31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBACHAWENE AZINDUA KLINIKI INAYOTEMBEA

Na RAMADHAN HASSAN-MPWAPWA


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene, amefungua mpango maalumu wa kliniki tembezi wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, wenye lengo la kutoa huduma za matibabu kwa wananchi.

Pia, amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya nchi nzima kupeleka huduma za matibabu hayo karibu na wananchi ili kuepuka gharama kubwa za matibabu.

Uzinduzi wa kliniki tembezi ambao ulihusisha madaktari bingwa mkoani Dodoma, ulifanyika juzi katika Hospitali ya Benjamini Mkapa iliyoko wilayani hapa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Waziri Simbachawene alisema huduma hiyo imekuwa ikipunguza gharama za matibabu na kwamba madaktari wana wajibu wa kuhakikisha wanawafikia wananchi. 

Pia, alizitaka halmashauri zote nchini kusogeza huduma za matibabu karibu na wananchi ili matatizo yao yaweze kutatuliwa.

“Niwaombe wakuu wa wilaya na mikoa nchini, kwamba msaidie ili hizi huduma ziweze kuwafikia wananchi walio katika maeneo yenu,” alisema Simbachawene.

Kwa upnde wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. James Kiologwe, alisema Mkoa wa Dodoma umejipanga kutoa huduma za matibabu ya uhakika kwa gharama nafuu na kwamba mpango huo utaendelea katika wilaya zote za mkoa huo.

“Tumejipanga kutoa huduma hizi katika wilaya zote za Mkoa wa Dodoma na lengo letu ni kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wenye matatizo,” alisema Dk. Kiologwe.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabiri Shekimweli, alisema wananchi wilayani Mpwapwa wameipokea vizuri huduma hiyo na wanaamini itakuwa na manufaa kwa wakazi wa Mpwapwa

Naye Nelly Kaguli, mkazi wa Mpwapwa, alisema kupitia huduma hiyo, imewawezesha kupata matibabu kwa ukaribu na kuiomba Serikali kufanya zoezi hilo kuwa endelevu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles