoni.

Mbaya zaidi, wasanii wetu wengi ambao hufuata mkumbo mara nyingi wamekuwa wakiharibu kwa sababu wanafanya vitu kwa kulazimisha.

Komedi mbali na kutakiwa kuchezwa na wasanii mahiri wa eneo la uchekeshaji lakini pia utunzi wake huhitaji kazi kubwa sana kwani kuchekesha siyo kazi ya kitoto kama ambavyo wasanii wetu wamekuwa wakifanya.

Ukiangalia filamu za wasanii ambao wamejipachika ukomediani utaona wazi namna walivyopwaya na matokeo yake wameonekana vituko tu na si wachekeshaji kama wanavyodhani.

Wengine wanabadili sura zao na hali yao ya kuongea wakidhani kwamba huko ndiko kuchekesha, wanashindwa kutambua kwamba uchekeshaji unaweza kufanywa bila hata mtu kujibadilisha kama wafanyavyo.

Ni vyema ikafahamika kwamba uchekeshaji ni kipaji na ni taaluma pia, si kila mmoja anaweza kuwa mchekeshaji na si kila mwigizaji anaweza kuigiza komedi kirahisi kama inavyofikiriwa.

Wakati mkiendelea kutafakari namna ya kurejea mlipotoka, ni vyema kila msanii akabaki kwenye nafasi yake. Si kila msanii anaweza kufanya kila kitu. Chagua kitu kimoja utakachoweza kukifanya kwa umahiri mkubwa.

Siyo kudandia kila kitu. Sanaa haipo hivyo. Wengine walilewa umaarufu, wakaendekeza starehe na kusahau kuwa usanii ni pamoja na ubunifu. Kama unalala klabu kila siku, huo ubunifu utatokea wapi?

Sitachoka kuandika. Nitaandika tena. Wikiendi njema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here