27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

SIMULIZI YA UTAWALA WA MOI KUPOTEZA MADARAKA (3)

NAIROBI, KENYA


KATIKA mfululizo wa makala hii, Mkuu wa zamani wa Ktengo cha Habari cha Rais Daniel arap Moi, Lee Njiru pamoja na mambo mengine anasimulia kipindi cha saa 72 za ‘mateso’ wakati kiongozi huyo akisubiri kukabidhi madaraka kwa upinzani baada ya chaguo lake kushindwa vibaya.

Jana tuliona wakati Moi akipanda helikopta kuondoka Ikulu, huku Mkuu wa Utumishi wa Umma, Sally Kosgei akimwangalia kwa huzuni, hisia za uchungu zikimteka, akashindwa kujizuia kumwaga machozi kama mtoto baada ya kuona Rais mstaafu huyo ‘akilipwa mateke’ ndani ya muda mfupi tu baada ya kuachia madaraka na watu ambao wengi wao aliwatengeneza.

Ikumbukwe siku hiyo ya Desemba 30, 2002, ni Kosgei huyu aliyejikuta akiondoka katika sherehe za kuapishwa kwa Rais Mwai Kibaki bila viatu baada ya Moi kufanyiwa vurugu. Sasa endelea…

Mbali ya Moi na walinzi wake, wengine waliopanda helikopta hiyo walikuwa Njiru na John Lokorio, aliyekuwa katibu binafsi wa rais mstaafu.

Hali ndani ya helikopta katika safari hiyo ya dakika 40 ilitawaliwa na ukimya na huzuni, Njiru anakumbushia.

“Wakati unapoondoka mahali ambapo umepahesabu ni nyumbani kwa robo karne, si kitu rahisi kwa kweli. Lakini nakumbuka Mzee alikuwa mtulivu wakati wote wa safari, ingawa hakuzungumza wakati wote huo,” alisema.

Familia ya Moi ilikuwa imejipanga kumpokea nyumbani Kabarak.

Baada ya chai, kulikuwa na sherehe ndogo ya kuondoka kwake Ikulu.

 

FUNZO

“Kipindi kirefu cha utumishi wangu wa umma na cha maisha ya ustaafu, kilikuja kutoa funzo kuhusu uhusiano na maofisa waandamizi waliomzunguka Moi,” anasema Njiru.

Bila madaraka, marafiki haraka haraka walimtelekeza rais wa zamani, wengi wao hao walienda kusaka upatanisho na kutafuta nafasi au mahali pa kuweka ubavu katika Serikali mpya ya Kibaki.

 

KUJIKOMBA TENA

Akihutubia umati Ikulu mwaka jana, Naibu Rais William Ruto alikumbushia namna Moi alivyotelekezwa kama takataka ndani ya muda mfupi baada ya kuonekana profesa huyo wa siasa hakuwa na mbinu zaidi za kuiokoa Kanu kutoka ‘kaburini’.

“Tulikuwa tukiangalia televisheni katika chumba hiki (cha Ikulu) wakati Moi alipoingia na kuniambia nikamwite Uhuru na kumwagiza aandike hotuba ya kukubali kushindwa.

“Awali kabla ya hilo, tulikuwa watu zaidi ya 40 chumbani hapo tukisubiri hatua inayofuata kutoka kwa bwana mkubwa, lakini wakati tulipokuwa tukiandaa hotuba ile, tulijikuta tumebakia watatu tu.

“Kundi hilo ni la watu waliokuwa wakisubiri miujiza kutoka kwa Moi wakiwa na dhamira ya kuendelea kuula, waliondoka baada ya kubaini hakuna kitu kama hicho,” alisema Ruto.

Njiru alisema kuwa baadhi ya waliomwacha Moi baada ya kuondoka Ikulu, walianza kujikomba tena mwishoni mwa 2003 wakati walipobaini profesa huyo wa siasa bado hajaisha kwa nguvu na ushawishi.

 

USALITI

“Kwa kawaida huwa nawauliza baadhi ya watu hawa wanapokuja kunitembelea na kunisifu namna nilivyoweza kubakia na Mzee kwa kipindi chote hicho kigumu, ‘Wapi mlikuwa Desemba 30, 2002?’ Ni neno ninalowauliza, wanabakia kubabaika na kuondoka kwa aibu,” anasema Njiru.

