31.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

SIMULIZI YA MWANAFUNZI MWENYE UONI HAFIFU ANAYEWASHANGAZA WALIMU

Na MAREGESI PAUL – ALIYEKUWA SONGEA


WATU wenye ulemavu wa ngozi, macho na viungo, mara nyingi wamekuwa wakichukuliwa kama watu wasiokuwa na msaada katika jamii.

Kutokana na hali hiyo, wengi wao wamekuwa wakiishi maisha ya shida na mara kadhaa wanakosa elimu ya kuwasaidia kuendesha maisha yao kwa kuwa

baadhi ya watu hawawaamini.

Wakati hali ikiwa hivyo, Serikali imekuwa ikijitahidi

kuwasaidia watu wenye ulemavu ili nao wajione wako sawa na jamii nyingine isiyokuwa na ulemavu.

Pamoja na jitihada hizo, watu wenye ulemavu wamekuwa wakisoma kwa shida na mara

kadhaa kushindwa kupata mafanikio kitaaluma kutokana na kukosa msaada kutoka serikalini na katika jamii inayowazunguka.

Pamoja na uwapo wa mazingira magumu ya usomaji na ujifunzaji shuleni, mwanafunzi mwenye uoni hafifu, Geofrey Ndungulu (24), mkazi wa Kijiji

cha Lusonga, Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma, anaeleza jinsi alivyosoma kwa shida na sasa anatarajia kujiunga na moja ya vyuo vikuu nchini, baada ya kuwa amekamilisha maombi ya vyuo hivyo.

Katika mahojiano na MTANZANIA aliyoyafanya hivi karibuni, Ndugulu ambaye kwa sasa yuko katika mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT),

Kambi ya Ruvu, Mkoa wa Pwani, baada ya kuhitimu kidato cha sita mwaka huu, anasema amefika hapo alipo baada ya kusaidiwa na mfanyabiashara mmoja aliyejitolea kumsomesha.

“Historia yangu kimaisha si nzuri kwa sababu nimezaliwa katika familia masikini, wilayani Mbinga ambayo haikuwa na uwezo kabisa wa kunisomesha.

“Nakumbuka kabla ya kuanza shule, siku moja mwaka 2007, nilikuwa barabarani nikitembea na watoto wenzangu nikiendesha taili ya baiskeli, ndipo nikaonana na mfanyabiashara wa madini anaitwa Ferdinand Masawe.

“Huyo jamaa aliniuliza kwanini siendi shule wakati watoto wengine wenye umri kama mimi wako shuleni.

“Nilimwambia natamani kusoma ila sisomi kwa

sababu sioni vizuri na familia yangu haiwezi kunipeleka hospitalini nikatibiwe, kisha niende shuleni na kibaya zaidi baba yangu ameshafariki tangu

mwaka 2003 na sasa naishi na mama yangu mzazi ambaye naye ni maskini.

“Yule jamaa aliguswa na maelezo yangu, hivyo akafanya mpango akaja kuonana na mama yangu mzazi na kukubaliana namna ya kunitibu ili

nianze kusoma.

“Baada ya makubaliano hayo, siku moja Masawe alinichukua mimi na mama yangu na kunipeleka Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma ambako nilipatiwa matibabu ya macho kwa gharama zake kadiri

ilivyowezekana na hapo nikaanza kuona kidogo kidogo kwa sababu mwanzoni nilikuwa naona kwa kubahatisha.

“Baadaye, Masawe alinifanyia mpango nikaanza darasa la kwanza katika shule yenye watoto wenye mahitaji maalumu iitwayo Luhira Shule ya Msingi, iliyoko Manispaa ya Songea, Mkoa wa Ruvuma ambako nilianza darasa la kwanza mwaka 2007.

“Kwa bahati nzuri, sikusoma kwa kufuata madarasa kama inavyotakiwa kwa sababu nilikuwa na uwezo mzuri darasani, hivyo nilirushwa madarasa na hivyo kunifanya elimu ya msingi niisome kwa miaka mitano

badala ya miaka saba.

“Mwaka 2011, nilihitimu elimu ya msingi na kufaulu kwa daraja la kwanza na kuanza masomo ya sekondari mwaka 2012 katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Songea (Songea Boys) ambayo nayo ina madarasa ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

 

“Wakati naanza masomo, wenzangu walikuwa wakiniambia maneno ya kunikatisha tamaa, kwamba shule hiyo haijawahi kufaulisha mwanafunzi

mwenye uoni hafifu au asiyeona kutokana na mazingira ya usomaji yalivyo magumu.

“Nikawaambia, nitakuwa wa kwanza kufaulu na nilipofika ‘form two’ (kidato cha pili) na kufanya mtihani wa Taifa mwaka 2013, nilikuwa wa kwanza shuleni, pia nilikuwa wa kwanza kwa shule za nyanda za juu kusini baada ya kupata division one (daraja la kwanza) ya point saba,” anasema Ndungulu.

Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo, matokeo hayo yalimfurahisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye wakati huo alikuwa Naibu Waziri wa TAMISEMI baada ya kutembelea

shuleni hapo.

Kutokana na ufaulu huo, anasema Waziri Mkuu Majaliwa alimpa zawadi ya Sh laki moja na baadhi ya

viongozi aliokuwa nao kwenye msafara, nao walimpa zawadi za fedha pia.

“Pamoja na matatizo ya macho niliyonayo nilipohitimu kidato cha nne mwaka 2015, nilipata ‘division two’ (daraja la pili) ya poit 18 na nikachaguliwa kujiunga na

Shule ya Sekondari Mpwapwa iliyoko Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kidato cha tano na sita.

“Pamoja na kupata matokeo hayo kidato cha nne, hadi leo naamini wasahihishaji walinikata maksi kwa sababu mwenyewe najijua na najua nilivyokuwa nimefanya mtihani.

“Nilipokuwa Mpwapwa Sekondari, katika darasa letu la HGK lilikuwa na wanafunzi 47, lakini wenye mahitaji maalumu tulikuwa wawili ila mwenzagu alikuwa haoni kabisa tofauti na mimi ninayeona kwa kuungaunga.

“Nilipokuwa kidato cha tano, tulipofanya mtihani wa

kufunga muhula wa kwanza, nilishika nafasi ya sita darasani, jambo ambalo liliniumiza kichwa.

“Kwa hiyo, nilijitahidi na tulipofanya mtihani wa kufunga mwaka, nilikuwa wa kwanza na mtihani wa muhula wa kwanza ‘form six’ (kidato cha sita), nikawa wa pili.

“Kwa yale matokeo ya form six yaliyotoka hivi karibuni, nimekuwa wa kwanza shuleni kwa kupata ‘division one, pointi saba. Kwa bahati nzuri, tayari nimechaguliwa kuanza masomo ya Shahada ya kwanza ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) japokuwa hadi sasa sijajua kama nitapata mkopo kwa asilimia 100.

“Kwa hiyo, ninachotaka kusema hapa ni kwamba, naiomba Serikali inisaidie mkopo ili nitimize ndoto zangu kwa sababu nisipopata huo mkopo, uwezekano wa kusoma ni mdogo kwani mfadhiri wangu ambaye ni Masawe, kwa sasa ana majukumu mengi na hawezi kunisomesha kwa asilimia 100 kama alivyokuwa akifanya huko nyuma,” anasema Ndunguru.

Wakati huo huo, Ndungulu anasema wakati akiwa kidato cha nne Shule ya Sekondari ya Wavulana Songea, yeye na mwenzake Yusuf Mwenda, walichaguliwa kwenda kushiriki mashindano ya Vijana Wanasayansi wa Tanzania (YST) yaliyofanyika Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.

“Nakumbuka katika mashindano hayo, shule 120 zilishiriki na tulikuwa wanafunzi 240 ambapo washiriki tulikuwa tukihojiwa na majaji watatu Wazungu kupitia maandiko yetu tuliyokuwa tumeandika yakihusu ni kwanini wanafunzi wenye upofu, hawasomi masomo ya sayansi.

“Katika mashindano hayo, andiko letu lilikuwa la tano kati ya washindi 10 waliokuwa wamechaguliwa. Baadaye nikapata fursa ya kukutana na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, ambaye alikutana na washindi nikiwamo mimi.

 

“Kutokana na ushindi huo, nilipewa zawadi ya shilingi 350,000, medali pamoja na cheti cha kutambua ushindi wangu,” anasema Ndungulu.

 

 

MAZINGIRA YA USOMAJI

Akizungumzia eneo hilo, anasema wenye ulemavu kama yeye wana wakati mgumu wa kusoma kwa kuwa mazingira yao ni magumu yakihusisha uhaba wa vitabu, mashine za nukta nundu, miwani ya kusomea, lenzi na uhaba wa walimu wenye elimu maalum.

“Kwa mfano, mimi naandika kwa kutumia mashine za nukta nundu, lakini jambo la kushangaza ni kwamba, hizo mashine nilipokuwa Songea Boys,

tulikuwa nazo saba wakati wenye mahitaji ni wanafunzi 50.

“Hata walimu wenye elimu maalumu pia hawatoshi na waliokuwa wakitufundisha, baadhi hawakuwa na mafunzo ya elimu maalumu kwani mwalimu anaweza kusema mnaona hapa, wakati akijua wengine hatuoni.

“Hata pale Mpwapwa Sekondari, tulikuwa na walimu wawili wenye mafunzo ya elimu maalum na alipostaafu mmoja, akabaki mmoja.

 

“Sasa fikiria, katika mazigira hayo utasomaje, kwanza vitabu huna, walimu huna na mazingira yote ya kusoma ni tatizo pia na hata miundombinu ya majengo si rafiki.

“Kwa hiyo, naiomba Serikali iliangile hili kundi maalumu kwa sababu na sisi ni binadamu kama wengine na tunahitaji kupewa heshima na kuajiriwa kama wengine,” anaeleza Ndungulu.

 

Wiki ijayo tutaendelea na simulizi hii ambapo Masawe atasimulia jinsi alivyokutana na Ndungulu na ni kwanini aliamua kujitolea kumsomesha.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles