Na Maregesi Paul, Dodoma
MWENYEKITI wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, amesema wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ni sawa na waigizaji wa nchini Marekani.
Amesema ushahidi wa uigizaji huo utadhihirika mwakani baada ya kushindwa kwao katika uchaguzi mkuu wa kumchagua rais, wabunge na madiwani.
Sitta alitoa kauli hiyo yenye kila dalili za kuwaombea anguko kubwa wanasiasa wa upinzani wanaounda Ukawa wakati akizungumza bungeni jana muda mfupi baada ya kutambulisha wageni waliolitembelea Bunge la Katiba.
“Kule Marekani kulipata kutokea viongozi ambao ni wacheza sinema kama Ronald Regan na Gavana Arnold Schwarzenegger wa Califonia. Wananchi wa kule waliweza kuwahimili viongozi hao wanaofanya mzaha kwa sababu ile ni nchi tajiri, lakini sisi ni maskini hatuwezi kuhimili viongozi wa namna hii.
“Kwa hiyo natoa ushauri tu kwamba, mwakani watakaposhindwa vibaya wakati wa uchaguzi kutokana na tabia zao hizo, basi warejee katika fani ya uigizaji ambayo Mwenyezi Mungu amewajalia,” alisema Sitta.
Wakati huo huo, Sitta aliitumia fursa hiyo kubeza taarifa zilizoripotiwa katika baadhi ya vyombo vya habari jana zikiwakariri baadhi ya viongozi wa Ukawa wanaopanga kumshitaki katika Mahakama ya Uhalifu wa Kivita iliyoko The Hague, nchini Uholanzi.
Alisema wanaopanga mpango huo hawawezi kufanikiwa kwa sababu hakuna alichokosea baada ya kuamua Bunge Maalumu la Katiba liendelee.
“Kwenye magazeti wameripoti Ukawa wanapanga kunipeleka kule The Hegue. Sijui kama wenzangu mnajua baadhi ya hawa viongozi wa Ukawa wana kipaji kizuri cha uigizaji.
“Hebu fikirieni vituko vyao, tulipokutana hapa mwanzoni tulivutana siku 18 za kura ya wazi au ya siri. Siku ya kuzikubali kanuni, watu hao waliopigania kufa au kupona kura ziwe za siri, wakaamua kupiga kura za wazi,” alisema Sitta.
Akiendelea kuwalalamikia Ukawa, alisema mmoja wa wajumbe wake alipeleka hoja binafsi akitaka Bunge hilo lisiendelee hadi hati ya muungano itakapopatikana na ilipopelekwa nakala yake yakaibuka madai mapya kuwa sahihi ya Mzee Karume imeghushiwa na baadaye Aprili 16 ilipoletwa hati halisi, walisusia Bunge.
“Hivi majuzi Mheshimiwa Rais amekutana nao mara mbili kwa jumla ya saa saba, wakaafikiana mambo ya kufanya, lakini baadaye wakakanusha makubaliano hayo na kumfanya Mheshimiwa Cheyo (John Cheyo, Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), awaumbue kwa kueleza walichokubaliana.
Wakati Sitta akisema hayo, mjumbe wa Bunge hilo ambaye pia ni mwakilishi wa vyama visivyokuwa na wabunge katika kikao cha Rais Kikwete na TCD, Fahmi Dovutwa, alisema yeye na baadhi ya wajumbe wenzake walikataa kusaini waraka ulioandaliwa na wajumbe wenzake kabla ya kikao hicho kwa kuwa haukuwa na ujumbe mzuri.
Alisema kabla ya kusaini waraka huo, walitakiwa kuusoma ili waelewe kilichoandikwa, lakini Ukawa hawakutaka kutoa fursa hiyo kwa kuwa walijua walichokuwa wakikitaka.
“Kuna ‘document’ moja tunaambiwa tulikataa kuisaini. Hii ilitokana na sababu kwamba, hatukupewa muda wa kuisoma ili tujue kilichomo. Ile document tulipewa dakika za mwisho kabla ya kuingia kwenye kikao na rais na ilikuwa na kipengele cha hatari kwani ilikuwa ikimtaka rais ajae aendelee na mchakato wa Katiba baada tu ya kuingia madarakani,” alisema Dovutwa.
Kauli hiyo ya Dovutwa inapingana na kauli ya Cheyo aliyoitoa wiki hii wakati alipozungumza na waandishi wa habari na kuwaambia kuwa, hakuna waraka wowote aliokataa kuusaini pamoja na Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema na Dovutwa mwenyewe.
Wakati huo huo, Dovutwa ameliambia Bunge la Katiba kuwa ameanza kupokea simu za vitisho kutokana na msimamo wake wa kutaka Bunge hilo liendelee na vikao vyake.
Akizungumza jana wakati kikao cha Bunge Maalumu kikiendelea, alisema analaumiwa zaidi na baadhi ya viongozi kama Maalim Seif (Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar), kwamba yeye ni kibaraka wa CCM.
“Kutokana na msimamo wangu, juzi nimepokea simu tatu za vitisho, wanasema watanifanyizia, sasa najiuliza, mimi nitawezaje kuwahujumu CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi?” alisema Dovutwa.
Akieleza zaidi, alisema katika kikao cha TCD kilichofanyika Septemba 8 na kuhudhuriwa pia na Rais Kikwete, yalifikiwa makubaliano ya kufanya mabadiliko katika Katiba kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao na katika suala la kusitisha Bunge, ilionekana hakuna mtu mwenye mamlaka ya kulisitisha.
Alisema hata katika kikao cha Agosti 31, rais alimuuliza Tundu Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki, Chadema), kuwa anataka alivunje Bunge kwa kutumia sheria gani wakati anajua hana mamlaka hayo na Lissu alikosa majibu.
Pia aliwalaumu Ukawa kwa kile alichosema wanataka kukwamisha mchakato wa Katiba ili Rais Kikwete aonekane hafai katika jamii.
Hili zee limechanganyikiwa, kuishiwa na kuhaka. Sitta kapimwe akili maana huna tofauti na Augustine Mrema na vichaa wengine wanaoendeshwa na matumbo yao