Kati ya wasaliti wote, hakuna wanaoumiza zaidi kuliko msaidizi wa karibu wa Moi, ambaye Njiru hakuwa tayari kumtaja, lakini ambaye amekuwa akifanya kazi upande wa upinzani kwa muda mrefu.

“Et Tu, Brute” (ikimaanisha ‘Hata wewe, Brutus’),” alisema akikariri igizo la William Njiru Shakespeare- Julius Caesar, ambapo mtawala wa zamani mashuhuri wa Dola la Roma, Julius Caesar anazungumza na rafiki na msiri wake Marcus Brutus, ambaye alishiriki katika mauaji yake.

 

FAGIA FAGIA

Katika siku za awali za utawala wa Kibaki, kulikuwa na hofu ya kushtakiwa kwa kundi kubwa la watu mashuhuri wa utawala wa Moi, ikiwamo tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu na uhalifu wa kiuchumi wa mstaafu huyo.

Hofu hizi kwa kiasi kikubwa hazikuwa na msingi, lakini fagia fagia ya wanaohesabiwa washirika wa utawala uliopita, ilianza kuwaandama mmoja baada ya mwingine na kuzua hofu na sintofahamu katika kada ya utumishi wa umma.

Maofisa waandamizi wa jeshi walistaafu katika makabidhiano ya haraka ya madaraka. Kuhesabiwa kuwa karibu na utawala wa zamani, kulikuwa tishio kwa ajira ya mhusika na hivyo wengi walilazimika kujitenga nao.

“Watawala wa zamani wa jimbo huko Nakuru, ambao walikuwa karibu nami wakati huo, walinionya nisiwapigie tena simu, vinginenvyo nitapeperusha kitumbua chao.

“Mmoja wapo alisitisha uhusiano nami, huku mwingine akiniambia nikimtafuta niwe namwandikia na kumkabidhi karatasi kwa mkono chochote atakachotaka au kuhitaji. Hilo ndilo pekee, ambalo angeweza kufanya katika mazingira yale,” anasema Njiru.

Njiru anasema uzoefu wa ustaafu kwa wengi kwa sehemu kubwa ya watu wa timu ya Moi ilikuwa wenye kuvunja moyo.

Wakati mwandishi alipomuuliza Njiru kuhusu uzoefu wake katika maisha hayo, alibakia kimya kwa muda kana kwamba swali hilo limemtoa pumzi.

Alipapasa macho haraka wakati akipangilia maneno.

 

KISAIKOLOJIA

“Kustaafu ni suala la kimwili na kisaikolojia. Uhamisho kutoka kazi uliyokuwa ukiifanya kwa muda mrefu kunadhalilisha na kuponda ponda moyo. Hisia ya kukata tamaa inakushinda, huwezi kupigana nayo kwa ngumi au kuiua kwa bunduki.

“Hisia ya kukataliwa na kukosa matumaini inaondoa kila jema la mwanaume wakati wa kuikabili,” anasema.

“Vipi kuhusu Moi?” Njiru akaulizwa.

Anasema kwa sehemu kubwa ya miaka 50 ya kujishughulisha kwake katika siasa, Moi alijulikana kwa kupokea makundi makubwa ya ujumbe Ikulu au nyumbani kwake Nairobi na Nakuru.

Vipi kuhusu namna alivyochukulia kustaafu kwake, kupoteza madaraka na changamoto zinazotokana nazo?

 

MTU WA CHUMA

Njiru anajibu swali hilo akisema: “Kustaafu huathiri kila mmoja kwa namna tofauti. Lakini kilichomsaidia Mzee ni kwamba yeye yu mtu wa chuma. Ni mtu aliyejiwekea msingi imara. Alikabili hali vizuri kwa utulivu.”

Njiru, ambaye amekuwa akiishi bila mke tangu mwaa 2005, anasema mchakato mzima wa kupanda na kushuka (madarakani) ulimfunza masomo muhimu ya maisha.

“Jihadharini na nguvu haribifu ya bahati. Bahati haitabiriki. Inaweza kufuta ubinafsi na unyenyekevu wako. Elimisha watoto wako unapoweza. Mtendee vyema mkeo,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles