30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Simbachawene awaonya wakimbizi makazi ya Katumba, Mishamo

Na Walter Mguluchuma-Katavi 

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amewaonya wakimbizi wanaoishi kwenye makazi ya Katumba na Mishamo mkoani Katavi na wale waliopewa uraia wa Tanzania kuacha kujihusisha na vitendo vya siasa wakiwa kwenye makazi hayo.

Alitoa maagizo hayo jana alipokuwa akiwahutubia katika mkutano wa hadhara wananchi wanaoishi kwenye Kambi ya Wakimbizi ya Mishamo wilayani Tanganyika mkoani Katavi.

Alisema kuna baadhi ya wakimbizi wa Burundi  na wale waliokuwa raia wa nchi  hiyo na kupewa uraia wa Tanzania wanaoishi kwenye Makazi ya Wakimbizi ya Katumba na Mishamo wamekuwa wakijihusisha na kufanya sisa za vyama vilivyoko Burundi huku wakiwa ndani ya makazi hayo.

“Wale ambao wamekuwa wakijihusisha kutengeneza magenge ya uhalifu kwa kufanya ujambazi, ujangili na kumiliki silaha kinyume cha sheria watambue kuwa shughuli hiyo haina tija kwao.

“Watakaobainika kufanya hivyo watarudishwa mara moja kwenye kwenye nchi yao kwani sheria hiyo ipo na kwa wale waliopewa uraia wa Tanzania utafutwa,” alisema Simbachawene.

Alisisitiza kuwa mahusiano ya Tanzania na Burundi ni mazuri na wanaotaka kuleta chuki zao watambue  wanapoteza muda huku akitahadharisha watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Simbachamwene alisema wanaofanya uhalifu watarudishwa nchini mwao na kwamba watambue kuwa wanawaponza hata wenzao ambao ni wema.

 Aliwataka waisaidie Serikali kwa kuwafichua wale wanaotaka kufanya siasa za Burundi wanapokuwa kwenye makazi hayo na wale wanaotaka kufanya vitendo vya uhalifu.

“Hakikisheni mnatoa taarifa kwa Serikali mara moja kwani vitendo hivyo vitawafanya mchelewe kupatiwa huduma muhimu kwenye makazi yenu,” alisema.

Aidha aliwaonya waache tabia ya kukataa makabila yao kwani wapo baadhi yao wamekuwa wakijiita wao ni Wasukuma  na wengine wamekuwa wakijiita kuwa ni Waha wakati Serikali inatambua ni Wahutu na Watusi.

Naye Mkuu wa Makazi ya Wakimbizi ya Katumba, John Mwita, alisema baadhi ya raia wanaoishi kwenye makazi hayo wamekuwa na tabia ya ubaguzi  unaotokana na sehemu wanazotoka, dini na tofauti za kisiasa za vyama vilivyopo Burundi.

Alisema kwenye makazi ya wakimbizi kumekuwa na changamoto ya kukinzana kwa sheria kutofautiana baina ya sheria za wakimbizi na zile za Serikali za Mitaa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera, alisema mkoa huo umekuwa ukifanya operesheni mbalimbali kwenye makazi hayo na kwamba wamefanikiwa kukamata zaidi ya silaha 100 zikiwemo za kivita.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles