25.2 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

Simulizi ya wanaume waliopoteza wake, watoto Kagera

img-20160918-wa0066Na Editha Karlo, Kagera
SEPTEMBA 10 mwaka huu ni siku ambayo wakazi wa Mkoa wa Kagera hawataisahau kwani walipoteza wapendwa wao na wengine kujeruhiwa na kupoteza mali zao baada ya tetemeko kubwa la ardhi kutokea.

Mwandishi wa makala haya aliamua kufunga safari na kwenda maeneo mbalimbali ambayo tetemeko la ardhi lilileta athari.

Advela Respicius ni mama aliyepoteza binti yake katika tukio hilo la kusikitisha, anasema ni siku isiyofutika wala kusahaulika katika historia ya maisha yake.

“Ilikuwa siku ya Jumamosi (Septemba 10) saa 9 alasiri nikiwa nyumbani kwangu nilisikikia kitu kama mlio wa katapila la kutengeneza barabara nikatoka nje lakini sikuona kitu na sikujua kama ni tetemeko, baada ya dakika 10 nikiwa katika mshangao nilipigiwa simu na mtu ananiuliza unamjua Verdiana? nikajibu ndio akakata simu,”anaeleza mama huyo.

Mama huyo mkazi wa Kijiji cha Rutenge Kata ya Kamachumu wilayani Muleba, anasema hali hiyo ilimshtua kwa sababu Verdiana ambaye alikuwa ni mjamzito ni binti yake (kwa sasa marehemu).

“Mkwe wangu (mume wa marehemu) alinipigia simu akilia na kuniambia mama uje Bukoba,” anasema.

Anasema hakurudi ndani badala yake alikimbilia kwa ndugu yake aliyeko jirani na kumweleza kisha akampatia nauli na kuondoka kuelekea Bukoba.

“Nikiwa kwenye gari niliwasikia watu wanasema tetemeko limepita watu wamekufa Bukoba, nilipata wasiwasi sana,” anasema.

Anasema baada ya kufika stendi ya mabasi Bukoba, alielekea eneo la Kashenye alipokuwa akiishi marehemu binti yake.

“Baada ya kufika nakumbuka niliona nyumba alimokuwa akiishi yote imekuwa kifusi kitupu kutokana na kudondoka yote.

“Majirani zake, askari na watu wa msalaba mwekundu walikuwa wakifukua kifusi hicho. Nikamuuliza mkwe wangu maana alikuwa akilia mwanangu yuko wapi… alinionyesha kwa ishara ya mkono nikatambua kafukiwa na kifusi. Nilipoteza fahamu, nikazinduka baada ya nusu saa,” anaeleza mama huyo kwa uchungu.

Anasema baada ya kujitambua alikuta tayari mwili wa mwanawe umeshatolewa kwenye kifusi na kisha wakaelekea hospitali kwa ajili ya uchunguzi.

Anasema mwili huo ulifanyiwa upasuaji na kutolewa mtoto wa kiume ambaye alikuwa amekufa tayari.

“Kwa kweli sikuwa na la kufanya zaidi ya kumshukuru Mungu. Tulirudi nyumbani na kulala chini ya mti ulioko jirani na nyumba mimi na wajukuu zangu watatu walioachwa na marehemu,” anasema.

“Marehemu ameniachia watoto watatu ambao sijui nianzie wapi kuwatunza kwa sababu bado ni wadogo. Wa kwanza ana miaka saba, wa pili minne na wa tatu ana miaka miwili.

“Mimi sina kazi ni mama wa nyumbani, tunaomba wote tuliopatwa na majanga kama haya tutupiwe jicho la huruma,” anasema huku machozi yakimtoka.

Anasema kuna uvumi umeenea kuwa mtoto wake alilaliwa na jiwe jambo ambalo amekanusha na kusema si kweli bali alikufa baada ya kulaliwa na kifusi cha ukuta.

KISA CHA FELIX

Alex Felix ni mkazi wa Kata ya Hamgembe ambaye amepoteza mke na mtoto katika janga hilo.

Anasema siku ya tukio alikuwa dukani na mkewe na kwamba muda mfupi kabla tetemeko halijatokea mkewe alirudi nyumbani kuchukua chakula akiwa na mtoto wao mdogo.

“Nimepoteza mke wangu aitwaye Lucy Alex na mtoto wangu Alisia Alex (7). Nakumbuka siku ya tukio wote tulikuwa dukani na ilipofika saa 8:30 mchana mke wangu akaamua kwenda nyumbani ambapo ni karibu na dukani ili akachukue chakula. Mara nyingi huwa akienda anatumia nusu saa kurudi lakini kabla ya nusu saa likatokea tetemeko.

“Baada ya nusu saa kupita mke wangu mpendwa akawa hajarudi, niliamua kufunga duka na kumfuata nyumbani. Nilipofika nilikuta ukuta mmoja wa nyumba yangu umeangukia ndani na mwingine nje.

“Nikaingia ndani haraka haraka nikaanza kumuita mke wangu hakuitika, nikatazama huku na huku sikumuona wala mtoto wangu, nikaamua kufukua kifusi cha ukuta wakati nikiendelea nikaona kipande cha kanga ya mke wangu.

“Nikaendelea kufukua ule udongo kama nafukua viazi shambani kumbe nikawa namfukua mke wangu na mtoto wangu mpendwa,” anaeleza huku akibubujikwa na machozi.

Anasema wakati akiendelea kufukua alipita jirani yake mmoja ambaye aliona hali hiyo kisha akaamua kukimbia na kuwaita majirani mbapo walifika na kumkuta akiendelea na shughuli hiyo… walimsaidia na kupata miili ya marehemu.

“Jumamosi ya Septemba 10 iliyoondoka na wapendwa wangu sitoisahau katika maisha yangu. Eee Mungu wape heri na mwanga wa milele waangazie wapendwa wangu, mke wangu umeondoka nakupenda watoto wako wanakutafuta Airine na Alistides wamekosa busara zako. kwaheri mke wangu tutaonana huko mbinguni,” anaongea kwa simanzi huku akitokwa na machozi yaliyoambatana na kwiki.

KISA CHA RWIZA

Naye Benson Rwiza mkazi wa Hamugembe amempoteza mke wake akiwa na mimba ya miezi tisa kutokana na tetemeko la ardhi.

“Naumia mno, nimepoteza mke wangu akiwa mjamzito na ndo alikuwa mtoto wangu wa kwanza, kwa kweli sitasahau kabisa hali hii,” anasema Rwiza kwa uchungu.

Rwiza anasema siku ya tukio mke wake alikuwa nyumbani amelala kwa  sababu alikuwa hajisikii vizuri.

“Mke wangu alikuwa amelala ndani anajisikia vibaya, nikatoka kufuata dawa dukani huku nyuma tetemeko likatokea akashindwa kukimbia nyumba ikamshukia na kufariki, tetemeko limeniulia mke na mtoto wangu,”anasema kwa uchungu.

TUKIO LA MWAKA 1968

Naye Anastazia Laulian (79) ni mkazi wa Kata ya Maruku Bukoba Vijijini, ambaye pia amejeruhiwa sehemu ya mguu wake baada ya kuangukiwa na mlango pamoja na matofali.

Kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera, anasema tukio la tetemeko liliwahi kutokea mwaka 1968 ambapo yeye alikuwa akimnyonyesha mwanawe wa tatu aitwaye Aulelia.

“Nilikuwa mdogo wakati huo, zamani tulikuwa tukiolewa tukiwa na umri mdogo, nakumbuka siku hiyo nilikuwa ndani namnyonyesha mwanangu.

“Ghafla nikasikia mtetemo kwenye nyumba nikahisi kama vile kuna jini kaingia ndani ya nyumba, nikakimbilia uvunguni mwa kitanda na mtoto wangu, lakini ilichukua muda mfupi kama dakika tatu tu ila halikuwa kubwa kama hili la sasa na wala nyumba hazikubomoka,” anasema.

Anasema baadaye alielezwa na mama mkwe wake kuwa ni tetemeko.

Bibi huyo anasema pia aliwahi kuambiwa na baba yake kuwa hata mwaka 1947 tetemeko liliwahi kutokea lakini lilikuwa dogo na wala halikuleta madhara.

Pia anafananisha tetemeko la sasa na matukio mbalimbali yaliyowahi kutokea mkoani humo na kuweka historia kama vile vita ya Kagera, ugonjwa wa Ukimwi, ajali ya meli ya MV Bukoba, utekaji wa kutumia silaha uliokuwa ukifanyika katika mapori mbalimbali, mvua ya Elnino na njaa aina ya Ibambula mabati iliyotokea mwaka 1945.

“Matukio kama hayo yaligharimu maisha ya watu wetu tukapoteza nguvu kazi ya Taifa na kutuingiza katika lindi la umaskini, sasa leo nyumba zetu zimeanguka hatuna pa kulala tunahangaika na wengine hatuna watoto wa kutusaidia,” anasema bibi huyo.

Anasema majanga kama hayo wamekuwa wakisikia katika nchi za mbali lakini leo yapo Bukoba.

“Baadhi ya watu wa zamani walikuwa wakisema ukiona limetokea tukio la kupatwa kwa mwezi au jua katika meneo yako ujue kuwa ni majanga makubwa yanakuja kwa hiyo hata hili tetemeko linaweza kuja kwa sababu hiyo.

“Tunaiomba Serikali ituangalie kwa jicho la huruma kama walivyotuokoa na kutuleta hospitali, tujengewe nyumba maana nawaza nikitoka hapa nitaenda kulala nje,” anasema.

Stanslaus Francis ni mmoja wa wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya mkoa huo, anasema siku ya tukio alitoka Bukoba Vijijini na kuja Bukoba Mjini kumtembelea ndugu yake ambaye alikuwa na sherehe ya Kipaimara cha mtoto wake.

Anasema wakati sherehe zikiendelea walisikia tetemeko kubwa na kudhani ni itilafu ya umeme.

“Hali hiyo iliendelea kwa dakika nne hivi tukaanza kukimbia kuelekea nje, lakini mimi kabla ya kutoka nilikutana na ukuta ukanipiga kiuno na miguu nikaanguka chini na kuzimia. Baada ya tetemeko kutulia walikuja raia wema kwa kusaidiana na vikosi vya uokoaji na kunibeba kisha kunileta hapa hospitali.

“Tunajua Serikali inao wataalamu ambao wamekuwa wakipima na kuona mambo haya mapema, tunaomba wakati mwingine watupatie elimu mapema na si kusubiri majanga yatokee na kusababisha madhara makubwa ndipo waanze kuhangaika,” anasema Francis.
HOFU YA TETEMEKO LINGINE

Joyce Ndukeke ni mmoja wa waathirika hao anasema tangu wamepatwa na janga hilo hawajapata msaada wowote na kuwa wanachokifanya ni kujikusanya pamoja na kulala nje.

Ndukeke ambaye ana watoto wanne anasema wakati tetemeko hilo likitokea alikuwapo nyumbani pamoja na watoto wake.
“Nyumba zetu zimeanguka hatujapata msaada, hatuna pa kulala tunalala nje na watoto, lakini sasa tuna hofu zaidi maana wataalamu wanasema matetemeko yataendelea kujirudia hata mwezi mzima, tunaomba tusaidiwe kujengewa mahema maana huu ni msimu wa mvua inaweza kunyesha wakati wowote,” anasema Ndukeke.

 

WAKALA WA JIOLOJIA

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia nchini, Profesa Abdkarimu Mruma, anawataka wakazi wa Kagera kuchukua tahadhari muda wote na kuzingatia elimu inayotolewa ya namna ya kukabiliana na matetemeko ya ardhi, ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

Kuhusu tetemeko lililotokea Septemba 10 mwaka huu, Mtendaji huyo anasema ni muhimu wananchi kuzingatia elimu wanayopewa kwa sababu matetemeko yanaweza kuendelea kutokea.

Mruma anasema duniani kote hakuna kipimo kinachoweza kutambua viashiria vya matetemeko ya miamba na kuwa hatua zilizopo ni kuangalia vitu vinavyoweza kupunguza athari pindi tetemeko linapotokea.

“Wananchi wanapaswa kuzingatia elimu wanayopewa, mfano linapotokea tetemeko wanaweza kusimama kwenye kingo za nyumba maana ukuta hauwezi kuanguka na kuwafunika, utaangukia nje au ndani” anasema.

Anasema wakati wa tetemeko wanaweza kuingia chini ya meza au kitanda ili ukuta ukianguka vitu hivyo vipunguze kasi ambayo ingeweza kuwasababishia majeraha makubwa.

“Tetemeko likitokea wananchi wazime umeme, lakini pia wasitumie vyombo vya moto ili kupunguza athari,” anasema Mruma.

Anasema tangu nchi ipate Uhuru hilo ni tetemeko la tisa kutokea Kagera, ingawa mengine yalikuwa madogo na kuwa kitovu cha matetemeko hayo ni Minziro wilayani Misenyi.

“Kagera likitokea tetemeko athari zinakuwa kubwa kuliko maeneo mengine kutokana na kuwepo kwa miamba laini, mfano tetemeko lilitokea Kagera na Mwanza, la Mwanza linakuwa na athari  ndogo maana kuna miamba migumu.

 

MKUU WA MKOA

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu, Salum Kijuu, anasema tetemeko hilo lilikuwa na ukubwa wa kipimo cha alama 5.7 (richter) na watu 17 walipoteza maisha kutokana na kuangukiwa na kuta za nyumba, waliojeruhiwa ni 253, nyumba zilizoanguka ni 840 huku nyumba 1,264 zikipata nyufa kubwa.
Anasema wameunda kamati ndogo itakayosimamia misaada yote na kuhakikisha inawafikia walengwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,784FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles