Na Paul Kayanda, Kahama
JESHI la Polisi Mkoa wa Shinyanga limewatia mbaroni watu sita wakiwa katika harakati za kuuza viungo vinavyosadikiwa kuwa vya binadamu mwenye ulemavu wa ngozi (albino).
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, alisema watuhumiwa hao walikamatwa Mei 20 mwaka huu saa saba mchana wakiwa katika nyumba ya kulala wageni iliyopo Mtaa wa Phantom, Kata ya Nyasubi wilayani hapa.
Alisema katika msako huo ulioendeshwa kwa kushirikiana na ofisa wa polisi Nzega, ulifanikiwa kuwatia mbaroni Bahati Kirungu (56), Mwalimu wa Shule ya Msingi Katungulu iliyopo Kata ya Wendele Kahama, Mhoja John (24), Bilia Busanda (39), Aboubakary Ally (25), Shija Makandi (60), Regina Kashinje (40) wote wakazi wa Nzega mkoani Tabora.
Alisema Mei 19 mwaka huu walipata taarifa za kuwapo kwa watu waliokuwa wakitafuta soko la viungo vya albino na hivyo kuweka mtego uliofanikiwa kuwakamata baada ya kufikishwa Kahama walikoelezwa kuwapo mteja.
Aliwashukuru wananchi kwa kutoa taarifa na kuwaomba kuendelea na ushirikiano huo ili kukomesha vitendo hivyo.
Alisema watuhumiwa waliokamatwa bado wanafanyiwa mahojiano zaidi ili kukamilisha masuala kadhaa ya uchunguzi na baada ya kukamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.