24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Sitta adaiwa kutumia Bunge la Katiba kusaka urais

Samuel Sitta
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta

NA ELIZABETH HOMBO

MBUNGE wa Mkanyageni, Habib Mnyaa (CUF) amesema Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, anataka kulitumia Bunge la Katiba kwa nia ya kufanikisha dhamira yake ya kutaka urais.

Mnyaa alisema ni jambo la kushangaza kuona Sitta akihangaika kusaka suluhu na wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Akizungumza na MTANZANIA Jumatano, Mnyaa alisema ni jambo lisiloingia akilini kwa Sitta kutaka kuwasuluhisha huku akijulikana wazi anasimamia kile kinachoaminiwa na chama chake.

“Mambo mengine yanashangaza … hivi tutakuwa na suluhu gani na Sitta, wanatufanya hatuna akili, Sitta yeye anaunga mkono Serikali mbili na ndio msimamo wa chama chake na si siri kuwa anatumia mchakato huu kutaka kugombea urais wa nchi,” alisema Mnyaa.

Alisema CCM hawataki Katiba Mpya ipatikane kabla ya uchaguzi kwa sababu wanajua ikipatikana kuna vipengele vitawabana.

“Ni ukweli ulio wazi kuwa CCM hawataki Katiba ipatikane kabla ya uchaguzi kwa sababu wanajua inawabana kwenye mambo mbalimbali,” anasema.

Alieleza kushangazwa na hatua ya baadhi ya watu kuwataka warudi bungeni huku wale waliobadilisha rasimu ya Katiba na kujadili ya kwao wakiachwa.

“Mbona walileta Katiba yao yenye Serikali mbili hawazungumziwi, lakini watu wameng’ang’ania Ukawa warudi bungeni, tutarudije wakati CCM wamekuja na rasimu yao ya Serikali mbili badala ya tatu iliyopo kwenye Rasimu iliyowasilishwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.

“Kwanini tusijadili hii rasimu halisi ya Serikali tatu halafu inapoenda kwenye maoni ya wananchi ikataliwe huko? Kwanini CCM wanalazimisha mambo?” Alihoji Mnyaa.

Alishauri kuwa endapo Katiba Mpya haitapatikana kabla ya uchaguzi, marekebisho yafanyike kwenye Katiba ya sasa hususan kuwepo tume huru ya uchaguzi, kura ya maoni na daftari la wapiga kura.

Sitta alipotafutwa ili kuzungumzia madai ya Mnyaa, hakuweza kupatikana, hata hivyo katika siku za karibuni Mwenyekiti huyo wa Bunge la Katiba, amekuwa mstari wa mbele kusaka suluhu ili kuhakikisha mchakato wa Katiba Mpya unaendelea.

Katika kuhakikisha nia ya kupata Katiba Mpya inafanikiwa aliunda Kamati ya Maridhiano iliyowahusisha wajumbe kutoka vyama vyote vya siasa pamoja na wale wanaotoka kwenye kundi la wajumbe 201.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. Hoja kubwa ni hiyo ya ndugu Mnyaa kwamba badala ya kubadili rasimu, ijadiliwe hii ya wananchi na baadaye ipelekwe kwa wananchi wao watapigia kura, kama ni kukataa maoni yao wenyewe basi wakayakatae wao lakini siyo kupenyeza sera za CCM. Na hoja kubwa ni hiyo tu watanzania tumeshaelewa isipokuwa wanaCCM na uongozi wao, wana agenda yao ya siri ambayo haitafika mbali. “Sauti ya wengi (siyo ndani ya Bunge la katiba) ni sauti ya Mungu”, Wananchi waliotoa maoni ni wengi kuliko hawa wanaotaka kuyachakachua ndani ya Bunge la Katiba. “Vita kati ya Mungu na Binadamu nani atashinda?”. Jibu unalo ni kwamba Mungu atashinda. Tukae natusubiri.

    • Nami naunga mkono hii hoja ya Mnyaa kwamba badala ya kubadili rasimu, ijadiliwe hii ya wananchi na baadaye ipelekwe kwa wananchi ikapigiwe kura. Kama madai ya CCM ni ya kweli kwamba chaguo la muundo wa serikali 3 halikuwa la watanzania walio wengi ukweli utajulikana kutokana na kura ya maoni. CCM inangangania kubadili pendekezo la serikali 3 kwa sababu inaelewa fika kwamba hilo ndio chaguo la watanzania waliowengi na hivyo kwenye kura ya maoni ni lazima lipite.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles