.Wazazi wafunguka jamii inavyowatazama kwa sura mbili tofauti
. Wenyewe waeleza kiini cha wao kuamua kuwa watawa
Na Upendo Mosha- Rombo
FAMILIA yenye watoto wanne watawa (Mapadri) wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi, imesema licha ya wao kuona kuwa imebarikiwa, jamii imekuwa ikiwabeza kuwa wamekatisha uzao wa ukoo wao na wengine wakiwapongeza.
Watoto hao wanne wa familia moja wamefanikiwa kupata upadrisho kwa nyakati tofauti Jimbo la Moshi.
Hivi karibuni taarifa zao zimekuwa zikisambaa katika mitandao ya kijamii na kuzua hisia tofauti kwa wananchi.
MTANZANIA ilifunga safari hadi nyumbani kwa kwa wazazi wa mapadri hao Kijiji cha Kiraeni wilayani Rombo ambako baba yao mzazi, Inyasi Mkwe, alisema jambo hilo ni baraka katika familia hiyo licha ya jamii kulichukulia kwa namna tofauti.
“Jambo hili limekuwa ni baraka kwa familia yangu. Pamoja na kwamba wapo wanaotupongeza, lakini wapo wanaobeza kwamba ukoo umekatika, hamna namna nyingine ya kuzaliana jambo ambalo si kweli,” alisema.
Inyasi alisema yeye na mkewe Angelista, walibarikiwa kupata watoto saba ambao kati yao watano ni wa kiume na wawili wa kike.
Alisema mtoto mmoja wa kiume ameoa, wawili wa kike wameolewa na wanne waliobaki ndio mapadri.
“Kweli jamii imekuwa ikituchukulia kwa namna wanavyojua, lakini jambo la msingi si kuangalia ya ulimwengu huu kwani mwisho wa mambo yote dunia hii tunapita,” alisema.
Akizungumzia namna yeye na mkewe walivyowalea watoto hao, alisema hawajawahi kumshawishi mtoto yeyote awe padri isipokuwa waliwalea katika misingi ya kumjua Mungu na kulipenda kanisa.
“Sisi sio bora sana katika malezi ya watoto, la muhimu ni kumshukuru Mungu kwamba watoto wetu wamefika hapo walipofika, la msingi tuliwafundisha misingi ya kumjua Mungu na sisi kuishi maisha ambayo yalikuwa mfano kwao,” alisema.
Inyasi alisema watoto hao walisoma katika shule za seminari na baadaye kuamua kujiunga na masomo ya dini na kuwa mapadri.
Mama mzazi wa watoto hao, alisema watoto wake ambao wamepata upadrisho, ni Innocent Mkwe, Leandry Kimario, Proches Masomo na Ezekiel Mkwe.
Alisema licha ya jamii kuwachukulia tofauti, bado yeye anaamini suala hilo ni la kiimani zaidi na kwamba haoni fahari ya kuwa na wajukuu wengi ambao hawamjui Mungu.
“Hakuana fahari ya kuwa na wajukuu ambao hawamjui Mungu, nimefurahi sana suala hili na pia mimi nina wajukuu saba wananitosha,” alisema
Mbali na hilo, alisema yeye kama mama alimshawishi mtoto wa kwanza kuingia katika upadri na kumlea katika misingi ya dini, lakini wengine watatu waliamua kwa ridhaa yao wenyewe bila kulazimishwa na mtu.
Aidha alitoa wito kwa wazazi kuwalea watoto katika maadili mema, kwani malezi ya wazazi ndiyo yanayoamua tabia ya mtoto ya baadaye.
“Wazazi walee watoto katika maadili mema kwani malezi yao ndiyo yataamua mtoto aweje baadaye, ni muhimu kuwekeza katika malezi,” alisema.
Mmoja wa watoto hao, Padri Proches Masomo ambaye ni padri katika Kanisa la Useri Rombo, Jimbo Katoliki la Moshi, alisema alipadrishwa mwaka 2011 na kwamba yeye na ndugu zake walilelewa katika misingi ya kulipenda kanisa na kwamba jambo hilo ndiyo siri ya mafanikio yao.
“Wazazi walitulea katika misingi ya kulipenda kanisa na niliamua hili kwa hiari yangu mwenyewe na wazazi walifurahia hili bila pingamizi,” alisema Padri Masomo.
Alisema jambo hilo licha ya kufanyika baraka, limepokewa kwa namna mbili tofauti, wengine wakiwapongeza na wengine kuwabeza.
Padri Masomo alisema yeye na ndugu zake walipadrishwa kwa miaka tofauti. Wa kwanza ambaye ni Innocent alipadrishwa mwaka 2002, Padri Leadry 2007 na Padri Ezekiel mwaka huu.
Naye Padri Leadry Kimario, alisema alipata upadrisho mwaka 2007 na kwamba wito huo ulianza tangu akiwa mdogo, akipenda kujitoa katika shughuli mbalimbali za kanisa.
“Nilipenda kutumikia kanisa na nilikuwa na karama hiyo tangu nikiwa mdogo, pia wazazi wangu waliniandaa katika malezi ya dini kwani sikumbuki ni lini hatukuwahi kusali nyumbani pamoja na wazazi.
“Wazazi walijenga mazingira ya sisi kupenda kusali na walifanya hivyo sio ili sisi tuwe mapadri, ila walituongoza kiroho na sisi tulipenda kumtumikia Mungu na kanisa,” alisema.
Akizungumzia namna jamii inavyotafsiri, alisema wapo wanaoona ni baraka, lakini na wale wanaoona kwamba watakatisha uzao jambo ambalo hawalijali sana, zaidi wanatii sauti ya Mungu katika utume.