*Magdalena ang’ara kwa wanawake
*Wakata tiketi kushiriki mbio za Dunia
Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM
MWANARIADHA Alphonce Simbu amefanikiwa kung’ara kwa mara nyingine na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania, baada ya kushinda mbio za Standard Chartered Mumbai Marathon zilizofanyika jana nchini India.
Ushindi huo umemwezesha kukata tiketi ya kushiriki mashindano ya riadha ya Dunia yanayotarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu jijini London nchini Uingereza.
Simba alishinda mbio hizo kwa kutumia muda wa saa 2:09:32, huku mpinzani wake aliyeshika nafasi ya pili, Bahadur Singh Dhoni, kutoka India akimaliza kwa kutumia saa 2:19:51 na mshindi wa tatu Sanjith Luwang alikimbia kwa muda wa saa 2:21:19.
Ushindi huo umemwezesha Simbu kufuzu kwa kiwango cha daraja A katika mbio za Dunia zitakazofanyika jijini London, Uingereza pamoja na Mtanzania mwingine, Magdalena Crispian aliyeshika nafasi ya nne kwa upande wa wanawake akimaliza mbio za kilometa 31 kwa kutumia muda saa 2:34:51.
Kwa ushindi huo, Simbu amefanikiwa kupata kitita cha Dola za Marekani 67,000 (sawa na Sh milioni 149).
Katika kiasi hicho, Dola 42,000 zimetokana na ushindi alioupata katika mbio hizo, huku Dola 15,000 amepewa kwa ajili ya heshima ya ushiriki wake na Dola 10,000 zilitolewa kama ziada.
Akizungumzia mafanikio ya mwanariadha huyo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday, aliliambia MTANZANIA kuwa ushindi huo umewapa uhakika wa kuingiza wanariadha wawili katika mbio za Dunia mwaka huu.
“Simbu ameshinda mashindano makubwa yaliyopo kwenye orodha ya Jumuiya za mbio fupi na ndefu (AIMS), kwani amefanikiwa kupunguza muda wa dakika mbili ikilinganishwa na muda aliotumia katika mbio za Olimpiki zilizofanyika mwaka jana.
“Simbu na Magdalena wamefikia viwango vya daraja ‘A’ kwa ajili ya kushiriki mbio zinazosimamiwa na Shirikisho la Riadha la Dunia (IAAF) za ‘IAAF Track and Field’ ambazo mwaka huu zitafanyika London, Uingereza,” alisema Gidabuday.
Aidha, Katibu huyo alisema Simbu anatarajia kutua jijini Dar es Salaam leo akitokea India.
Katika taarifa aliyoitoa kwenye mtandao wa wadhamini wa mbio hizo, Benki ya Standard Chartered, Simbu alisema ushindi huo umetokana na kuzifanyia kazi mbinu alizofundishwa na kocha wake.
“Nilijiandaa vizuri, sikuogopa wala sikujali chochote kama ningekimbia kwenye milima au tambarare, lakini ushindi ndio ulikuwa kwenye malengo yangu,” alisema Simbu.
Safari ya mafanikio kwa mwanariadha huyo ilianzia katika michezo ya Olimpiki mwaka jana alipofanikiwa kumaliza nafasi ya tano kwa kutumia muda wa saa 2:11:15 katika mbio za marathon (km 42) zilizofanyika jijini Rio de Jeneiro, nchini Brazil.