22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

SIMULIZI YA PADRI ALIYEFUNGA NDOA DAR

Na ARODIA PETER-DAR ES SALAAM


JINA la Padri Privatus Karugendo si geni kwa Watanzania  wengi.  Jina hili lilianza kuchomoza mwaka 2002, baada ya vyombo mbalimbali vya habari kumnukuu akitoa mada kwenye mkutano wa Ukimwi akiunga mkono matumizi ya kondomu ili kujikinga na ugonjwa huo.

Mjadala mkali uliibuka,huku baadhi ya watu wakiegemea zaidi sheria na misingi ya Kanisa Katoliki kwamba kiongozi huyo wa kiroho amekengeuka kwa kupigia debe matumizi ya kondomu.

Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu nyumbani kwake, Tabata Chang’ombe, Dar es Salaam jana, Padri Karugendo ambaye alifunga ndoa na mkewe Rose Birusya wiki iliyopita katika Kanisa la St Peters, Dar es Salaam, amewahi kuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Buziku Jimbo Katoliki la Rulenge hakutetereka, badala yake aliendelea kushikilia msimamo wake  kwa hoja  kuendelea kunyamazia matumizi ya kondomu ni sawa na kuruhusu vifo vinavyotokana na Ukimwi.

“Msimamo wangu  ulitokana na uzoefu wa miaka 20 nikiwa padri, najua jinsi watu wasivyokuwa waaminifu katika suala zima la mahusiano” anasema Padri Karugendo na kuongeza.

“Kwa hiyo kujificha katika kivuli cha matakwa ya dini, huku jamii ikiteketea kwangu niliona ni dhambi kubwa, niliikataa,” anasema.

Kutokana na msimamo huo, mada yake hiyo huenda ilikuwa ndio mwisho wa mchunga kondoo huyo wa Mungu kukanyaga madhabahuni akihudumu kama Padri.

Mada hiyo, ilisababisha mwendelezo wa adhabu kwa Padri Karugendo kabla ya hajamaliza nyingine ya kifungo cha mwaka mmoja akiwa nje ya kanisa.

Padri Karugendo, aliamriwa kuondoka kanisani na kwenda kuishi nyumbani  kwa wazazi wake, Kijiji cha Ibwera Tarafa ya Katerero Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera kwa kosa la kukaa nje ya kituo cha kazi kwa muda mrefu.

Akisimulia historia ya maisha yake, Padri Karugendo anasema kabla ya adhabu ya kurudishwa kwa wazazi wake, hakuwa na uhusiano mzuri na bosi wake ambaye ni Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Rulenge, Severin Niwemugizi.

Anasema kwa kuwa wazazi wake walikwisha tangulia mbele ya haki, hakwenda Ibwera kama alivyoamriwa badala yake, alipata msaada wa kupangishiwa nyumba ya kuishi na aliyekuwa Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli  Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza ambaye sasa ni Askofu wa dayosisi hiyo.

Mchungaji Bagonza alimpangishia nyumba kwa muda wa miaka miwili.

“ Kimsingi kosa nililotuhumiwa nalo la kukaa nje ya kituo cha kazi lilitokana na ujio wa wageni marafiki zangu kutoka nchini Holland.

“Mazingira ya Kanisa la Buziku hayakuwa rafiki, hakukuwa na vyoo na huduma nyingine mbalimbali kwa wageni, niliomba ruhusa kwa bosi wangu kuwa wageni hao nitawapeleka Bukoba na baadaye niliwasindikiza hadi Dar es Salaam wakarudi kwao.

Padri Karugendo, anasema kitendo hicho hakikumfurahisha bosi wake, hivyo alimpa adhabu hiyo ambayo baadaye ilikuja kuwa mojawapo kati ya mashtaka saba aliyoshtakiwa nayo kwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani wakati huo, Papa Benedict wa XVI.

Anasema anakumbuka kabla ya adhabu hiyo, mkuu wake wa kazi alikwisha mtuhumu kwa nyakati tofauti kwa makosa mbalimbali ambayo hakuwahi kuhusika nayo.

Anasema aliwahi kumtuhumu  kujihusisha kimapenzi na msichana aitwaye Rose ambaye ndiye amekuwa mkewe wa ndoa.

 “Nilituhumiwa eti najihusisha na msichana mmoja kimapenzi,ukweli ni kwamba huyo binti (Rose) na wenzake, walikuwa wanasomeshwa na Jumuiya ya Mkamilishano iliyokuwa chini ya kanisa hilo,nilikuwa msimamizi wake,”anasema wakati huo hakuwa na mawazo yoyote na msichana huyo zaidi ya kumsaidia apate elimu.

Anasema Jumuiya hiyo, ilianzishwa na aliyekuwa Askofu wa Jimbo hilo, Christopher Mwoleka kwa lengo la kuwaweka pamoja waumini, mapadri, masista na watumishi wengine wa kanisa katika jimbo hilo.

Chini ya Jumuiya ya Mkamilishano, watu walifundishwa kuishi na kufanya kazi kwa umoja bila kujali cheo, nafasi ya mtu katika jamii, jambo ambalo lilizaa matunda ambapo watoto kadhaa wa familia zisizo jiweza walisomeshwa bure hadi nchini Uingereza ambapo baadhi yao wanaishi huko hadi leo.

Usikose mwendelezo wa simulizi hii toleo la gazeti hili kesho.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,215FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles