26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Simulizi ya mwanafunzi aliyezuiwa na baba yake kufanya mtihani darasa la saba

Mwandishi wa makala haya (kulia), akifanya mahojiano na Yusria Msumi. Kushoto ni mama yake mzazi.
Mwandishi wa makala haya (kulia), akifanya mahojiano na Yusria Msumi. Kushoto ni mama yake mzazi.

Na FARAJA MASINDE – ALIYEKUWA PWANI

LICHA ya ukweli kwamba elimu ni haki ya msingi ya kila mtoto, lakini wapo ambao wamekuwa wakikosa haki hiyo kutokana na changamoto lukuki zikiwamo za wazazi kushindwa kutambua thamani ya elimu, mazingira magumu pamoja na umasikini uliokithiri.

Bado kumekuwapo na sababu zingine ambazo ama kwa kujua au kutokujua, baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwakosesha watoto wao haki ya kupata elimu kwa makusudi.

Mkoa kama Shinyanga ni moja ya mikoa ambayo baadhi ya watoto wa kike wamekuwa wanakosa haki yao ya kupata elimu kutokana na baadhi ya wazazi kuwaozesha wakiwa masomoni.

Wazazi wamekuwa wakiwakatisha masomo wanafunzi hasa walio kwenye ngazi ya msingi kwa madai kuwa kusoma hakuna faida yeyote na badala yake wakubali kuolewa ili familia zao ziweze kunufaika na mali ikiwamo ng’ombe na vitu vingine licha ya ukweli kuwa vitu hivyo vyote haviwezi kushinda thamani ya elimu.

Hata hivyo ukatili unaofanywa na wazazi kwa watoto wao kwa siku za karibuni umeenda mbali zaidi hadi kufikia hatua ya kuwazuia kutofanya mitihani ya kuhitimu masomo yao.

Madhila hayo ya kuzuiwa kufanya mitihani ndiyo yaliyomkuta Yusria Msumi (13) ambaye ni miongoni mwa wahitimu 77 wa Shule ya Msingi Churwi iliyoko Kata ya Tumbwi, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Safari yake ya kielimu imekuwa na historia inayohuzunisha.

Yusria mwenye ndoto ya kufika chuo kikuu na kuwa mwalimu wa somo la Hesabu kutokana na kulimudu vyema anasema, licha ya kufanikiwa kuhitimu elimu ya msingi lakini safari yake ya miaka saba ilibeba changamoto lukuki kutokana na baba yake (jina linahifadhiwa) kutokuwa na nia njema na masomo yake.

Huku akiongea kwa kujiamini, Yusria anasema siku ya kwanza ya mitihani hiyo, baba yake alimuamuru kuvua nguo za shule na kumtaka kwenda kujificha kwenye shule ya chekechea anayoimiliki.

“Baba yangu amekuwa akinisisitiza kila siku kuwa ni lazima nirudie darasa la saba kwani hayuko tayari kuona nikiingia kidato cha kwanza kwa wakati huu kwa madai kuwa sijafikia kiwango anachokihitaji kitaaluma.

“Hivyo siku ambayo tulikuwa tunaanza mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi, asubuhi na mapema nikiwa nimejiandaa tayari kwenda shule, baba aliniambia hakuna kwenda shule hivyo nibadilishe nguo.

“Nilijaribu kumuuliza kwanini lakini baba alirejea tena kauli yake hiyo ya kunitaka nibadili nguo za shule na kuvaa za nyumbani kisha nitangulie shuleni kwake. Mimi nilifanya hivyo na kuelekea shuleni kwake huku nikiwa nimeambatana naye,”anasema Yusria.

Anabainisha kuwa wakati wenzake wakiendelea kujiandaa na mtihani, baba yake alikuwa akiendelea kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha anahujumu elimu yake.

“Tulipofika shuleni kwa baba aliniambia tuelekee Hospitali ya Mbagala Maji Matitu, mara baada ya kufika hapo mimi na baba tuliingia kumwona daktari na baba alimwambia kuwa alikuwa akihitaji cheti cha kuonyesha kwamba naumwa uti wa mgongo.

“Baada ya baba kuwasilisha maombi hayo, daktari alimuuliza juu ya lengo lake la kufanya hivyo na alimjibu kuwa alikuwa hayuko tayari kuona nikifanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi.

“Daktari alimtaka baba kufika shuleni nilikokuwa nasoma kwa ajili ya kutoa taarifa kwa Mwalimu Mkuu kwa kuhofia kuingia matatani,”anasema.

Anaendelea kubainisha kuwa kufuatia majibu hayo, baba yake aliondoka na kwenda shuleni kutoa taarifa ili kurahisisha mpango wake wa kupata cheti cha ugonjwa wa uti wa mgongo.

Hata hivyo mambo yalibadilika baada ya walimu kutokuwa tayari kuamini kilichokuwa kikielezwa na baba huyo kama ni cha kweli.

“Baada ya baba kufika shuleni, walimu walimuuliza kuwa nipo wapi ndipo akawaambia nilishindwa kufika shule kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya uti wa mgongo. Lakini baada ya kauli hiyo mwalimu alisema ugonjwa huo ulikuwa ni wa ghafla mno na hivyo akahitaji kuwasiliana na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mkuranga (OCD), ili niletewe mtihani hospitali.

“Walimu walimwambia baba kuwa walikuwa wakinitegemea mimi kwa ajili ya kuitangaza shule kiwilaya na kimkoa na hata kitaifa,” anasema Yusria huku akionekana mwenye huzuni kubwa.

Anasema wakati baba yake akiwa shuleni hapo, polisi pamoja na baadhi ya maofisa wa maendeleo wa kata walikwenda kwenye hospitali iliyotajwa na kumkuta Yusria akiwa amevalia nguo za nyumbani.

Hivyo wakamchukua na kurejea naye shule na kuvuruga mpango wa baba huyo wa kutaka kukatisha ndoto za mwanawe.

Mitihani

Yusria anasema ana uhakika kuwa atafaulu kwa sababu alifanya vyema mitihani yake licha ya kuwa aliifanya akiwa katika wakati mgumu.

“Licha ya kusongwa na changamoto za baba yangu ambaye alitaka kukatisha ndoto zangu, lakini nina imani kuwa nitafanikiwa kufanya vyema. Namshukuru Mungu kwani nimefanya vizuri sana katika mtihani wa Hisabati na naamini kuwa   nitafaulu na kuingia kidato cha kwanza ili siku moja niweze kuifikia ndoto yangu yakuwa mwalimu kama si mama Samia Suluhu (Makamu wa Rais),”anasema Yusria.

Yusria anasema umekuwa ni utaratibu wake wa kila mwaka wa kujibu mtihani kwa kutumia dakika chache hali inayomfanya apate muda wa kujiridhisha na majibu yake kabla ya kuuwasilisha kwa msimamizi.

“Kwa wastani kwenye mitihani yangu nimekuwa nikitumia si zaidi ya saa moja, hii ni kwa sababu nafahamu vitu vingi.

“Huwa napenda sana kujisomea kwa sababu bado nina safari ndefu ya kutimiza malengo yangu.

“Baba yangu amekuwa akinisaidia kuhakikisha kwamba nasoma vyema, lakini nashindwa kuelewa ni kitu gani kilimpata mpaka akafikia hatua ya kutaka kukatisha ndoto yangu,”anasema.

Baba atoweka

Licha ya kwamba alitiwa nguvuni na vyombo vya usalama, lakini mzazi huyo alikimbia na kwenda kusikojulikana huku akitoa matamshi kwa mama mzazi wa mtoto huyo kuhakikisha kwamba anamchukua mwanawe kwani hataki tena kumuona.

Baba huyo pia alitelekeza pikipiki yake katika Kituo cha Polisi Mbagala Maji Matitu kwa kuhofia kukamatwa. 

Wanaomfahamu wamzungumzia

Watu mbalimbali wanaomfahamu baba huyo wanasema amekuwa ni mdau mkubwa wa maendeleo ya elimu shuleni hapo hadi kufikia hatua ya kujitolea kugharamia uchapishaji wa mitihani ya mazoezi ya wanafunzi kila mwisho wa wiki.

“Kwakweli sisi wenyewe jambo hili limetushangaza sana kwa sababu huyu mwenzetu ni mdau mkubwa wa elimu na hatujui kitu gani kilimpata,” anasema mmoja wa wakazi wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Salum Issa.

Mama mzazi

Mama mzazi wa Yusria, Aziza Sebarua, ambaye alitengana na mumewe miaka kadhaa iliyopita, anasema kitendo hicho kimemsikitisha hasa ikizingatiwa kuwa mwanawe ana uwezo mkubwa darasani.

“Mimi sifahamu ni jambo gani lililomkuta baba yake kwa sabbau licha ya kwamba tumetengana, lakini amekuwa akitimiza mahitaji yote ya mtoto wetu.

“Ila inanishangaza kuona kwamba amefikia hatua ya kumkana mtoto wake wa kumzaa kwa madai ambayo hayana msingi, mpaka kufikia hatua ya kukimbia akiwa mikononi mwa polisi huku akinitolea kauli za kwamba hatahusika tena na badala yake nitamlea mimi mwenyewe,”anasema mama huyo.

Anasema mwanawe ana uwezo mkubwa darasani na mara zote amekuwa akishika nafasi ya kwanza au ya pili tangu alipoanza darasa la kwanza.

“Kwasasa nahitaji apumuzike kidogo ili baadaye tuangalie namna gani atakavyosoma masomo ya awali kabla ya kuingia kidato cha kwanza, alikuwa hayuko tayari kupumzika, alitaka kuendelea na masomo mara tu baada ya kumaliza mtihani.

“Natamani sana kuona ndoto ya mwanangu ikitimia kwani amepitia changamoto nyingi, najua baba yake amechangia kumvuruga, lakini nina uhakika atafaulu na kufikia malengo yake,”anasema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Shule

Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Shule hiyo, Fatuma Kaisi, anasema jambo hilo limewasikitisha sana na kuiomba Serikali kunusuru elimu ya mtoto huyo.

“Hatujui ni kitu gani kilichomkuta baba yake mpaka akaamua kufanya ukatili wa namna hii kwa mtoto wake. Tunahisi amechanganyikiwa kwa sababu awali tulikuwa tukimuuliza kwanini alitaka kufanya ukatili huo akawa analia huku akisema kuwa hata yeye hafahamu kilichomtokea.

“Yusria ana kipaji cha kipekee kutokana na kufanya vyema kwenye mitihani mbalimbali, aliwahi kuongoza kwenye mtihani uliohusisha shule zote za kata, hakuna asiyemfahamu hapa kijijini na kata nzima, ndiyo maana kila aliyesikia taarifa za tukio hili alipigwa na butwaa kuona kwamba mtoto huyu anataka kukatishwa ndoto yake.

“Mtoto huyu amepitia mapito mengi, kuna wakati huwa anasingiziwa tuhuma za wizi jambo ambalo ni hatari sana hata akirudi kuishi na baba yake huyo, hivyo tunaomba watu wa ustawi wa jamii kuhakikisha kuwa mtoto huyu anaishi kwenye mikono salama,” anasema Fatuma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles