Sitakuwa ‘mnafiki’ kama ole Millya na wenzake

0
1779
Aliyekuwa Mbunge wa Simanjiro, James Ole Milya

SIASA inaendelea kubaki kuwa siasa. Hakuna wa kuibadili.

Duniani kote, siasa imekuwa ni mchezo unaoendeshwa kwa fitna, hakuna wa kutenganisha mambo haya mawili. Siasa na fitna ni mapacha walioungana, ambao hakuna wa kuwatenganisha, ndivyo mfumo ulivyojengwa.

Wakati nikiendelea kutafakari kile alichokizungumza Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally na yanayoendelea kutokana na kauli yake aliyoitoa mwishoni mwa wiki iliyopita, kuhusu wananchi kukata tamaa kushiriki katika chaguzi kutokana na kutokuwa na imani na mifumo ya uchaguzi, mapya yanaibuka.

Kauli ya Dk. Bashiru, Mwalimu wa Chuo Kikuu aliyebobea katika Sayansi ya Siasa na Uongozi kuhusu kushuka kwa morali ya wapiga kura ambao wamekuwa wakijitokeza kwa kiasi kidogo, kisichozidi asilimia 50 ya waliojiandikisha inafikirisha.

Suala hili nimelizungumza mara kadhaa katika makala zangu, hasa kutokana na mahojiano niliyowahi kuyafanya na baadhi ya wananchi baada ya uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo ya Kinondoni na Siha.

Inawezekana ameamua kufanya tofauti, kutokana na nadharia zake alizozizoea katika tafiti ambazo amekuwa akizifanya na kuzitumia darasani, inawezekana anajaribu kuliweka katika vitendo sasa, akitarajia mafanikio katika mamlaka yake aliyonayo.

Hoja hii inahitaji muda na ufuatiliaji wa karibu, kwa kuwa tunaofuatilia tunaelewa kuwa siasa za Tanzania na kote duniani msingi wake ni ‘fitna’, hivyo tunawaachia wataalamu wa fitna waliopo ndani ya chama chake kuendelea kutumia fitna kulinda nafasi zao. Ninaona muda ndio utakaoeleza.

Kwa sasa turejee katika hili linalohusu wanasiasa wanaojinasibu kujiuzulu ubunge kutoka katika vyama vya upinzani, kisha kurejea katika nyadhifa zao hizo kwa kuwania tena kupitia CCM, chama kilichowapokea na kuwapa mbeleko katika chaguzi za marudio.

Kwa hesabu ya haraka, wabunge wanne wameshafaidika na ‘ofa’ hiyo inayodaiwa imewanusuru katika madeni makubwa waliyokuwa wamekopa katika maeneo mbalimbali na sasa wanaweza kuishi kwa uhuru.

Wanaoeleza hayo wanaweza kuwa na ushahidi, kwa kuwa ni suala la ‘pata nipate’ linalompa ubunge ujasiri wa kuachia nafasi yake na kurejea katika nafasi hiyo hiyo, bila hata kupitia mchakato wa kura ya maoni ndani ya chama, suala ambalo linaweza kutafsiriwa kama mwendelezo wa ‘rushwa ya uchaguzi’ aliyoizungumzia Dk Bashiru wiki iliyopita. Hakuna suala linalofanyika bila faida.

Hoja ya msingi hapa ni kwamba kwa wanaohama, wanashawishiwa na CCM na dola kwa namna ambayo ni siri yao kwa kuwa bila kushawishiwa na kuhakikishiwa ahueni ya mizigo yao ‘binafsi’ hawawezi kuhama, Bajeti zote, ya kuwashawishi na ya uchaguzi mdogo zinakuwa zimeshaandaliwa.

Wabunge wanne ambao tayari wameshanufaika kwa kuhamia CCM na kurejeshewa ubunge wao ni Maulid Mtulia (Kinondoni-CUF), Dk. Godwin Mollel (Siha- Chadema), Julius Kalanga (Monduli- Chadema), Mwita Waitara (Ukonga- Chadema).

Wengine ambao wametangaza kujiuzulu ubunge kwa kisingizio cha kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli huku wakibeza vyama vilivyowasababisha kuonekana na kupata ubunge huo ni Zuberi Kuchauka (Liwale- CUF), Marwa Chacha (Serengeti) na mwishoni mwa wiki iliyopita, mbunge wa Simanjiro (Chadema), James Millya aliungana nao.

Hawa watatu nao wanaendelea kujihakikishia kurejea katika nafasi zao kupitia CCM, huku tayari Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole akitangaza muda wa ukomo kwa wale ambao wanahitaji kujiuzulu ubunge na kuwania tena katika chaguzi ndogo kupitia CCM ni mwaka 2018.

Ikumbukwe tu kwamba kwa mujibu wa sheria za uchaguzi, chaguzi ndogo zinatakiwa kufanyika hadi itakapobaki miezi 18 kabla ya uchaguzi mkuu unaofuata, hivyo haziwezi kufanyika baada ya Machi mwaka 2019.

Kwa watakaojiuzulu Desemba 2018 watapata nafasi ya kuandaliwa chaguzi hizo hadi Machi mwakani, ndani ya muda wa ukomo uliopo kwa mujibu wa sheria za uchaguzi.

Ikumbukwe pia mwaka 2019 ni mwaka wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kwa hiyo Polepole na wenzake wanajipanga kwa ajili hiyo hivyo lazima wahitimishe mpango wa hamahama ya wabunge na madiwani.

Tangazo la Polepole ni hitimisho la hamasa kwa wabunge wengine wanaotajwatajwa kuwa katika mpango wa kuhama ambao ni Wilfred Lwakatare (Bukoba Mjini-Chadema), Magdalena Sakaya (Kaliua-CUF), Jafary Michael (Moshi Mjini-Chadema), John Mnyika (Kibamba-Chadema), Joshua Nasari (Arumeru Mashariki-Chadema), Saed Kubenea (Ubungo-Chadema) na Esther Bulaya (Bunda Mjini-Chadema), Japokuwa wote wamekanusha.

Iwapo hao pia watatangazaa kujiuzulu, kwa pamoja au mmoja mmoja, si tatizo kwa sababu kwa mujibu wa mtazamo wao na kwa hali halisi, wanatimiza matakwa yao binafsi na ni haki yao ya kidemokrasia, ambayo haiwalazimishi kuheshimu haki ya kidemokrasia ya wale waliowachagua, ambao watarudi tena kuwaomba kura kwa mara nyingine.

Suala linalokera ni kiwango cha juu cha unafiki, cha kujaribu kutangaza kukifia chama wakati wakiwa kwenye mipango ya kukihama chama na kuachia ubunge, kisha kutafuta ‘njia ya dhihaka’ ya kukihama chama na kutafuta namna ya kuchafua chama anachotoka, kilichomfikisha hapo alipo.

Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili ya Oxford: Mnafiki- ni mtu anayesema kinyume na anavyotenda; mtu anayetoa ahadi kisha asitimize.

Ufafanuzi wa Kiswahili katika Wikipedia, unaeleza kuwa: Unafiki ni utovu wa ukweli katika mwenendo wa binadamu hasa kwa lengo la kujipatia sifa. Mnafiki anatenda vema kwa nje, lakini nia yake si kufuata dhamiri yake na maadili anayojua ni mazuri, bali ni kupendeza watu wengine ili kupata faida fulani kutoka kwao.

Kwa mtazamo wake, Millya kama ambavyo wengine walioondoka Chadema na CUF wanaeleza, anaungana nao kusema kuwa chama cha siasa kinapaswa kuwa taasisi yenye mwelekeo wa kiitikadi na inayowatuma wawakilishi akiwamo yeye kuwahamasisha wananchi kushirikiana na Serikali kutafuta na kuleta maendeleo na si vinginevyo, huku akijua kwamba chama alichokuwamo kinahitaji kushika dola na hakiwezi kushika dola kwa kuisifu Serikali iliyopo madarakani. Ni unafiki huu.

Millya haendi mbali na wenzake sita waliojivua uanachama na ubunge, anasema kinachosikitisha badala ya kusimama pamoja katika mafanikio ya Rais Magufuli na kumsaidia kwa kumpa mbadala wa hoja na mipango, matokeo yake upinzani umekuwa na kazi ya kubeza na kuponda chochote kinachofanyika. Ni unafiki wa kiwango cha juu huu, anajua wazi kwamba mengi yanayotekelezwa ni sehemu ya hoja na mipango mbadala.

Akipita katika nyayo za waliomtangulia, anasema bahati mbaya hata pale yanayofanyika na kugusa na kubadilisha maisha ya Watanzania, wanamkosoa, na kwamba hizo si siasa alizokuwa akizitarajia upinzani zifanye katika Taifa ambalo lina kazi kubwa la kukombolewa kiuchumi. Kama si unafiki, sijui alitarajia upinzani ufanye nini?.

Mimi ninasema, iwapo nikiwa mbunge kama walivyokuwa hawa waliohama kutoka upande mmoja kwenda mwingine, nitafanya tofauti kwa kuzingatia ukweli na kueleza kwa uwazi mambo binafsi yaliyonisibu na kunisukuma kuhama, si kutumia njia za kinafiki za kujengeana ubaya kwa matatizo yangu.

Nikiwa mbunge kwa nafasi niliyochaguliwa na wananchi, kama mwanasiasa, fitna ni jambo lisilokwepeka, ila nitafanya tofauti, sitatumia fitna wakati wa kuondoka katika chama kilichonibeba kwenda chama kinachonipokea, nitakuwa muungwana kwa vitendo na kuuishi uungwana kwa kuwaaga vizuri hawa waliokuwa nami kwa kipindi chote, hadi nikaonekana na kushawishiwa.

Kweli, nitafanya tofauti, wakati wa kujivua uanachama baada ya kushawishiwa na upande mwingine na kuahidiwa ‘mazingira na malisho ya kijani’ huko niendako, nitayachukua madhaifu yao kama sehemu yangu kwa kuwa nilikuwa sehemu yao katika kipindi chote tulichokuwa pmoja na sikuweza kufanya lolote kuyarekebisha.

Nitafanya tofauti, nitatoa shukrani kwa chama hiki kilichonipokea, kunipa nafasi na kunifikisha hapa nilipo kwa kuwa tayari kitakuwa kimechangia katika historia ya maisha na harakati zangu na ndicho kilichonifikisha katika mafanikio niliyonayo leo na nitaweka kando kasoro au tofauti ndogo ndogo zilizowahi kujitokeza wakati wa utendaji wetu wa kila siku, ni kweli, sitakuwa mnafiki.

Nikiwa mbunge ambaye ninataka kujivua uanachama kwa siku zijazo na kisha kuachia ubunge wangu kwa nia ya kuuwania tena katika chama kipya kinachotarajia kunipokea, nitafanya tofauti, sitafuata nyayo za wanafiki waliotangulia, nitajenga mazingira mapya ya kiungwana yatakayokuwa mfano kwa wengine walioko mbioni, nitaonesha njia mpya ya kufanya ‘siasa zenye staha’  kwa kutambua mchango wa huku ninakotoka, nikitarajia kutoa na kupokea mchango wenye manufaa huko ninakokwenda.

Nitafanya tofauti, nitahakikisha ninajenga na kutekeleza kwa vitendo dhana ya ‘siasa si uadui’ na kutoa fursa ya demokrasia inayonijenga mimi na taswira yangu kwa umma, hata kama nimeshawishiwa na kushiriki katika ‘Bajeti maalumu’ ya kuninasua katika mizigo yangu ya madeni na mikopo niliyoibeba, ambayo kwa utashi wangu nimeamua kuitumikia ili kumaliza matatizo yanayonikabili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here