Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Wakulima wa mbogamboga katika Kata ya Kipunguni wamehamasishwa kujiwekea akiba ili waweze kununua simu za kisasa zitakazowawezesha kupata masoko kirahisi kwa njia ya mtandao.
Uhamasishaji huo umefanywa na Kikundi cha Sauti ya Jamii Kipunguni kinachojishughulisha na harakati za kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ambacho pia kinaiwezesha jamii kujikomboa kiuchumi.
Akizungumza wakati wa kuwapa elimu wakulima hao Mkurugenzi wa Sauti ya Jamii Kipunguni, Selemani Bishangazi, amesema kupitia kampeni ya ‘Siachwi Najichanga Nimiliki Simu Janja’ wanalenga kuwahamasisha wakulima kununua simu hizo ili kupata masoko kirahisi.
“Matumizi ya simu ni zaidi ya mawasiliano, hivi sasa teknolojia imekua kwahiyo mambo mengi yanafanyika kupitia mtandaoni, kwa shughuli zenu za kilimo cha mbogamboga mnaweza pia kufanya biashara mtandaoni na mkajiongezea vipato maradufu. Ndiyo maana tunawahamasisha muweke fedha kidogo kidogo muweze kumiliki simu janja,” amesema Bishangazi.
Mmoja wa wakulima ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wakulima Vijana Amani, Mwashabani Mohamed, amesema wazo la kuwa na simu janja ni zuri kwani litawasaidia kukua kibiashara.
“Mwanzoni wakati wa kipindi cha Corona kilikuwa kigumu sana tunatembeza mboga unafika unagonga nyumba ya mtu unaambiwa hawakaribishi wageni kwa sababu ya corona, lakini tukiwa na simu janja tunaweza tukafungua Instagram, WhatsApp, Facebook na mitandao mingine tukauza mboga na kupata wateja wengi,” amesema Mwashabani.
Mwashabani amewashauri wakulima wengine kujiwekea akiba waweze kununua simu janja kwani zitawarahishia kufanya biashara na kuepuka kutumia nguvu kubwa kutafuta wateja.
“Mpaka uanze kubeba mboga unatembeza mtaani mchicha, tembele lakini kwa simu janja unapiga picha mboga zako unawatumia wateja anachagua kisha unamfikishia, kwahiyo unakuwa hautumii nguvu kubwa,” amesema.
Amesema katika umoja wao wako wakulima 28 na kupitia kilimo cha mbogamboga wamenufaika kwa kumudu mahitaji yao ya msingi na kuepuka kuwa wategemezi kwa wazazi na walezi.