SIMU MPYA ILIYOUNDWA KWA VIPANDE VYA GALAXY NOTE 7

0
667

Na MWANDISHI WETU,

KAMPUNI ya mawasiliano ya Samsung imeanza kuuza simu nyingine ambazo inasema imetumia baadhi ya sehemu na vipande vilivyokuwa kwenye simu za Galaxy Note 7 zilizokumbwa na matatizo.

Simu hizo za Galaxy Note 7 zilikuwa zinashika moto na kulipuka kutokana na tatizo kwenye betri zake.

Kampuni hiyo imesema simu hizo mpya kwa Kiingereza Note Fan Edition zitapunguza athari za kimazingira kutoka kwa mabaki ya simu hizo ambazo ziliacha kuuzwa kutokana na hitilafu ilizokuwa nazo.

Simu hizo mpya zitauzwa Korea Kusini pekee na zitaanza kuuzwa  Julai 7.

Kampuni hiyo imesema simu hizo zitakuwa na betri ndogo ambazo ni salama zaidi kuliko zilizokuwa kwenye simu za awali.

Samsung iliacha kuunda simu za Galaxy Note 7, ambayo ilifaa kuisaidia kampuni hiyo kushindana na simu mpya za iPhone, mwishoni mwa mwaka jana baada ya kwanza kuwaomba wateja wazirejeshe zifanyiwe ukarabati lakini hatua hiyo haikufaulu.

Inakadiriwa kwamba simu 2.5 milioni zilirejeshwa kwa kampuni hiyo.

Simu hiyo mpya itakuwa na vipande kutoka kwa simu ambazo zilirejeshwa na wateja na vipande vingine kutoka kwa simu za Samsung ambazo hazikuwa zimeuzwa.

Betri ndogo na bei nafuu

Watetezi wa mazingira wamekuwa wakiishinikiza Samsung kutumia tena baadhi ya sehemu za Galaxy Note 7 ili kupunguza taka ambazo zingetokana na simu hizo.

Inakadiriwa kwamba simu 400,000 mpya zitaanza kuuzwa.

Bei yake itakuwa ni won 700,000 za Korea ($615; £472), ambayo ni asilimia 30 chini ya bei iliyokuwa ya Galaxy Note 7.

Simu hizo zitakuwa na betri za 3,200 mAh na Samsung wanasema betri hizo zimechunguzwa vyema.

Note 7 zilitumia betri za nguvu ya 3,500 mAh.

Simu za Samsung Galaxy Note 8, ambazo zitatolewa kuifuata Note 7, zinatarajiwa kuanza kuuzwa baadaye mwaka huu.

Betri kulipuka

Uamuzi wa kampuni hiyo ya simu kusitisha mauzo ya simu ya Galaxy Note 7 mwaka jana, kulikosababishwa na taarifa za kulipuka kwa betri zake ni hatua isiyokuwa ya kawaida kwa kampuni kubwa ya kiteknolojia.

Kampuni hiyo ilisema kwamba ilibaini kasoro iliyopo katika betri hizo lakini haikutoa maelezo zaidi.

Iwapo Betri ya Lithium-ion zinashika chaji haraka ni hatari mno kunapotokea kasoro kwa sababu huenda ikasababisha moto.

Mtaalam mmoja aliishauri kampuni hiyo kutafuta madini mbadala ya lithium.

”Nadhani tunapaswa kuwa na wasiwasi na kutafuta betri zilizo salama,”alisema mtaalamu wa kuhifadhi nishati Profesa Clare Grey kutoka chuo kikuu cha Cambridge.

Aliongeza: ”Hilo ni lengo zuri la utafiti na maendeleo viwandani.”

Mwaka jana, simu 35 za Galaxy Note 7 ziliripotiwa kushika moto duniani baada ya mauzo ya takriban simu milioni 2.5, hii ni kwa mujibu wa Samsung.

Betri za Lithium zinazotumika na Samsung hutumika zaidi katika viwanda vya kiteknolojia-Lakini ni nini kinachozifanya kuwa hatari?

Ni muhimu kujua vile zinavyofanya kazi. Betri hizo huwa na Cathode, Anode na Lithium.

Cathode na Anode huwa zimetawanywa na maji maji yanayoitwa Elektrolait pamoja na kifaa kilicho na mashimo madogo madogo kinachojulikana kwa jina la kitawanyishi.

Lithium hupitia kitawanyishi hicho ndani ya majimaji hayo.

Iwapo Betri inapata chaji haraka na kupata joto, Lithium huzunguka katika Anode ambayo husababisha moto.

Profesa Grey alisema kuwa kwa kawaida kuna eneo linalodhibiti chaji inayoingia katika betri hiyo. Betri huwekewa muda ili zisiweze kupata chaji kwa haraka. Hii ndio maana huchukua muda mrefu mtu anapochaji betri.

Lakini betri huanza kutoa ishara za kufura kabla ya kufeli kabisa kwa sababu seli zilizo ndani yake hufura na kupasuka lakini kufura huko hakutokei mara kwa mara.

Na iwapo haitafura utahisi joto lisilo la kawaida katika simu, lakini ukweli ni kwamba simu zetu huongeza joto wakati zinapotumika.

Hata hivyo, kampuni hiyo inasema kuwa unapohisi betri yako imeanza kuwa na joto itoe na ununue nyengine.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here