24.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

SIRI YA NJUGU KWA AFYA YAFICHUKA

vigna_subterranea_4350578751
Njugu mawe

 

ULAJI wa gramu 20 tu za jamii ya njugu kila siku huondoa theluthi moja ya uwezekano wa kukumbwa na kifo cha mapema, utafiti unabainisha.

Jamii ya njugu hasa walnuts, mbegu za alizeti na pekani zina kiwango kikubwa vya vitoa sumu (antioxidants) na hivyo kuwa na uwezo wa kulinda mwili dhidi ya uharibifu wa seli.

Njugu, ambazo kiufundi iko katika jamii ya mikunde, inaleta afya mno kiasi kwamba utafiti unadhani hata siagi inayotokana jamii ya karanga inaweza kurefusha maisha marefu, ijapokuwa sukari na chumvi zilizomo zinaweza kufuta baadhi ya faida.

Uchambuzi wa tafiti 20 uliofanywa na Chuo cha Imperial cha London, Uingereza ulibaini kuwa watu wanaokula kila siku wakia ya njugu wanapunguza hatari ya kupatwa na maradhi ya mishipa ya moyo kwa karibu theluthi moja na hatari ya kupata saratani kwa asilimia 15.

Utafiti unaonesha zinaweza pia kuzuia watu kufa kutokana na maradhi ya upumuaji na kisukari ijapokuwa kuna ushahidi mdogo kuhusu hilo.

Mwandishi mwenza wa ripoti ya utafiti huo, Dk. Dagfinn Aune, kutoka Shule ya Afya ya Umma katika chuo hicho cha Imperial, alisema: ‘Tulibaini kupungua kwa kiasi kikubwa kwa hatari ya kupata maradhi mengi, ambayo ni kiashiria kikubwa cha uwapo wa uhusiano baina ya njugu na matokeo mbalimbali ya kiafya.

Ni matokeo mazuri mno kwa kiwango hicho kidogo cha chakula.’

Tafiti za awali ziliwahi kueleza kwamba karanga hulinda dhidi ya maradhi ya moyo na kuzuia vifo vya mapema, lakini kulikuwa na ushahidi mdogo kuhusu namna zinavyodhibiti hatari ya maradhi ya saratani na mengineyo.

Utafiti unaashiria kwamba njugu aina ya walnuts zinaweza kuwa nzuri zaidi katika kuondoa saratani na karanga halisi hupunguza hatari ya kupata kiharusi.

Kula njugu kwa wingi kwa siku kunaweza kuhusisha njugu tatu kavu zenye mbegu moja ndani ya ukuta wa ovari ambao unakuwa ngumu wakati wa ukomavu wake. Aina hii ya njugu ni pamoja na walnuts, almondi, hazelnuts, korosho, pistachios na pekani.

Hata hivyo njugu za Kibrazil (Brazil nuts) ambazo ni mbegu na karanga, zinazowekwa katika daraja la mikunde, zilionekana kuwa na virutubisho vinavyofanana.

Pamoja na uwapo wa mafuta kwa wingi, njugu zote hizi zinajenga afya kwa sababu zina mafuta yenye lehemu nzuri ya poly-unsaturated, wakati huo huo pia zikiwa na nyuzi nyuzi, magnesium na vitamin E.

Inaaminika kuwa hulinda dhidi ya maradhi ya moyo na mishipa ya damu kwa kusaidia mwili kuvunja vunja lehemu na kuondoa ukinzani wa mwili kwa insulin.

Utafiti huo uliofanywa na Imperial College London na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Norway na kuchapishwa na jarida la Tiba la BMC unakuja baada ya ule wa Chuo Kikuu cha Havard nchini Marekani.

Utafiti huo uliofanywa na taasisi ya tiba ya chuo hicho, ulisema ulaji jamii ya karanga husaidia kurefusha maisha kwa miaka miwili hadi mitatu.

Utafiti huo uliochukua miaka 30 unasema tabia ya ulaji wa karanga, korosho, alizeti au almonds mara kwa mara una faida kwa miili yetu kwa vile zina virutubisho na madini mbalimbali ambayo husaidia ufanyakazi bora wa mwili.

Aidha Taasisi ya Chakula na Dawa (FDA) ya Marekani, inashauri kuwa ulaji wa njugu katika mlo kila siku kwa kiasi kisichopungua gramu 43, ambacho ni sawa na ujazo wa karanga kwenye kiganja cha mkono.

Sababu kuu ni kuwa njugu hupunguza hatari ya mtu kupata magonjwa ya kisukari, moyo, shinikizo la juu la damu na saratani ya utumbo.

Magonjwa haya kwa kiasi fulani huchangiwa na sumu zinazijikusanya mwilini.

Kwa sababu hiyo, utafiti uliona kuwa njugu zina virutubisho na madini ambayo hupunguza sumu mwilini ambazo huchangia kutokea kwa magonjwa haya.

Kwamba karanga zina mkusanyiko wa virutubisho vingi ikiwa ni pamoja na protini, wanga, mafuta ya omega-3, na omega -6, madini, vitamini na vitoa sumu mwilini .

Aidha utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Purdue nchini Marekani unasema njugu aina ya almond ina manufaa mengi mwilini kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha protini na virutubisho vingine vyenye kusaidia kuratibu mfumo mzima wa mwili ikiwamo maradhi ya moyo, kisukari.

Ni kwa vile zina uwezo mkubwa wa kupunguza kiwango cha lehemu ndani ya mwili pamoja na kuimarisha mifupa, misuli, viungo na kukabiliana na shinikizo la damu

Aina hizi za karanga, zile ambazo hupatikana kwa wingi Tanzania na mataifa jirani ni pamoja na karanga, korosho, ufuta, alizeti na almondi.

Aina nyingine kama vile chestnuts, hazelnuts, walnuts na pestachio hazipatikani kwa wingi ukanda huu ila zinaweza kupatikana katika maduka makubwa ya kisasa zikiwa zimetoka nje ya ukanda wa Afrika Mashariki au bara Afrika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles