WINFRIDA MTOI Na ASHA KIGUNDULA – DAR ES SALAAM
TIMU ya Yanga imeondoka jijini Dar es Salaam kwenda mkoani Mara, ambako itakabili Biashara United, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Uwanja wa Karume mjini Musoma.
Kwa upande mwingine, wapinzani wa Yanga, timu ya Simba nayo iliondoka jana hiyo hiyo jijini humo kwenda mkoani Mtwara, kwa ajili ya mchezo waje na Ndanda utakaochezwa Uwanja wa Nangwanda, Sijaona.
Timu hizo kila moja itacheza michezo miwili zikiwa huko kwa maana ya Yanga Kanda ya Ziwa na Simba Kanda ya Kusini.
Yanga baada ya kuivaa Biashara United, Wanajangwani hao wataelekeaBukoba, kuikabili Kagera Sugar dimba la Kaitaba.
Simba ikimalizana na Ndanda itasafiri hadi Lindi ambako itapepetana na Namungo Uwanja wa Majaliwa.
Baada ya mchezo na Namungo, Wekundu hao litafuatia tukio la Wekundu hao kukabidhiwa kombe la ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
Simba imefanikiwa kutwaa ubingwa huo, baada ya kufikisha pointi 79 katika michezo 32, licha ya kusaliwa na michezo sita kabla ya msimu kufikia tamati.
Kigezo kilichoipa ubingwa ni washindani wengine 19 wanaoshiriki ligi hiyo kutokuwa na uwezo wa kufikisha pointi hizo, hata kama watashinda michezo yao yote waliyobakiwa nayo.
Baada ya ziara zao Kanda ya Ziwa na Kusini, Simba na Yanga zitarejea Dar
es Dalaam kabla ya kuumana Julai 12 katika pambano la nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania maarufu Kombe la Azam(ASFC).
Meneja wa timu ya Yanga, Abed Mziba, alisema wameondoka na wachezaji 24, akiwemo Bernard Morrison huku walibaki Dar es Salaa ni wale majeruhi kama Papy Tshishimbi.
Alisema Morrison ameambatana na wenzake baada ya kumaliza tofauti kati yake na klabu hiyo ikiwemo kuwaomba msamaha wachezaji wenzake.
“Timu imeondoka na wachezaji 24, mechi tulizonazo ni ngumu tunahitaji kuwa na kikosi kipana, waliobaki Dar es
Salaam ni wa majeruhi pekee,”alisema Mziba.
Naye Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema wamesafiri na kikosi chao chote kwakua wakiwa Ruangwa mkoani Lindi watakuwa na hafla ya makabidhiano ya kombe.
Alisema wameelekea Kusini wakiwa na vitu viwili vya kufanya, kuhakikisha wanachukua pointi zote sita na kusherehekea ubingwa wao.
“Tumeondoka Dar es Salam alifajiri, wachezaji wote wapo katika hali nzuri, tuko tayari kwa mapambanpoi pamoja na sherehe zetu za kukabidhiwa kombe,” alisema Rweyemamu.