27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, December 7, 2023

Contact us: [email protected]

Sitta avaa udikteta

Samuel Sitta
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta

FREDY AZZAH NA ESTHER MBUSI, DODOMA

MWENYEKITI wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, ni wazi sasa ameamua kuvaa ‘joho la udikiteta’, baada ya kuitaka Serikali kuvibana zaidi vyombo vya habari.

Sitta ameonekana kuwa mmoja wa watu wanaoweweseka baada ya kuitaka Serikali kudhibiti vyombo vya habari vinavyorusha midahalo mbalimbali ya Katiba.

Bila kutaja jina la chombo husika, Sitta alionekana wazi kutofurahishwa na midahalo ambayo mwishoni mwa wiki iliyopita imefanyika jijini Dar es Salaam na kurushwa moja kwa moja na televisheni ya ITV.

“Kuna chombo kimoja kinachoshangaza sana, kinaongoza kwa midahalo na wanawaalika hawa (wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba) na wao wanaenda, na kinachoshangaza wanaitwa watu wa aina moja tu.

“Chombo hiki chenyewe kinajiweka kwenye mkingamo, Serikali ipo hapa inasikia,” alisema Sitta.

Wakichangia hoja ya mabadiliko ya kanuni iliyowasilishwa kwenye Bunge hilo jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge, Pandu Ameir Kificho, baadhi ya wajumbe walitaka kutungwe kanuni zitakazowafunga midomo Ukawa, Wajumbe wa Tume ya Jaji Joseph Warioba na kufukuzwa kwa wajumbe wa kundi la  201 ambao wameungana na Ukawa kususia Bunge hilo.

Baadhi ya wajumbe waliotoa hoja hizo, ni Mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangala (CCM), aliyesema itungwe kanuni itakayowabana watu waliotakiwa kuwepo ndani ya Bunge hilo, lakini kwa sasa wanalipinga wakiwa nje.

Alisema Tume ya Jaji Warioba ilishamaliza kazi, lakini bado wanaendelea kukosoa kazi inayofanywa na Bunge Maalum.

“Wajumbe wa tume kazi yao ilishamalizika, lakini sasa hivi kazi zao kila siku ni hili Bunge na kupotosha, ongeeni na wazee wenzenu muwaambie waache, waambieni muda wao umeisha,” alisema.

Alisema aliwahi kushiriki mdahalo na Jaji Warioba na alimuhoji ni wapi Bunge Maalum la Katiba lilipokosea, lakini hakuwa na jibu.

“Ninachokipendekeza leo, wewe na wazee wenzio, waambie hawa wazee watuache. Hawa wazee wamelelewa na taifa hili, haya ndiyo malipo yao. Ikishindikana iwekwe kanuni ya kuwabana,” alisema.

Dk. Zainab Gama, alisema kazi ya tume hiyo imeisha na sasa wasiendelee tena kuwaingilia.

Alisema itungwe kanuni itakayoruhusu Bunge hilo kumuita na kumuhoji mtu yeyote atakayelisema vibaya.

Wajumbe wengine walipendekeza itungwe kanuni itakayotaka wajumbe wa Bunge hilo wasipohudhuria mikutano kwa siku tano mfululizo bila taarifa, iwe wamejifuta kazi moja kwa moja.

Walisema kwa wajumbe wa kundi la 201, rais ateue wengine.

Wakati wa kuendelea kutoa michango yao, baadhi ya wajumbe hao walivilaumu vyombo vya habari ambavyo vinarusha mikutano mbalimbali.

Kwa upande wake, Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), alisema Bunge hilo linaweza kuendelea, lakini ni vyema kungekuwa na maridhiano ya pande zote.

Alisema kusiwe na kuharakishwa kwa Bunge hilo ili kupatikana kwa katiba na badala yake ikibidi baadhi ya vifungu vichukuliwe kwenye rasimu ya sasa na kuboresha katiba ya zamani.

Alisema kila kitu kinaweza kufanyika hata kupata theluthi mbili kwa kila upande na kuipitisha katiba hiyo, lakini ni vyema kuwepo na maridhiano na aina ya mfumo wa Serikali ambao ni msingi kwa kila kitu.

“Kujadili sura zote na kupiga kura mwisho bado tatizo halijaondoka, tatizo hapa kuna nchi mbili, watunzi wa rasimu wangetupa msingi wa Serikali moja, mbili, lakini hatuna hivyo vitu, tuna vya Serikali tatu, kama bado ujaamua mambo ya utawala itakuwa ni tatizo tu, tujenge mambo mengine yote, lakini kwanza tuamue aina ya utawala tunaoutaka,” alisema Cheyo.

KANUNI

Katika hatua nyingine, Sitta amebariki kufumuliwa kwa kanuni na kuandika upya baadhi yake, hali itakayoruhusu Bunge hilo kuendelea na shughuli zake bila kuwepo Ukawa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge, Kificho, aliwasilisha marekebisho ya kanuni 13 ikiwamo ile inayoruhusu suala la kupiga kura ili kupitisha sura mbalimbali lifanyike baada ya kujadiliwa kwa sura zote.

Awali kanuni hiyo ilikuwa inataka upigaji kura ufanyike kila baada ya kujadiliwa kwa sura mbili na kuandikwa na Kamati ya Uandishi.

Kutokana na hali hiyo, ilitegemewa baada ya Bunge kukutana kwa awamu ya pili, suala la kuanza kufanyika lingekuwa ni kupigia kura ibara ya kwanza na ya sita ambazo zilishajadiliwa na Kamati ya Uandishi ikapewa jukumu la kuandika.

Hata hivyo, hali hiyo ilionyesha ingekuwa kikwazo kwa Bunge hilo kuendelea na kazi zake kwani Ukawa wameendelea na msisitizo wa kutorudi bungeni, hivyo upatikanaji wa theluthi mbili kutoka Bara na Visiwani ili kukidhi matakwa ya sheria ilikuwa vigumu. “Kanuni ya 36 inapendekeza ifutwe na kuandikwa upya kwa lengo la kuainisha utaratibu utakaotumika wakati wa kupiga kura ibara ya katiba. Aidha inapendekeza upigaji kura kwa ibara za sura zote ufanyike kwa muda usiozidi siku zisizopungua 15,” alisema Kificho.

Ratiba ya mkutano wa Bunge hilo ambayo ilikuwa imeshagawiwa kwa baadhi ya wajumbe, inaonyesha upigaji kura ulitarajiwa kuanza Oktoba 10 hadi 21, huku Mwenyekiti wa Bunge akitarajiwa kuwasilisha katiba inayopendekezwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar, Oktoba 31.

Hata hivyo, Sitta alisema lengo la kubadilishwa kwa kanuni hizo ni kutoa mfululizo mzuri wa kujadili na kuandika katiba hiyo.

Alisema utaratibu wa awali ulikuwa unafanya kuwepo na mkanganyiko endapo suala moja lingepigiwa kura na kupitishwa kisha baadaye katika sura zinazofuata zikikataliwa, ingeweza kufanya wajumbe hao warudi na kupigia tena kura sura ambazo zimeshaamuliwa.

Marekebisho hayo, pia yanataka kila mjumbe asaini yeye binafsi karatasi ya mahudhurio iliyoandaliwa kwa ajili hiyo.

Kabla ya marekebisho, kanuni hiyo ilikuwa inamtaka mjumbe ambaye hatahudhuria vikao vitatu mfululizo bila sababu za msingi kupewa onyo kali na Mwenyekiti wa Kamati na endapo ataendelea mara mbili au zaidi, Mwenyekiti wa Kamati atalipeleka jina lake kwenye Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalum kupata ushauri wa hatua za kinidhamu zinazofaa kuchukuliwa dhidi yake.

Akizungumzia kuhusu marekebisho hayo, Kificho alisema kanuni zilizofanyiwa marekebisho ni ya 14, 15, 32, 32b, 33, 35, 36, 46, 47, 54, 60, 62 na 65 ambapo hayo yamependekezwa ili kukidhi haja na kuleta tija katika uendeshaji bora wa shughuli za Bunge Maalum.

“Kanuni ya 14 inapendekezwa kufanyiwa marekebisho kwa kufuta fasili ya (4) ili kuondoa sharti la Bunge Maalum kukutana Jumamosi, marekebisho haya yanalenga kuwapa wajumbe muda wa kupumzika na kufanya tafiti na mashauriano juu ya mambo mbalimbali yanayohusu rasimu ya katiba ili kuboresha michango yao wakati wa mijadala kwenye kamati na ndani ya Bunge.

“Katika kanuni ya 32, mapendekezo ya marekebisho katika fasili ya kwanza yanalenga kuondoa utaratibu uliokuwapo wa kila Kamati ya Bunge Maalum kujadili rasimu ya katiba kwa wakati mmoja kwa kuzingatia mgawanyo wa sura angalau mbili zinazofanana,” alisema Kificho.

Kwa mujibu wa Kificho, katika marekebisho haya kila kamati itajadili sura zote za rasimu ya katiba, na katika fasili ya pili kamati zitajadili sura za rasimu kwa muda usiozidi siku 15 ambao ni mfupi.

Aidha, kanuni ya 32b, imefutwa na kuandikwa upya kwa lengo la kuruhusu masharti ya kanuni ya 46 na 46a, yanayohusu Bunge Maalum juu ya mamlaka ya Mwenyekiti wa Bunge Maalum kutoa adhabu yatumike pamoja na marekebisho husika katika kuendesha majadiliano kwenye kamati.

Katika kanuni ya 33, ilipendekezwa kufuta maneno ‘dakika sitini’ na kuwekwa ‘dakika mia moja na ishirini’ kwa lengo la kuongeza muda wa kuwasilisha taarifa ya maoni ya wajumbe walio wengi sanjari na kufuta fasili ya (5), (6) na (7) na kuandikwa upya kwa lengo la kuongeza muda wa kuwasilisha maoni ya wajumbe walio wachache kutoka dakika 30 hadi 60 na pia kumpa mwenyekiti mamlaka ya kuweka utaratibu utakaozingatiwa wakati wa mijadala na taarifa za kamati na sura zote za rasimu zijadiliwe bungeni kwa muda usiozidi siku 16.

“Kanuni ya 35 inapendekezwa fasili ya (6) hadi (11) zifutwe na kuandikwa upya kwa lengo la kuweka utaratibu wa namna ya kujadili na kupitisha masharti ya sura za rasimu pamoja na mpya zitakazopendekezwa.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. Akipata Urais ndiyo itakuwa hatari, atabadilisha katiba ili atawale kama hayati rais Banda wa Malawi! hana uvimulivu na moyo wa kuwatumikia Watanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles