27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Sisi ni Watanzania, sisi ni Wahadzabe – 2

001

Na MARKUS MPANGALA,

WIKI iliyopita tulianza kueleza simulizi za hostoria ya jamii za Wahadzabe, kama zilivyoandikwa na Daudi Peterson akishirikiana na Richard Baalow na Jon Cox kwenye kitabu cha “Wahadzabe kwenye nuru ya mioto milioni’. Tuliona namna ambavyo Wahadzabe walivyomwamini Haine (Mungu wao) pamoja na asili zao. Endelea…

Miongoni mwa simulizi za kusisimua zaidi ni zile zinazoeleza asili ya Wahadzabe kutoka kwa Ikanawangube’e Kenebe’e ikiwa na maana yana watu wa kwanza kuanzisha ukoo wa Wahadzabe. Pia kuna  Gelanebe’e watu wazima walioumbwa kutokana kwa watu wa Twiga wa Ikanawangube’e Kenebe’e(uk.12&13).

Tunaelezwa historia ya jamii za Wahadzabe wa kwanza ni kutoka kwa Mhadzabe Tsiikayo aliyekamatwa na zimwi Duduk’we. Chanzo cha kukamatwa kwake kilitokana na na sherehe kubwa iliyoitishwa na Mtemi Kitentemi wa Wanyisanzu, ambapo aliachwa nyuma na wenzake walipokuwa wakitoka shereheni. Ndiyo ukawa mwanzo wa kukamatwa kwake.

“Hadithi ya chanzo chetu ya hivi karibuni inafanana na Mtemi Kitentemi wa Wanyisanzu ambaye hapo zamani za kale aliwakaribisha Wahadzabe kwenye sherehe kubwa. Kwenye sherehe hiyo Wahadzabe wengi walipewa sumu na kufa. Kitentemi alikuwa mtu tunayemwita rafiki wa tumbaku na bangi-asiyekuwa rafiki wa kweli.

“Walioponea chupuchupu kufa kwa sumu walihama na kuelekea Anau (iliyoko mashariki) Dilodabe’e (iliyoko magharibi) na Sanzako (iliyoko kaskazini). Haya makundi makuu matatu ndiyo chimbuko la vikundi vinne  vidogo vidogo vya kijiografia ambavyo ni Wa-Sipungamebe’e, Wa-Dundamebe’e, Wa-Tli’ikanebe’e na Wa-Mangolanebe’e. Baada ya tukio hili palitokea njaa kali kwa Wanyisanzu,

“Ili wapate kupona, Wanyisanzu wengi walihama kuja kuishi na Wahadzabe ili wafaidike na vyakula vya porini ambavyo haviathiriwi na ukame kama ilivyo kwa mazao ya chakula yanayolimwa. Wimbi hili la uhamiaji lilisababisha kuoana na kuzua ile hadithi kwamba Wahadzabe walitokea Ukerewe katika eneo la Ziwa Victoria ambalo ndiko walikotokea Wanyisanzu na siyo Wahadzabe,”(uk.21).

Tofauti na simulizi nyingi, ni kwamba kitabu hiki kinachimbua kinaga ubaga kuhusiana na jamii ya Wahadzabe ambao kwa namna moja ama nyingine imekuwa ikiishi kwenye maeneo tofauti na wakazi wengine.

Imezoeleka kuwa watu wote wanatakiwa kuishi kwenye makazi rasmi ama nyumba ambazo hujengwa kwa matofali na kadhalika. Lakini maisha ya Wahadzabe yamekuwa mistuni na wanaishi kwa kutegemea uwindaji na shughuli nyinginezo za kiuchumi.

Mathalani, mwandishi wa kitabu hiki anatusimulia namna ambavyo Wahadzabe wanavyofanya shughuli zao za uwindaji kama njia ya kujipatia kitoweo. Anasema shughuli za kiuchumi za Wahadzabe zinaegemea kwenye uwindaji wa kutumia upinde na mishale. Aidha, anabainisha kuwa Wahadzabe hawali wanyama wanaotambaa au viumbe wa majini yaani samaki wa aina yoyote.  Vilevile mwandishi anatueleza kuwa Wahadzabe wanawake na watoto wanaruhusiwa kula Kobe mwenye madoa kama chui, lakini wanaume ni mwiko kula kobe akiwa na mishale ya sumu. Hilo ni kutokana na imani zao, ambazo wamezirithi kutoka kale yaani Mababu wa Kihadzabe.

Kwenye uwindaji Wahadzabe wanatumia mishale ya aina tatu; kuna mishale ya hiko, ambayo  ni mahususi kwa ndege na wanyama wadogo yenye ncha za miti. Pili mishale ya kasama ambayo ni kichwa kipana cha chuma kilichopondwa kukifanya hapa, hutumiwa kwa ajili ya digidigi ama mnyama aliyejeruhiwa.

Pia kuna Iinako, mishale ya chuma yenye ncha moja, wa kiume na nchi mbili wa kike ambayo ina sumu na mipini yake ni ya kupachikwa kutumika kwa wanyama wakubwa. Anasema mti unaopendelewa kwa ajili ya mishale ya iinako ni  tlebako, kongoroko na kwa nadra embereko Uk.42).

Ndani ya kitabu hiki utapata simulizi mbalimbali kuhusiana na majina ya ndege, wanyama, maeneo na kadhalika. Yapo maelezo mbalimbali pia kuhusu maeneo na mengine ambayo yanawatambulisha Wahadzabe kama jamii ambayo imejikita kulinda utamaduni wao kizazi hadi kizazi. Bahati mbaya Wahadzabe ni jamii inayokabiliwa na uhaba wa ardhi kufuatia jamii za jirani kumega ardhi zao mara kwa mara.

Kutokana na mtindo wao wa kuishi kijadi kumechangia kuona ardhi zao ni kama vile hazina mmliki (Terranulius). Lakini pia wapo wanaoelimika kwa elimu ya kisasa na wamekuwa chachu ya mabadiliko madogo ndani ya jamii yao. Kwa hakika Wahadzabe wanayo mengi ya kusimulia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles